Sigara Na Tumbaku: Mtazamo wa Uislamu - 2
Sigara Na Tumbaku: Mtizamo Wa Uislamu - 2
Imetafsiriwa na Naaswir Haamid
Fatwa Za Wanachuoni Mbalimbali
Fatwa Ya
Shaykh Muhammad Bin Ibraahiym
Shukrani zote ni za Allaah, tunamsifu na kumshukuru, kuomba msaada Wake na msamaha Wake. Yeyote ambaye Allaah Amemuongoza, hakuna yoyote wa kumpotosha, na yeyote ambaye Allaah Amempotosha, hakuna yeyote wa kumuongoza. Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Rasuli Wake wa mwisho, Nabiy wetu Muhammad, na watu wake wa nyumbani na Swahaba zake.
Ama ba'ad:
Hakika tunaishi ndani ya zama za utatanishi, ambapo ukweli unachanganywa na uongo, na hakuna yeyote anayeweza kutenganisha baina ya hivyo viwili isipokuwa kwa wale ambao Allaah Amewapa upambanuzi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ
Enyi walioamini! Mkimcha Allaah Atakupeni upambanuzi na Atakufutieni maovu yenu, na Atakughufurieni. [Al-Anfaal: 29]
Na kwa namna ambayo wengi wamechanganyikiwa ni kwenye sigara/tumbaku ambayo imeenea sana ndani ya zama zetu. Mtihani wake umewaathiri watu wengi, hata wale ambao tunaweza kuamini kuwa ni miongoni mwa waadilifu, wanashiriki sana hadi tunawaona wakiitumia sehemu zilizo wazi, wasioona madhara yake kwa Diyn yao na afya.
Pia, uharibifu mkubwa umefanywa na wale wanaojiita wanachuoni, wakiwachanganya watu na kutowapatia uwazi wa hukumu kuhusiana na sigara/tumbaku, wakitoa kisingizio kwamba hakuna ushahidi wa wazi unaoweza kupatikana kuhusu uharamu wake. Kama tutajikubalisha na hoja hii, mmoja anaweza kuona kwamba hatutaweza kutoa hukumu ndani ya masuala mengine ya Diyn, kwa hakika Allaah, nje ya Busara Zake zisizo na mipaka, Ametoa hukumu za jumla na kuturuhusu kuhukumu masuala mahsusi, hivyo kuifanya Diyn Yake kuwa ni chanzo kikuu cha sheria za wakati wote, ndani ya dunia hii na inayofuata, hadi mwisho wa wakati.
Yeyote mwenye ufahamu mdogo wa Uislamu na vyanzo vyake hatakuwa na wasiwasi kuhusu uharamu wake, lakini akili za watu wengine zimechafuliwa kwa sababu ya kujikita na dhana za uongo, kufuata kwa upofu kwa kiwango kikubwa hadi akili zao zimeacha kufanya kazi, zimekuwa hazina uwezo wa kutambua chochote isipokuwa ushauri ambao wanaufuata.
Kwa hivyo ni juu ya wale ambao Allaah Amewapa tawfiyq[1] ya kuelewa lengo la Diyn ni kuvunja minyororo ya ujinga na ufuasi wa upofu, na kuwafafanulia watu ukweli wa sigara/ tumbaku ambayo inachukuliwa kama ni jambo jepesi na wengi hivi leo.
Kwa sababu hii, tunaona kuna haja ya kwamba fataawaa[2] za wanachuoni ambazo Allaah Amezichagua kutokuwa ni za kijinga kueleweka, kuwafafanulia wote uharamu wa jambo hili ovu na baya, na kuwa miongoni mwa wale wenye kutoa ushindi kwa Diyn Yake, bila ya kuogopa lawama za wale wenye kulaumu. Tunamuomba Allaah Awalipe malipo mema wale waliosaidia kuchapisha kazi hii, na kuwapa malipo kwa lolote jema linalotokana na kazi hiyo, Amiyn.
Shukrani zote ni za Allaah Pekee, na Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Muhammad, wa mwisho katika Rusuli.
