Makbuus Dajaaj/ Machbuus ya Kuku (U.A.E)
Makbuus Dajaaj/ Machbuus ya Kuku (U.A.E)
Vipimo
Mchele wa Basmati - 4 vikombe
Kuku (mkubwa kiasi) - 1 (wa Lb 6 -7)
Vitunguu vilivyokatwakatwa - 3
Samli - 4 vijiko vya supu
Buharaat (bizari ya Machbuus) - 2 vijiko vya supu
Bizari ya manjano (haldi/tumeric) - 1 kijiko cha chai
Nyanya zikizomenywa na kukatwakatwa - 3
Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa - 2 vijiko vya supu
Loomi (ndimu kavu) au ya unga - ½ au ½ kijiko cha chai
Mdalasini kijiti - 1
Karafuu nzima - 3
Hililiki nzima - 4
Maji - 5 vikombe
Kotmiri iliyokatwakatwa - ½ kikombe
Chumvi - kiasi
Vipimo Baharaat (Binzari)
Baharaat – Bizari ya Makbuus
Pilipili Manga - ½ kikombe
Gilgilani (Corriander seeds) - ¼ kikombe
Mdalasini vijiti - ¼ kikombe
Karafuu - ¼ kikombe
Bizari ya pilau (cumin seeds) -1/3 kikombe
Hiliki - 2 vijiko vya chai
Paprika ya unga - ½ kikombe
Namna Ya Kutayarisha Baharaat (bizari)
- Chambua hiliki utoe kokwa zake, kisha tia vitu vyote katika mashine ya kusagia (grinder) usage hadi iwe unga.
- Changanya na Paprika bizari ikiwa tayar.
- Ihifadhi katika chupa yenye mfuniko wa kubana vizuri.
Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Makbuus
- Osha na roweka mchele kwa muda kiasi.
- Msafishe kuku, mkate vipande vinne weka kando.
- Katika sufuria ya kupikia, tia samli, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (brown). Tia baharaat na bizari ya manjano, kaanga kwa dakika moja hivi.
- Tia vipande vya kuku, chumvi, thomu, punguza moto na umkaange kuku katika masala ya vitunguu.
- Tia nyanya, karafuu, loomi, mdalasini, hiliki, changanya vizuri na endelee kukaanga.
- Tia maji (inategemea mchele unaotumia, huenda ukahitaji zaidi). Funika na pika kwa muda wa dakika 20-25.
- Mwaga mchele maji uliyorowekea, mimina mchele katika supu, tia kotmiri, changanya vizuri, funika uchemke mchele, punguza moto na pika wali kama inavyopikwa pilau ukoroge mara moja au mbili tu.
- Ukishaiva wali, pakua katika sinia/sahani na weka vipande vya kuku juu katikati ya wali.
Kidokezo:
- Ukipenda badala ya kupika wali katika sufuria baada ya kutia mchele na kukaribia kuiva, na kabla ya kukauka supu yote, mimina katika treya ya jalbosi (Treya ya foil) upike ndani ya oveni (bake) kwa mtoto wa takriban 400-450º kwa muda wa dakika 20-25.
- Baharaat hiyo inatumiwa katika vyakula vya nchi za Kiarabu (Gulf States), hivyo unaweza kutumia kupikia machbuus ya vitoweo vingine kama nyama na samaki na vyakula vinginevyo kama michuzi n.k.