Mama Anataka Talaka, Baba Hataki Kutoa Hadi Waweko Kaka Zake, Ni Lazima Kuweko Shahidi Ili Itolewe Talaka?

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatullahi wabarakatu nawashukuruni sana kwa kujibu maswali yetu mbali mbali na inshallah mungu atawazidishia wepesi wa kila kitu kwa kutuelewesha watu kama sie tosojuwa dini vizuri inshallah...

swali langu la leo ni kwamba mie baba yangu na mama yangu wako katika ugomvi na kwa sasa hawaishi pamoja kwa muda kama sikosei ni miezi saba sasa. Sasa mama yangu akaniambia kama anataka kudai talaka kwani baba yangu kamdhulumu sana katika maisha yake, akamwambia baba yangu kama anataka talaka ila baba yangu akamwambia kama unataka talaka siwezi kukupa mpaka uwaambie kaka zako waje na tuongelee vizuri kwani sijakuokota barabarani, sasa mama akawaambia kaka zake ila kaka zake wamekataa kwani wanasema wanaogopa dhambi, sasa mie sijaelewa inakuwaje watapa dhambi ikiwa mama mwenyewe anataka talaka? Sasa naomba mnieleweshe vizuri shukran


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka. Mara nyingi sana tumezungumzia sana kuhusu matatizo ya kindoa na kijamii ambayo yanaleta matatizo mengi zaidi katika maisha yetu hapa ulimwenguni. Hii inatokea kwa sababu mara nyingi katika ndoa zetu huwa hatuchaguani kwa misingi ya Dini bali huwa tunachaguana kwa sababu nyingi nyingenezo. Kwa ajili hiyo huwa tunakumbana na changamoto nyingi katika suala la ndoa na wanandoa.

 

Ama kuhusu suala la talaka zipo njia nyingi ambazo kwayo talaka hutolewa. Na kwa kuwa Uislamu ni njia kamili ya maisha imetupatia muongozo kuhusu hilo kwa hiyo shida kama hizo huwa kwa hakika si tatizo wala shida. Katika mas-ala haya ya talaka huwa ni ya upande wa kuumeni ila kwa nyakati nyingine inapitia kwa Qaadhi. Kwa hakika ni makosa kwa wanandoa kuishi mbali mbali kwa muda huo mwingi wa miezi saba bila kuvunja ndoa kama hiyo. Ilikuwa ni wajibu wa mama alipoona kuwa anadhulumiwa afuate mwelekeo ufuatao ili kupata suluhisho:

1.      Azungumze na mumewe kuhusu hayo matatizo na dhuluma kama zipo na kumpatia mume wakati wa kujirekebisha.

2.      Hakufaulu katika hilo, basi ilikuwa hana budi ila kuita wawakilishi kutoka upande wake, upande wa mume na mume mwenyewe aweko. Na hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha kuwa lau wanataka islahi basi wataifikia bila ya tatizo lolote.

3.      Ikiwa hakukupatikana ufumbuzi wa aina yoyote ile itambidi yeye aende kwa Qaadhi au Shaykh anayeshughulikia mambo ya Waislamu katika mji au kijiji. Qaadhi au Shaykh baada ya kusikiliza kila upande atatoa uamuzi kulingana na sheria ya Kiislamu.

 

Suluhisho kwa sasa kwa sababu baba na mama wapo mbali mbali ni kuitisha kikao kama anavyotaka baba. Sasa ni jukumu lako kuwaelezea wajomba zako (kaka zake mamako) kuwa wao hawana dhambi kwani ndio agizo la Uislamu wao kuhudhuria. Pia huenda wao wakawa sababu ya baba yako na mama yako kurudiana na kuishi pamoja kwa sababu ya baba kutoa ahadi ya kujirekebisha.

 

Tunawaombea wanandoa hao wawili waweze kusuluhisha tatizo hilo kwa kurudiana au kuachana.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share