Niliulizwa kuhusu hukumu ya sigara/ tumbaku, ambayo watu wengi wajinga na wapuuzi wanaipendelea, juu ya ukweli kwamba kila mtu anatambua kuwa tumeshaeleza uharamu wake. Sisi, wanachuoni na walimu wetu, walimu wao, na wanachuoni wote wenye kutafuta ukweli kutoka viongozi wa Da'wah[3] wa Najd[4] na ulimwengu wote wa Waislamu waliobaki, kutoka enzi za machomozo mnamo mwaka 1010 AH hadi hii leo, uharamu wake umeelezwa, wote wakiegemeza ushahidi wao kutoka misingi ya Diyn na maarifa.
Kwa sababu hii, hapo mwanzo nimehisi sio sahihi kujibu suala hili, lakini kwa kuwa ni haki ya msingi ya muulizaji, na kwa vile hili ni khabiyth[5], kama mtu asivyotegemea, imeenea sana, nimeamua kuendelea kulijibu.
Kwa hivyo ninasema:
Hakuna shaka yoyote kwamba sigara ni kitu khabiyth na kichafu, na kwamba baadhi ya nyakati ina sifa ya kuwa na kilevi, na baadhi ya wakati inafanya kazi kama ni kiliwazo cha uongo. Uharamu wake umeegemezwa kwenye maandiko ya Qur-aan na Sunnah[6], hoja zenye maana, na pia kutoka matamshi ya matabibu na watu wengine ambao wanauelewa mnasaba wake.
Ya Mwanzo: Chanzo Sahihi.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema ndani ya Qur-aan:
الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ
Wale wanomfuata Rasuli; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza munkari, na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu. [Al-A'raaf, 7:157]
Imesimuliwa katika Hadiyth[7] ndani ya [Swahiyh al-Bukhaariy], kutoka kwa Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), amesema kwamba: amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Kila chenye kulevya inatambuliwa kuwa ni khamr (ulevi) na kila khamr ni haraam (hairuhusiwi)."
… na ndani ya maelezo ya [Muslim]:
"… na kila chenye kulevya ni haraam."
Pia imepokelewa na At-Tirmidhiy (aliyeieleza kwamba ni Hadiyth [Hasan[8]) na Abu Daawuud]:
"Kila chenye kulevya ni haraam, na kila chenye kiwango kikubwa cha kilevi, hata kwa kiwango kidogo ni haraam."
Aayah zote hizi tukufu na Ahaadiyth za kweli zina msimamo mmoja kuhusu uharamu wake, kwa sababu baadhi ya wakati ni yenye kulevya na kwa wakati mwengine ni yenye kutoa liwazo ya uongo, wala hakuna anayekataa kuhusu ukweli huu isipokuwa wale wanaokataa ukweli wa hisia zao. Hakuna shaka yoyote, maandiko haya pia yanathibitisha uharamu wa aina nyenginezo za vilevi na vitulizo.
Imepokewa na [Imaam Ahmad na Abu Daawuud] kutoka kwa Umm Salamah, (Radhwiya Allaahu ‘Anha), kwamba amesema:
"Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha kila chenye kulevya na kila kitulizo."
Al-Haafidh, az-Zain al-'Iraaqi amesema:
"Isnaad[9] yake ni Swahiyh[10]," na as-Suyutiy pia amesema kuwa ni Swahiyh ndani ya kitabu chake cha Al-Jaami'-us Swahiyh."
Uvutaji sigara pia unahusisha upotezaji wa pesa, kumfanya mvutaji kujitolea kuacha mambo mengi ya msingi kwa lengo la kuihodhi sigara, na hakuna yeyote anayeweza kulipinga hili.
Ndani ya Hadiyth inayopatikana kutoka Swahiyhayn[11],Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Hakika Allaah Amekuharamishieni: kuwaasi wazee, kuwazika hai binti, na kudai haki zenu hali ya kuwa hamuwapi wengine, na Amewahamakia[12]: mazungumzo ya upuuzi, kuendelea kuuliza[13], na ubadhirifu wa pesa."
