Kudai Haki Ya Warithi Waliodhulumiwa.

SWALI:

 Katika uhai wake, kaka yangu alimiliki shamba ambalo lilivamiwa na watu wa jirani waliotaka kumiliki shamba hilo kinyume na taratibu za nchi. Kwa vile kaka yangu alikuwa na warka wa kumiliki shamba hilo, wavamizi hawakupata haki ya kuendelea kulima kama walivyokusudia. Hata hivyo, kaka yangu aliwaahididi wavamizi hao kuwalipa shilingi 25,000/= kwa kila eka waliyolima kwa madhumuni ya kudumisha mahusiano mema. Kaka yangu alifariki siku chache tu baada ya kuwaahidi hivyo.

Hatua niliyochukua ni kukutana na wale wavamizi na kuwahidi kuwa ningetekeleza nia ya aliyefariki kaka yangu kwa madhumuni yale yale aliyowaambia, ya kudumisha mahusiano mema.

Kitu cha kusikitisha, wale watu wakafanya ulaghai wa kujifanya ni wamiliki wa shamba lile na wakauza sehemu ya shamba la aliyefariki kwa mtu mwingine. Nikiwa msimamizi mkuu niliyeteuliwa kusimamia mirathi ya aliyefariki, nimelazimika kugharimia wakili wa kudai haki ya watoto na mke wa aliyefariki.

 Kwa mujibu wa sheria zinazotawala mikataba hapa duniani, kitendo cha watu wale kuuza sehemu ya shamba kwa mtu mwingine kwa njia za hila ni ukiukwaji wa makubaliano ya kudumisha mahusiano mema ambayo ndiyo msingi mkubwa uliomsukuma aliyefariki kuahidi kuwalipa, ingawa hakuwa na wajibu wa kufanya hivyo.

SWALI: Je, kwa mujibu wa uislam na Kur'an tukufu, bado ninao wajibu wa kutekeleza ahadi hiyo? Iwapo sitaitekeleza ni nini hukumu yake?

Wabillah tawfiq

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu aliyouliza swali lake hili. Hili ni miongoni mwa matatizo mengine ya kijamii kwa watu kuwa na ujasiri wa kuvamia mali za watu na kutokuwa na khofu kwa Allaah. Uvamizi aina hiyo ni dhulma na jambo hilo halikubaliki katika nchi yoyote ile yenye ustaarabu na ubinaadamu.

Haiwezekani kwa mtu kukurupuka na kuvamia ardhi ya mwingine bila ya idhini. Allaah Amuweke pema kaka yako kwani inaonyesha alikuwa mtu mwema mpaka akaonelea atatutue mzozo huo kwa kuwapatia wavamizi pesa ambazo si haki yao.

Hakika ni kuwa ahadi ni miongoni mwa mambo ya msingi katika Uislamu ambayo yanafaa yatekelezwe. Kutofanya hivyo kunamuingiza mtu mwenyewe katika unafiki. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) naye Anatuelezea umuhimu wa kutekeleza ahadi pale Aliposema: “Enyi mlioamini! Tekelezeni wajibu wenu (ahadi)” (5: 1).

Hatua uliochukua ndugu yetu ili kuweza kuondoa mzozo huo kwa njia ya kuwanyia wema pia ni nzuri lakini inaonyesha kuwa hao watu hawana nia nzuri baada ya wema huo wote. Pia ni ajabu kuwa wavamizi waliachwa mpaka wakakita mizizi yao katika ardhi isio yao.

Kuchukua wakili muadilifu na muaminifu ni miongoni mwa jambo jema ulilofanya. Hiyo ni kuwa Uislamu unatuhimiza sana kuwa tuwe ni wenye kutetea haki zetu kwa njia zote za halali zinazohitajika. Ili liwe funzo kwa wengine ikiwa mtashinda kesi hiyo nasi tuna imani kuwa kwa sababu mko katika haki mutakuwa ni wenye kushinda inshaAllaah. Inabidi hao wavamizi wasio na adabu wafundishwe ustaarabu kwa kutiwa adhabu. Hisani kama hiyo mliyoifanya haipatikani kabisa katika dunia hii lakini hao watu ni watovu wa wema mliowafanyia. Nasaha zetu kwenu ni kuwa nyinyi msivunje ahadi yenu. Pindi mtakaposhinda muwe ni wenye kuwalipisha gharama mlizotumia za wakili. Watakapolipa gharama hizo basi mnaweza kuendelea kuwapatia zile pesa walizoahidiwa na kaka yako za shilingi 25,000.

Kufanya hivyo inshaAllaah itawafundisha wavamizi wengine wasiwe ni wenye kucheza na mali za watu bila ruhusa ya wenyewe. Tunaonelelea uendelee kufanya hivyo kwa kuwalipa mlioahidi lakini hayo yawe baada ya kesi na wao kulipa gharama hizo za kesi yako. Hii ni njia moja ikiwa watu wenyewe si Waislamu kuwavutia katika uzuri na wema wa Uislamu. lau watu wenyewe watakuwa ni Waislamu basi wajirudi, watubie, watengeneze maadili yao na wawe Waislamu wema na wazuri.

Tunakutakia kila la kheri katika kesi yako hiyo, muwe na mafanikio na kila mmoja apate haki yake inshaAllaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share