Kuwapa Watoto Majina Ya Allaah Au Majina Yanayomshirikisha Allaah Kama 'Abdur-Rasuwl, 'Abdul-Husayn

 

Kuwapa Watoto Majina Ya Allaah

Au Majina Yanayomshirikisha Allaah Kama 'Abdur-Rasuwl, 'Abdul-Husayn

Nini Hukmu Yake?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

  

SWALI 1

 

Nini hukumu ya kuwapa watoto majina ya Allah sw kama vile SHAQUR, SATARU na mengineyo???

 

Assalam alaykum

 

SWALI La 2:

 

Nini sheria inasema kuhusu mtu kupewa jina kama la Abdul-Rasul? Je, ikiwa ameshafikia umri mkubwa anapaswa  kubadilisha au si lazima?      

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu  (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na kuandika kikamilifu (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ‘Ibaadah, na ‘ibaadah inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala hawakufupisha katika kuandika kwenye barua zao walipomtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike. Kwa faida zaidi bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

 

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Katika Maandishi

 

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

Ufafanuzi Wa Kiburi Na Mas-ala Ya Bid’ah Katika Jibu La “Hukmu Ya Kufupisha Thanaa”

 

 

Ama Kuhusu swali lako ni kwamba mzazi au mlezi anafaa kujiepusha kumpatia mtoto wake jina ambalo ni maalum kwa Allaah. Haifai kumuita mtoto kwa jina kama la Al-Ahad (Mmoja pekee), Asw-Swamad (Mwenye kukusudiwa kwa haja zote), Al-Khaaliq (Muumbaji), Ar-Razzaaq (Mwenye kuruzuku) na kadhalika.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimbadilisha mtu aliyesilimu aliyekuwa akiitwa Abul-Hakam (baba wa Hukumu) akimwambia kuwa Allaah Pekee Ndiye Mwenye sifa hiyo ya Al-Hakam, na Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza kama ana watoto na majina yao, yule mtu akataja wanawe watatu, Shurayh, Muslim na 'Abdullaah. Basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Kuanzia leo wewe ni Abuu Shurayh.” [Abu Daawuwd].

 

Kadhalika Abuu Hurayrah alikuwa akiitwa 'Abdush-Shams (Mja wa jua) lakini alipoingia Uislamu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimbadilisha jina lakena kumuita 'Abdur-Rahmaan.

 

Hata hivyo, yapo majina mengine ambayo ni sifa ya Allaah ('Azza wa Jalla)    na pia ya wana Aadam  kama vile Maalik (mfalme). Kwa hiyo, kumuita mtoto jina hilo hakuna tatizo. Mbali na hayo ni vyema kuwaita watoto majina ya Allaah kwa kufuatanisha na 'Abd (mja). Kwa mfano majina hayo yatakuwa kama 'Abdu-Allaah, 'Abdur-Rahmaan, 'Abdul-Fattaah, 'Abdur-Razzaaq, 'Abdus-Salaam na kadhalika.

 

 

Kuhusu swali la pili, ni kwamba  haifai kabisa mtu kuitwa 'Abdur-Rasuwl (Mja wa Rasuli), au 'Abdun-Nabbiy (Mja wa Nabbiy, au 'Abdul-Husayn (Mja wa Husayn). Majina haya utayakuta sana kwa Mashia na watu kutoka Asia. 

 

Hakika majina kama hayo hayafai na ni makosa makubwa, kwani uja na utumwa ni wa Allaah Pekee na si wa kiumbe yeyote.

 

Hao wote kama Rasuli  au Al-Hussayn ni waja wa Allaah na watumwa wake na ni wana Aadam na hawawezi katu kuwa waumba au waabudiwa. Hata ikiwa mtu hajakusudia kuwafanya ni waabudiwa au waumba, vilevile ni makosa na haifai.

 

 

Majina yapo mengi mazuri na yenye maana nzuri nzuri. Allaah Ana majina mengi ambayo mtu anaweza kuyatumia kwa uja wake na hakuna haja ya kuwatuza viumbe hadi kujipa uja kwao.

 

 

Hayo ni matatizo pia yanayosababishwa na ghuluww za watu wanaotukuza maimamu wao hadi kuwapeleka katika daraja ya uungu. Ni hatari kubwa sana kwa mja kuingia katika balaa hilo la kumpeleke  katika ushirikina kwa kujua au kutokujua.

 

 

Na ikiwa mtu alipewa jina katika majina hayo yasiyofaa na wazazi wake, basi anapaswa kwenda kubadilisha jina hilo hata kama ameshafikia umri mkubwa ili ajiepushe na shirki.

 

Uislamu unamruhusu mtu kubadili jina lolote baya hata ikiwa kapewa na wazazi wake. Tuchukue mfano wa matukio tuliyotaja juu ya Maswahaba kubadilishwa majina yao na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share