Inafaa Kuwatolea Salaam Mashia Na Kuswali Nao?
Inafaa Kuwatolea Salaam Mashia Na Kuswali Nao?
SWALI:
Asalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh, Kwanza nawashukuru kwa jitihada zenu za kutujibu maswali yenu pamoja na kuwa maswali ni mengi, Nawaombea Allah Subhaanahu Wa Taala awazidishe ujuzi, elimu na subra ili mzidi kutuelemisha sisi ndugu zenu zaidi.
Mimi ninatokea Afrika Mashariki na Alhamdulillah nimejaaliwa kupata kazi nchini Oman. Katika huu mji ninapofanya kazi, asilimia kubwa ya wakaazi ni dhehebu la Shia, sasa maswali yangu ni je:
1. Inafaa kuwatolea salam au kuitikia salam zao maana huku kila mtu hutoa salaama ya 'Asalaam aleikum' na huwezi jua nani sunni na nani shia.
2. Hapa kazini tunatumia chumba kimoja kufanyia ibada, ina maana na watu wa shia huswali humo humo ila huja na miswala yao yenye vipande vya mawe, je inafaa kusali pamoja nao?
Nawataka radhi kwa kuwa sikujua category halisi ya swali hili ila natumai Inshaallah mtajaaliwa kunipa majibu kwa manufaa yangu na ya ndugu zangu wengine waislam.
Asalaam Aleikum
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Ama kuhusu suala hilo la kutoleana salamu na Mashia ni kuwa ikiwa huwezi kujua nani Sunni na nani Shia utajibu salamu ya kawaida ya Kiislamu.
Na ikiwa una uhakika kuwa huyo ni Shia na anaonyesha uadui wake wazi kwa kutukana Maswahaba na kuwakufurisha, na kuwatukuza kupita kiasi ‘Aliy, Faatwimah, Al-Husayn n.k. na kufanya shirki zao za kuamini kuwa maimamu wao wanajua ghayb na wana uwezo wa kuwasaidia wao zaidi ya Allaah na kuwa wao ni bora kuliko Mitume na mengineyo kama hayo, basi haifai moja kwa moja kutoleana nao salaam na hata kuswali nyuma yao na hata Maulamaa wameona kuwa wako kwenye shirki kubwa na hata kula vichinjo vyao haifai.
Lakini hata hivyo, tujue pia kuna Mashia wasio Ithna’ashariyah kama wale walioko Yemen ambao ni Shia Zaydiyah, wao ni kinyume na hawa ithna’ashariyah ambao wamezagaa Afrika Mashariki na Mashariki ya kati. Hao Zaydiyah hawatukani wala kukufurisha Maswahaba.
Ama kuhusu swali lako la pili ni kuwa Swalah zetu zinatofautiana na Swalah wanaoswali Mashia, hivyo inavyohitajika ni nyie kama Masunni hapo mswali jama’ah yenu au mmoja wenu awe ni Imaam kuwaswalisha wote. Ikiwa Imaam atakua Mshia basi msiswali nyuma yake, itabidi mngoje mpaka amalize kisha ndio mswali nyinyi jama’ah yenu, au kama kuna nafasi pembeni au pengine mswali jama'aah yenu na mjitenge nao.
Wala isiwahadae baadhi ya nyakati kuona Shia anaswali nyuma yenu, wao hufanya hivyo kwa taqiyyah, na baada ya hapo huirudia Swalah yao.
Rejea makala zilizomo katika tovuti uone kauli kali za Maimaam wanne na Maimaam wengine wakubwa wa Ummah huu walivyosema kuhusu Mashia.
Na Allaah Anajua zaidi