Mwanamke Asiyeolewa, Je, Shari’ah Inamkataza Asikate Nywele Zake?
Mwanamke Asiyeolewa, Je, Shari’ah Inamkataza Asikate Nywele Zake?
SWALI
Assalam ALaykum.
Swala: mimi ni binti wa kisilamu ambaye sijaolewa na bado naishi na wazazi wangu.. Nataka kupunguza nywele kwa sababu nywele zangu zinakatika sana au kukata kistyle but wazazi wangu wananikataza. Je katika dini ye2 ya kislam imekatazwa bint ambaye hajaolewa asikate nywele na kama imekatazwa kwa nini? Na nnaomba nipewa aya yoyote iliyo sema hivyo.. Walaykum Salaam.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakika ni kuwa hukumu ya kukata nywele kwa mwanamke ni sawa ikiwa ameolewa au hajaolewa. Shari’ah ya Kiislamu imemtaka mwanamke awe ni mwenye kubakisha nywele zake asiwe ni mwenye kuzikata kabisa kwani hilo limekatazwa.
Kile ambacho ameruhusiwa ni kukata kidogo. Na hilo ni kwa mujibu wa Hadiyth iliyopokewa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kunyoa nywele si jukumu lililowekewa wanawake; kukata kidogo ndivyo inavyotakiwa” [Abu Daawuud]. Na Hadiyth nyingine kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wanawake (mahujaji) hawafai kunyoa (vichwa vyao); wanaweza tu kupunguza nywele zao” [Abu Daawuud]. Ibn al-Mundhir amesema: “Yapo maafikiano miongoni mwa wanachuoni kuhusu hili, kwa kuwa kunyoa nywele za kichwa cha mwanamke ni aina ya adhabu”.
Kwa maelezo ya hapo juu ni wazi kuwa mwanamke hafai kunyoa kabisa lakini aweza kukata kitu kidogo katika nywele ama kukata kimitindo kama ulivyosema hilo halifai kabisa kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hilo. Na pia katukataza vilevie kuwaiga makafiri katika mambo yao. Na ukitazama mitindo mingi ya nywele na mavazi inaanzia kwa makafiri.
Na Allaah Anajua Zaidi