Kitakachofuata kutokana na tamko hilo kutoka kwa madhaahib[14] makuu manne kitafafanua nini kilikusudiwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kutoka kwa fuqahaa[15] wa Hanafiyyah[16],Shaykh Muhammad al-'Ayni ameeleza ndani ya maandiko yake kwamba kuna sababu nne zinazopelekea kuharamishwa:
1) Matamko ya matabibu na watu wengine wenye elimu ya suala hili, wamethibitisha kwamba uvutaji sigara ni kudhoofika kwa afya ya mtu, na vitu vyote vyenye madhara kwa mtu yanaharamishwa kwa mujibu wa makubaliano ya wanachuoni walio wengi.
2) Matabibu wanaamini kwamba ni kilevi, na kila kilevi kinaharamishwa ndani ya Diyn. Hili linathibitishwa na Hadiyth ya Imaam Ahmad iliyosimuliwa na Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘Anha), amesema:
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha kila chenye kulevya na kila kitulizo."
Inatambulika kuwa ni yenye kulevya na matabibu wengi, na matamshi yao yanachukuliwa kuwa ni ushahidi na fuqahaa wengi wa vizazi vya mwanzo na vinavyofuata.
3) Harufu yake mbovu inayowachukiza wengine wasiovuta sigara, zaidi kwenye mikusanyiko ya Swalaah, hakika, inawachukiza Malaika pia. Imepokewa na Swahiyhayn kama ilivyosimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), kwamba amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"Yeyote anayekula kitunguu thomu au kitunguu maji, akae mbali na sisi na Masaajid[17] zetu, na akae nyumbani mwake."
Ni ukweli usiopingika kwamba harufu mbovu inayotokana na sigara ni mbaya zaidi kuliko harufu ya kitunguu thomu au kitunguu maji. Katika Hadiyth nyengine ndani ya Swahiyhayn, iliyosimuliwa pia na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Malaika hakika wanaumia kwa mambo ambayo yanawaumiza wanaadamu."
Katika Hadiyth nyengine, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Yeyote anayemkera Muislamu amenikera mimi, na yeyote anayenikera mimi amemkera Allaah." [Imepokewa na at-Twabaraaniy ndani ya al-Awsat kama ilivyosimuliwa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) yenye isnaad hasan.]
4) Ni upotezaji wa pesa na israfu, kwani haina manufaa yoyote yanayoruhusiwa, wala sio dharura inayoruhusiwa. Isipokuwa, kwa mujibu wa watu wenye elimu ndani ya nyanja hii, kuna madhara halisi ndani ya sigara.
Miongoni mwao ni Abul-Hasan al-Misriy al-Hanafi aliyesema yafuatayo:
Ushahidi kutoka vyanzo sahihi na maelezo kutoka kwa watu wenye maarifa wameruhusu kuzuiwa uvutaji wa sigara.
Mara ya mwanzo ilitokea mnamo mwaka 1000 AH ndani ya ardhi za Mayahudi, Wakristo na Zoroastriani (Majuuz). Ililetwa katika ardhi ya Kiislamu ya Magharibi (al-Maghrib) na Myahudi, akidai kuwa ni mtu wa dawa, aliyewaalika watu kuitumia. Mtu wa mwanzo aliyeiingiza Ar-Ruum[18] alikuwa ni Mkiristo mwenye jina la Ataclean.
Mtu wa mwanzo aliyeiotesha ndani ya ardhi za Sudani alikuwa ni Zooroastrian (Majuuz). Baadaye ilifikishwa Misri[19], Hijaazi[20], na ardhi nyenginezo.
Hakika Allaah Ameharamisha kila kilevi. Iwapo mtu atajadili kwamba sio kilevi, basi bado itabaki kuwa ni matendo yanayochukiza, yanayoharibu mwili wa mvutaji sigara, ndani na nje. Kilevi ni aina yoyote ya kuiharibu akili, hata ikiwa haishirikishwi iwapo mtu anaifurahia, na hakuna shaka yoyote kwamba hili linatokea pale mtu anapovuta sigara kwa mara ya kwanza. Lakini iwapo hatakubali ukweli wa kwamba ni kilevi, itabaki kuwa ni yenye kuondosha maumivu na kitulizo (kwa njia ya udanganyifu).
