Urithi Wa ‘Ami Yetu Unatumiliwa Na Nduguze, Watoto Hawapati Kitu, Je Sisi Tuwalipe Watoto Hao?

SWALI:

 

Assalamu aleikum warahmatullahi wabarakatuh ramadhan mubarak

Mimi swali langu ni kua ami yangu alifariki miaka 3 nyuma kawacha mali yake nyengine kwa ndugu yake wa kiume, na vyombo vyake kwa ndu yake wa kiume mwengine, pamoja na urithi wa wazee wake hajaupata walipofariki. Na kawaacha watoto 8 na wake wawili. Urithi huo mpaka leo tunawakumbusha hawa wazee waulipe na wawagawanyie watoto hao na wake zake bado kila siku zikienda hawana mali hio ya kuwalipa na wakiwa nazo wanazitumia, jee tunaweza sisi wengine kuwalipia hawa watoto au munatushauri vipi tufanye?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu urithi.

Hakika ni jambo ambalo halitarajiwi kuwa watoto na wake za aliyefariki watanyimwa urithi wao kwa sababu ya ‘Ami zao ambao wamekatalia nao kwa ujeuri tu. Ukweli ni kuwa hilo ni deni juu ya migongo yao na lau watakufa katika hali hiyo basi watapata matatizo mengi sana.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema yafuatayo kuwaamuru jamaa waliobaki:

 

Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa” (4: 2).

 

Inatakiwa hao ‘Ami wafahamu kuwa wenye kula mali ya mayatima wana adhabu kali,

 

Hakika wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni” (4: 10).

 

Inatakiwa mwanzo mzungumze na hao ‘Ami kwani kuwaacha hivyo watakuja kuwadhulumu na wengine na hiyo itazidisha kuwafanya wao wadhulumu. Ikiwa imeshindikana inatakiwa muwapeleke kwa Qaadhi wa sehemu yao ili kuondoa dhuluma na kuwa funzo kwa wengine. Na lau itashindikana basi nyinyi mnaweza kuwasaidia hao mayatima waweze kujikimu kimaisha pamoja na mama zao na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atawalipa kwa yote hayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share