Amefunga Ndoa Isiyokubalika Kisheria Vipi Kuhusu Ibada Zake?

SWALI:

 

Asalaam alaykum warahmatullah wabarakatuh

Je ni vipi mtu atekeleze ibada ya funga na swala wakati amefunga ndoa ambayo haikubaliki ktk uislam. Lakini bado ni muislam na anatekeleza mengi tu katika uislam.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa isiyokubalika kisheria. Hata hivyo, swali lako haliko wazi. Hii ndoa ilifungwa namna gani hata isikubalike. Ikiwa imefungwa makosa aliyefungishaa ni nani? Ikiwa imefungwa kimakosa wajuzi wamefanya nini ili kurekebisha hali hiyo? Je, wanandoa wanajua kuwa ndoa yao si halali kisheria au vipi?

 

Ikiwa ndoa hiyo ina makosa ni kurekebisha makosa haraka iwezekanavyo, nawe unatakiwa uwe msitari wa mbele katika hilo kwani inaonekana wewe ni mjuzi katika jambo hilo. Ikiwa wanandoa walikuwa hawajui kuhusu hilo watakuwa kisheria hawana makosa, lakini ikiwa wamefanya makusudi basi watakuwa na madhambi. Ibadah ya Swalah na Funga inatekelezwa vile vile kama wanavyotekeleza Waislamu wengine bila ya tofauti yoyote ile. Tofauti itakuwa katika thawabu na ujira wa kutoka kwa Allaah Aliyetukuka, kwani atakuwa anapata thawabu ya matendo hayo na kupata madhambi kwa kuzini.

 

Kuhitimisha ni kuwa ni wajibu kwa wajuzi kuweza kuwapatia nasaha hao wanaoishi hivyo ili watoke katika madhambi na wasiruke patupu kwa Ibadah wanazofanya.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share