Imepokewa na [Imaam Ahmad na Abu Daawuud] kama ilivyosimuliwa na Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa) kwamba amesema:
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha kila chenye kulevya na kila kitulizo."
Wanachuoni wameeleza kwamba kitulizo ni kitu chochote ambacho mwisho wake ni chenye kutuliza (kwa kulevya) na kusababisha usingizi. Hadiyth hii itoshe kuwa ni ushahidi wa uharamu wake, lakini kwa kuongezea na hili, uvutaji sigara unaharibu mwili wa mvutaji sigara na roho yake: inaharibu moyo, mwili kukosa nguvu, na ngozi kupiga rangi ya umanjano.
Matabibu wanakubaliana kwamba ni yenye kuharibu ubongo. Inasababisha madhara kwa mwili wa mtu, tabia, heshima, na kiwango chake cha pesa. Hii ni kwa sababu inafanana na tendo la waasi, kwani wengi wao wanaovuta sigara ni wavunja sheria na wenye heshima za chini. Pia mvutaji sigara anakuwa na harufu mbaya isiyozuilika.
Miongoni mwa fuqahaa wa Hanaabilah[21], Shaykh 'Abdullaah bin Muhammad bin 'Abdil-Wahhaab, baada ya kutoa ushahidi wa maandiko kuhusu uharamu wa vitu vyenye kulevya na matamko ya wanachuoni kuhusu maana yake, amesema yafuatayo katika majibu yake ya tumbaku:
"Na kutokana na kile tulichokitaja kutoka matamko ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na matamko ya wanachuoni, sasa iwe wazi kwenu kwamba tumbaku ambayo imeenea ndani ya zama hizi ni haramu moja kwa moja. Na (hukumu) hiyo imesimamishwa na vyanzo vingi visivyo na idadi na mashahidi kwamba hakika inalevya kwa baadhi ya wakati, haswa pale inapotumiwa kwa kiwango cha juu. Vivyo hivyo, iwapo mvutaji sigara ataacha kuvuta kwa siku moja au mbili na kuirudia tena, itamlevya na kumuathiri akili yake hadi kufikia kwamba mvutaji kuipita gesi mbele za watu bila ya mwenyewe kuitambua! Tunaomba msaada wa Allaah kutokana na unyanyasaji wa aina hii.
Kwa hivyo haina faida yoyote kwa yule mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho kwamba atatafuta maneno ya mtu mwengine pale ambapo matamko ya Allaah na Nabiy Wake yamekuwa wazi kwake, yaani ndani ya masuala haya, kama alivyoshuhudia kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Rasuli wa Allaah ni jambo la kumtii lile aliloamrisha, kujizuia na yale aliyoyakataza na aliyoyatahadharisha, na kumuamini katika kila jambo alilotuamrisha."
Shaykh 'Abdullah Ababtayn amesema yafuatayo katika majibu yake kuhusu tumbaku:
Tunachoamini kwamba imeharamishwa, na sababu ya hili ni kwa mapindo mawili:
Sababu ya kwanza ni kwamba iwapo mvutaji sigara ataacha kuvuta sigara kwa kipindi na baadaye kuirudia, au kwamba akivuta kwa kiwango kikubwa, inasababisha kulewa. Iwapo haitosababisha kulewa, basi itasababisha kitulizo (kinachotokana na ulevi) na kusinzia. Katika Hadiyth ya Marfu’u[22] iliyopokelewa na Imaam Ahmad:
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha kila chenye kulevya na chenye kitulizo."
Nyengine ni kwamba inachukiza kwa wale wasiovuta sigara, na wanachuoni wana msingi wao wa ushahidi kutoka tamko la Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ
Na anawaharamishia maovu.. [Al-A'raaf: 157]
Lakini kwa wale waliozea hawaioni kuwa ni mbaya, kama vile mende asivyoelewa wingi wa uchafu anaoula.
