Zingatio: Rafiki Muovu

 

Zingatio: Rafiki Muovu

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni kawaida ya mwanaadamu kuathirika na kile kilicho mbele yake. Ndio sababu ukakuta kuna makundi ya watu wa umri tofauti. Watoto watacheza na watoto wenzao, vijana watajumuika na vijana wenzao, wazee nao wataketi barazani pamoja na wazee wenzao.

 

 

Ni nadra kuwakuta watoto wakijumuika pamoja na wazee katika mambo ya faragha. Kama ukiwakuta vijana pamoja na wazee itakuwa ni kwa sababu na tena kwa wakati maalum tu, kwani hilo sio kawaida ya wanaadamu.

 

 

Halikadhalika kwa upande wa utaalamu wa kazi. Binaadamu hukutana kwa kufanya usuhuba wa pamoja. Wafanyabiashara wataongea na wafanyabiashara wenzao, wakulima na wakulima, rubani na rubani na wengineo mfano wa hao.

 

 

Vivyo hivyo kwenye khulqa za watu. Mganga mshirikina utakuta ana wateja wake wenye kumshirikisha Rabb Aliye Mmoja Asiyestahiki kushirikishwa. Mnywaji pombe utakuta anapatana bei ya kreti ya pombe pamoja na muuza pombe. Mtoaji rushwa swahiba wake mkuu ni mpokeaji rushwa. Mdhulumu wa haki za watu anasaidiana kazi na wale wasiochunga haki za watu.

 

 

Katu Muumini hakubali kuchanganyika na mshirikina. Wala haijuzu kwa mwenye kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenye kuchunga mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuwa chanda na pete pamoja na mwenye kumuasi Rabb Mlezi. Naye Allaah Anasema (tafsiri):

 

الزَّانِي لَا يَنكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لَا يَنكِحُهَا إِلَّا زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ ۚ وَحُرِّمَ ذَٰلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ﴿٣﴾

Mwanamme mzinifu hafungi nikaah isipokuwa na mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina; na mwanamke mzinifu haolewi isipokuwa na mwanamme mzinifu au mshirikina. Na imeharamishwa hivyo kwa Waumini. [Al-Nuwr: 3]

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: "Tangamana na watu wema wa pole, utakuwa mmoja wao; na epukana na watu waovu usalimike na maovu yao."

 

 

Kwa hakika Qur-aan imethibitisha kwamba kila mtu atakutanishwa pamoja na mwenziwe siku ya Qiyaamah. Muovu kwa muovu na mwema kwa mwema. Pazia la ubaya wa kushirikiana pamoja kwenye maovu Siku hiyo litaondoshwa. Rabb Mlezi Atasema (tafsiri):

                

أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ﴿٢٤﴾ مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ﴿٢٥﴾ الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ﴿٢٦﴾

(Allaah Atasema): Mtupeni katika Jahannam kila kafiri mno, mkaidi! Mzuiaji wa kheri, mwenye kutaadi, mtiaji shaka. Ambaye amefanya mwabudiwa mwengine pamoja na Allaah, basi mtupeni katika adhabu shadidi. [Qaaf: 24-26]

 

 

Allaah Anaendelea kutupasha habari ya vioja vya Siku ya Qiyaamah kwa wale maswahibu waliosaidiana kwenye maovu. Kila mmoja atamlaumu mwenziwe:

 

قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَـٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ﴿٢٧﴾

Shaytwaan mwenzake atasema: Rabb wetu! Sikumvukisha mipaka kuasi lakini alikuwa (mwenyewe) katika upotofu wa mbali. [Qaaf: 27]

 

Rabb wa Mbingu na Ardhi Atawajibu (tafsiri): 

 

قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ﴿٢٨﴾ مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴿٢٩﴾

(Allaah) Atasema: Msikhasimiane Kwangu, na hali Nilishakukadimishieni onyo Langu! Haibadilishwi kauli Kwangu, Nami si mwenye kudhulumu waja. [Qaaf: 28-29]

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja wake wema na Atupe katika marafiki ambao watatuepusha na ghadhabu Yake, na watakotuelekeza kwenye njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na Radhi Zake, Aamiyn.

 

 

Share