Hukmu Ya Wadii Na Madhii

 

 

SWALI:

 

 

asalam alaikum,ndugu zangu waislamu.

Suali langu ni hili kuna vitu vingine vinavyomtokaga mwanamke kwenye sehemu ya siri,sijuwe kama ni wanawake wote,vile vitu ni vyeupe sio rangi ya maji,sijuwe nivifananishe na nini,ila vyeupe wakati mwengine vinarangi ya njano,naweza kidogo kuvifananisha na vitu ambavyovinavyomtokaga mtu kwenye meno kama anapitisha siku nyingi bila kupiga mswaki,naomba ndugu zangu  munielekeze kama ile pia ni najisi na hukmu yake mtu akiswali navyo.naomba munijibu ili niondoe wasisi.asante

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukran kwa swali lako hilo zuri. Hakika ni kuwa vipo vitu vyeupe aina mbili ambavyo vinamtoka mtu.

 

Kwanza: Wadii

 

 

Yanawatoka baadhi ya watu baada ya mkojo. Hii inafahamika kuwa ni najisi. ‘Aaishah (Radhiya Llahu ‘Anha) amesema: “Wadii inatoka baada ya kukojoa. Mtu anayetokwa anafaa aoshe sehemu zake za siri, kisha achukue wudhuu. Si lazima kuoga” (Ibn al-Mundhir).

 

 

Pili: Madhii

 

 

Ni maji meupe yanayonata yanayotoka katika sehemu za siri kwa sababu ya kuwaza tendo la ndoa au kutokana na matamanio yaliyozidi ya kimwili kwa kutazama, kushika, kushikwa n.k. Kawaida mtu hafahamu kwa uhakika kinachotoka. Inawatoka wanaume na wanawake, japokuwa kwa wanawake inakuwa ni nyingi zaidi. Wanazuoni wamekubaliana kuwa ni najisi. Ikiingia mwilini, ni wajibu kuiosha na inapoingia nguoni, inatosha kunyunyizia sehemu hiyo kwa maji. ‘Aliy (Radhiya Allaahu  ‘Anhu) anasema: “Nilikuwa ninatokwa na madhii mengi, hivyo nikamuuliza mtu amuulize Mjumbe wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo kwani niliona haya kwa sababu ya nafasi yangu kwa binti yake. Alisema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Fanya wudhuu na uoshe dhakari yako” (al-Bukhaariy).

 

 

Kwa mukhtasari ni kuwa ukitokwa na madhii inafaa uoshe sehemu yako ya siri, utawadhe na kama imeingia nguoni inatosha kunyunyiza maji katika hiyo sehemu.

 

 

Na ikiwa vinavyotoka sio katika hivyo viwili basi ni bora akaonane na daktari mahsusi wa wanawake ili ahakikishe zaidi isijekuwa ni maradhi fulani, Allaah Amuepushe nayo.

 

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share