Na kutoka kwa fuqahaa wa Shaafi'yyah[23],mwanachuoni anayetambulika kama ni Shaykh Najm al-Ghazzi ash-Shaafi'iy ameeleza yafuatayo:
Tumbaku ilijitokeza mara ya kwanza nchini Dimishq[24] ndani ya mwaka 1015. Wavutaji sigara walidai kwamba hailevyi. Hata kama tutalemaa na dhana hii, itabaki kuwa ni kitulizo. Ni vile vile kama ilivyoharamishwa kutokana na Hadiyth iliyopokelewa na Ahmad kama ilivyosimuliwa na Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘Anha):
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha kila chenye kulevya na kila kitulizo."
Ameendelea kusema:
Kuitumia mara moja au mbili haikadiriwi kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa (al-kabaair), isipokuwa iwapo mtu ataendelea bila ya kuiacha kuitumia, na kanuni hiyo hiyo inatumika kwa madhambi mengine madogo (as-saghaair).
Wanachuoni wameeleza kwamba madhambi madogo yana kanuni sawa kama ile ya madhambi makubwa iwapo yataendelea kuwa na moja kati ya sifa zifuatazo:
1) Kwamba mtu anaendelea nayo bila ya kuiacha.
2) Kwamba makatazo yake hayapewi kipaumbele, kwa kupunguza madhara yake na kutoijali.
3) Kwamba mtu anaweza kuwa na furaha akiwa faragha.
4) Kwamba mtu anajifakharisha nayo mbele ya watu.
5) Kwa kumfuata kutokana nayo mwanachuoni au mtu mwengine yeyote anayechukuliwa kama ni mfano kwa wengine.
Shaykh Khaalid bin Ahmad kutoka kwa fuqahaa wa Maalikiyyah[25] amejibu kwa kueleza yafuatayo:
Imaamah[26] anayevuta tumbaku/ sigara haruhusiki, na hivyo hivyo kwa kilevi chengine, biashara yake pia hairuhusiki.
Wafuatao ni baadhi ya wanachuoni wengine walioharamisha tumbaku na kueleza uharamu wake:
1) Kutoka kwa wanachuoni wa Shaykh Ahmad as-Sanhuuri al-Bahuuti al-Hanbali.
2) Kutoka kwa wanachuoni wa al-Maghrib: Abdul-Ghaith al-Qashshaash al-Maaliki.
3) Kutoka kwa wanachuoni wa Dimishq: an Najm al-Ghazzi al-'Aamiri ash-Shaafi'i.
4) Kutoka kwa wanachuoni wa Yemen: Ibraahiym bin Jumu'aan na wanafunzi wake, Abu Bakr al-Ahdal.
5) Kutoka kwa wanachuoni wa Haramayn[27]: Al-Muhaqiq Abdul-Maalik al-'Isaami na mwanafunzi wake Muhammad bin 'Al-laan, washereheshaji kutoka Riyaadh us-Swaalihiyn, na As-Sayyid 'Umar al-Basri.
6) Kutoka katika ardhi za Ruum: Shaykh Muhammad al-Khawaajah, 'Iysaa ash-Shahaawi al-Hanafi, Makki bin Farukh, As-Sayyid Sa'd al-Balkh al-Madani, na Muhammad al-Barazanji al-Madani ash-Shaafi.
Pia ameeleza:
Wanachuoni wote wa Ummah na Imaamu bora wameeleza kuhusu uharamu wake, na kuiharamisha kunufaika nayo katika njia yoyote.
Ya Pili: Wenye Akili (Hawaikubali)
Kutoka kwenye mawazo ya moja kwa moja na ithibati zisizo na idadi, tunakuja kutambua kwamba ni yenye madhara kwa afya ya mtu, mwili, na akili. Kifo, kutokwa na akili, kuzorota afya, kama vile kukohoa yanayopelekea kwenye kifua kikuu, maradhi ya moyo, na kupungua nguvu ya kusafirisha damu; yote haya yameshuhudiwa kuwa yanatokana na kuvuta sigara.
