Mtu Anapokuwa Karibu Na Kufariki Huwa Anaona Dalili Kabla Ya Siku 40?
Mtu Anapokuwa Karibu Na Kufariki Huwa Anaona Dalili Kabla Ya Siku 40?
SWALI:
Assalam alaykum warahmatu llah wabarakat amma baada yak kumshukuru allah subhanahu wataala na kumtakia rehma mtume wetu Muhammad swalla llahu alaih wassalam tunawashkuru sana ndugu zetu wa alhidaya kwa kutufunza mengi inshaallah Allaah atawapa kila la kheri dunian na akhera kuna mtu nilimsikia kuwa eti mtu akitaka kufa hujijua siku 40 kabla na dalili alonitolea kuwa hungara paji lake la uso jasho lake la mwili hubadilika huona haya kumuangalia mtu na pia ndoto anazoota humfanyisha ajue kuwa anakaribia kufa je hii kweli maanake sina uhakika nataka nijue
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakika suala hili la siku arobaini halijathibiti katika chanzo chochote kile cha Sheria. Na mas-ala haya ya mtu kujua siku yake ya kufa ni miongoni mwa mambo matano ambayo hakuna ayajuaye, na hata Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) hakuwa na elimu nayo. Anayataja Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾
Hakika Allaah Ana elimu ya Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi, na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Luqmaan: 34]
Ama pale mtu mwema anapotolewa roho yake, Malaika humbashiria mambo mema lakini hakuna anayejua au kuyasikia isipokuwa yeye mwenyewe. Dalili tunapata kutokana na kauli mojawapo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾
Hakika wale waliosema: Rabb wetu ni Allaah. Kisha wakathibitika imara; Malaika huwateremkia: (kuwaambia): Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa. Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba. Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Fusw-swilat: 30-32]
Baadhi ya makundi kama Masufi wao huamini kuwa mtu mwema ambaye ana makarama anaweza kujua siku yake anayoaga dunia. Hii ni ‘Aqiydah potofu na isiyopasa kabisa kuaminiwa, na ni sawa na ‘Aqiydah potofu ya Mashia ya kuamini kuwa Imaam wao wanajua watakufa lini na kifo watakachokufa!
Na Allaah Anajua zaidi