Naweza Kufungishwa Ndoa Bila Idhini Ya Mama Kwa Sababu Baba Karitadi

SWALI:

 

Asalaam aleikum, shukurani zote anastahiki kupewa Allah (swt). Ningependa kutumia fursa hii, kuuliza swali ambaye sina raha mpaka nipate jibu lake.

Je unaweza kufunga Nikkah bila idhini ya mama, ikiwa huna baba? Pengine baba kajitoa kwenye dini ya kislamu au kafa au yuko mbali. Je inaruhusiwa kama mama hataki na mtoto wa kike wanatakana na anaye ulowa naye?   


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.T) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuolewa bila idhini ya mama.

Kila jambo katika sheria ya Kiislamu ina masharti yake ili kusihi jambo hilo. Ama katika ndoa, masharti ya kusihi ni kama yafuatayo:

 

1.     Idhini ya walii (mzazi wa mwanamke au anayeshika mahali pake).

2.     Idhini ya mwanamke mwenye kuolewa.

3.     Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

4.     Mahari.

 

Hivyo, kusihi ndoa si lazima idhini ya mama lakini ni lazima kuwe na idhini ya baba. Ikiwa baba amekufa au ameritadi itabidi kutoke idhini ya babu upande wa baba, kisha kaka zako, kisha watoto wa kaka zako (waliobaleghe), kisha ma’ami zako na kisha watoto wao kwa mpangilio huo.

 

Ikiwa hao waliotajwa wako mbali mnaweza kuwasiliana akatuma barua ya kutoa idhini au akapiga simu kutoa idhini hiyo.

 

 

Hata hivyo, ni vyema kama mtazungumza na mama ili aweze kukubali ndio muwe na mahusiano mema na mama mzazi wako. Ikiwa mlifanya ndoa akiwa yeye amekataa inatakiwa mfanye juhudi kurudisha mahusiano mema na mama yako japokuwa ndoa yenu ni sahihi kabisa.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Ndoa Ya Siri Inafaa Ikiwa Wazazi Hawataki?

 

 

Ndoa Bila Ya Radhi Ya Wazazi

 

 

Kukosa Radhi Za Mzazi Kwa Kuolewa Na Asiyetakiwa Na Mzazi Bila Sababu Za Kisheria

 

 

Anaweza Kufunga Ndoa Bila Ya Kumshauri Mama Yake Asiye Muislamu?

 

 

Tunawaombea kila la kheri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share