Pale mtu anapoona madhara haya na mengine yanayotokana na sigara, anakubaliana kwamba uvutaji sigara hauruhusiki kabisa kabisa. Kama ilivyo hoja za mtu mwenye akili timamu ni kupata lile lenye kumpatia manufaa na kuwa na afya njema, pia inahusisha mtu kuwa mbali na yale yenye kumsababishia madhara, kama ilivyoamriwa na uharamu wake.
Na wala hakutakuwa na mafungamano ya wale wenye shaka na utashi ulioota mzizi ndani ya viungo vya bongo zao, hadi pale watakapoingizwa akilini mwao kwa dhana na fikra za uongo, na wataachwa wakiwa ni wafungwa wa utashi wao.
Ya Tatu: Ithibati Ya Matabibu
Matabibu wa hapo kale wanakubaliana wote kuhusu madhara yanayopatikana ndani ya sigara. Mtu anaweza kuona kwamba wametahadharisha dhidi ya sifa zake tatu:
1) Ladha yake mbovu,
2) Majivu yake,
3) Moshi wake na harufu yake, vitabu vyao (Matabibu) vikiwa vimeenea kwa sifa hii (mbaya).
Matabibu wa leo pia wapo makini na ubaya wa jani hili, na tunafupisha kwamba wametaja madhara yake na yanayopelekea kusababisha kwake (madhara).
Muhtasari wa yale waliyoyasema ni kama ifuatavyo:
Ni jani jembamba, lenye ladha mbovu. Baada ya uchunguzi na umakini, tumekuja kutambua kwamba tumbaku ni ya aina mbili, yote yakitokana na aina ya mimea yenye sumu, kama vile henbane. Ina potassium na ammonium salts, na aina nyengine inayoitwa nicotine.
Inatumiwa kwa matumizi tofauti:
1) Ya mwanzo ikiwa ni kwa kuchakuwa, na hii ndio yenye madhara na yenye ladha mbaya. Athari zake kwa afya ni zenye nguvu; sumu yake inayeyuka upesi kwenye mfumo wa mkojo na una madhara mabaya kwa mfumo wa akili.
2) Ya pili inaingizwa mwilini pamoja na (kutumia) aina nyengine za uchangamfu (mirungi). Kwa sababu hizi ni aina tofauti za sumu, hakika hizo pia zina madhara na hakuna shaka kwa hilo.
3) Ya tatu ni kwa kuichoma na kuivuta, hii ni aina maarufu ambayo ni sigara, ikiwa pia inavutwa kwa kutumia kiko na kiko za maji (shisha). Katika njia zote hizi, moshi unafika mdomoni katika hali ya juu ya joto.
Matabibu wamethibitisha kwamba inasababisha madhara mengi tofauti. Chembe chembe zake mwanzo zinatulia ndani ya mwili, na baadaye zinaleta madhara kidogo kidogo na kudhihirika kila muda unavyosonga mbele. Wameeleza kwamba moshi unaotoka kwenye majani ya tumbaku una chembe chembe za vilevi tofauti, kama vile nicotine. Pale inapoingia kwenye mdomo na mapafu, ina athari za jumla na kwa sehemu maalumu pia, pale inapoingia mdomoni, chembe chembe za sumu zinachuna mucous membrane, na kusababisha ongezeko la kiwango cha mate kukusanyika. Chembe chembe za mate zinabadilishwa na hivyo mfumo wake kuyeyusha chakula unapunguzwa. Pia, unaathiri sehemu za tumbo, na kusababisha matatizo ya kuyayusha chakula. Moshi unapofikia sehemu za mapafu kwa kupitia kwenye koromeo, chembe chembe za sumu zinazidi sehemu hizo, na bila ya shaka inapelekea kwenye moshi ulio mwingi. Koromeo hiyo inachunwa chunwa na kusababisha kukohoa, kwa kujaribu kutoa nje kiwango kikubwa cha moshi huo, kwa maarufu inajulikana kama belghamu (kamasi). Uvutaji sigara pia unasababisha kuziba kwa mishipa ya pafu na maradhi mengine ya kifua. Mabaki ya moshi (tar) yanatupwa ndani ya koromoeo na moyo, na hivyo kuongeza presha kwenye sehemu zake za kufunguka na kupunguza uingiaji wa oksijini, na hivyo kupunguza kasi ya kupata pumzi.
Sigara pia inasababisha kulala ovyo, kizunguzungu, kuumwa kwa kichwa na kutapika kwa wale wasioizoea na wale wanaojaribu kwa mara ya kwanza. Pia inasababisha misuli kuwa debwedebwe (kulegea) na kusinzia, ambayo yanaenda sambamba na kitulizo, (hiyo ni) sifa ya kurithiwa ya tumbaku kwa (matabibu) wengi. Yeyote anayeizoea matumizi yake, anaathirika na mapungufu mengi, uharibifu wa ladha, mfumo wa kuyeyusha chakula, ukosefu wa hamu ya kula; yote ambayo yapo wazi na matokeo yanayojulikana.
Hakuna shaka yoyote kwamba uvutaji mwingi wa sigara unasababisha kifo, iwapo ni kidogo kidogo au kwa kipindi kirefu. Hili liliwahi kutokea pale ndugu wawili waliposhindana nani atakayeweza kuvuta sigara nyingi zaidi. Mmoja wao alikufa kabla ya sigara ya kumi na saba, na huyo mwengine alikufa kabla ya kuikamilisha sigara ya kumi na nane!
Uvutaji sigara pia unasababisha uharibifu wa chembe chembe nyekundu za damu, kuiparaganya mifumo ya moyo, ukosefu wa hamu, kuharibu daraja za mwenendo wa mfumo wa ubongo, na hili linaonekana wazi kwa kusinzia na kuhisi kizunguzungu, athari zinazoonekana kwa yule mvutaji asiyezoea uvutaji sigara.
Mara moja Profesa Mustafa Hamaami aliwahi kusimulia ndani ya kitabu chake kisa kilichowahi kumtokea:
Siku moja nilikuwa natembea kwa miguu pamoja na mwanafunzi, tukapita sehemu inayouzwa sigara. Mwanafunzi huyo akanunua mbili. Akawasha moto moja ya sigara hiyo, na kuapa kwamba ni lazima mimi nijaribu hiyo ya pili. Hivyo, nikaivuta sigara; nikazidiwa na moshi wake na kujaribu kuutoa mdomoni, bila ya kuuingiza wote ndani. Akawa makini na jambo hilo na kusema: "Peleka ndani ulichovuta, kwani hicho ndicho kiapo changu kilivyosema," Sikukataa na nikafanya lile alilosema. Nikapeleka ndani pumzi moja, na kwa Allaah, sikuongeza zaidi ya hiyo na ghafla kila kitu kikaanza kuzunguka kama vile kinu kinachozunguka! Mara moja nikakaa chini, na nikafikiria kwamba hii itakuwa ni mara ya mwisho. Nikaanza kuwafikiria vibaya marafiki zangu. Kwa taabu sana, nikafika nyumbani kwangu. Nilifika kwa gari, na alikuwa pamoja nami akinisaidia. Baada ya tukio hilo, nilikaa nyumbani hadi takribani mwisho wa siku ya pili, hadi sikuhisi ni namna nilivyokuwa hapo jana. Niliwahadithia tukio hili watu wengi, nikiwafichulia yale yaliyofichikana kuhusiana na sigara. Waliniarifu kwamba sigara ina athari hii kwa yeyote asiyeizoea. Nikasema: "Iwapo mvuto mmoja tu ulinisababishia hivi, basi inakuwaje kwa wale walioizoea, wakati siku haipiti bila ya mtu kuivuta, haswa kwa wale wanaoivuta mara kwa mara!"
Uvutaji sigara pia unasababisha mparaganyiko wa ubongo (saikolojia) unaojulikana kama ni withdrawal, ambapo mtu asiyeweza kuiacha, iwapo atajaribu kuiacha, hatoweza kufanya kazi sawasawa na hawezi hata kuikamilisha kazi za siku zake hadi avute, na anapuvuta sigara, hali yake inajirudia kama kawaida.
Wanachuoni na matabibu wengi wameeleza kwamba mtu mwenye akili timamu, achilia mbali mwenye Diyn, inamwambia ashikamane na afya yake na kujiepusha na kujiingiza kwenye maradhi yatakayosababisha kifo kwa kuacha kuvuta sigara. Hili linakuja wazi zaidi kwa wale wenye miili dhaifu, watu wazima wasiokuwa na nguvu ya kupigana na maradhi, na wale wanaokuwa na matatizo ya belghamu.
Na kwa sababu hii, watu wengi wanajaribu kuiacha, wakikhofia madhara yake na harufu yake mbovu. Wanafikia kusema kwamba wataachana na wapenzi wao iwapo watairudia, wakijaribu kwa hilo kuachana nayo moja kwa moja, lakini pale utashi unapowazidi, hawawezi kuiacha. Wanairudia tena, hata kama itakuwa ni kumuacha mpenzi wake, kwani inamdhibiti kisawasawa yule aliyeizoea na kumuathiri akili yake kwa kumtuliza ndani ya vipindi vya hamaki na mashaka.
Na Allaah Anajua zaidi.
Na Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Mtumishi Wake na Rasuli Wake Muhammad, na juu ya watu wake wa nyumbani na Swahaba zake.
Muhammad bin Ibraahiym bin 'Abdil-Latwiyf Aali - Shaykh
4/6/1383 (AH). 20/09/1966 (M)
Itaendelea In shaa Allaah…
[1] Tawfiyq: Uwezo kutoka kwa Allaah kwenye kufanya jambo sahihi.
[2] Fataawaa: Wingi wa Fatwaa, lenye maana ya hukumu ya kishari’ah ndani ya Diyn.
[3] Da'wah: Wito kwa Uislamu. Hapa lina maana ya da'wah ya Muhammad bin Sulaymaan at-Tamiymiy.
[4] Sehemu kuu ambayo hivi leo inatambulika kama ni Saudi Arabia.
[5] Khabiyth: wingi ni khabaaith: Kilugha lina maana ya kitu chochote chenye kuonekana kuwa kina madhara mabaya. Kwa upande wa Diyn, kitu chochote chenye kuwa na madhara mabaya, ovu, na kisichoruhusiwa, yaani vitu, matendo, imani, watu na chakula. Khubth: Uovu.
[6] Sunnah: wingi Sunan: Matamshi, matendo au ridhaa ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
[7] Hadiyth: wingi Ahaadiyth: Simulizi ya matamshi, matendo, ridhaa au sifa za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
[8] Hasan: Hadiyth ya kweli, lakini ile ambayo isiyokuwa na sifa ya Sahihi.
[9] Isnaad: Mnyororo wa wasimulizi unaosimulia Hadiyth fulani.
[10] Swahiyh: Hadiyth yenye hadhi ya juu kwenye ukweli wake.
[11] Swahiyhayn: Kilugha, Swahiyh mbili. [Al-Bukhaariy na Muslim], vitabu viwili vyenye kuaminika vya Hadiyth, na ni vitabu viwili hivi tu miongoni mwa vitabu sita maarufu vya Hadiyth, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaaiy, Ibn Maajah na at-Tirmidhiy. Ambapo waandishi Muhammad bin Isma'iyl al-Bukhaariy na Muslim bin Hajjaaj an-Nisapuri waliazimia kuingiza Hadiyth bora za ukweli tu.
[12] Imaam an-Nawawi ameeleza ndani ya maelezo yake ya Swahiyh Muslim: "Wanachuoni wameeleza kwamba kinachokusudiwa hapa ni ridhaa, hamaki, na ghadhabu kutoka kwa Allaah ni amri Yake au makatazo, na malipo au adhabu." Pia Qur-aan, baada ya Allaah kueleza baadhi ya madhambi makubwa, yaani uzinifu, mauaji, na kuwaua watoto, Anawaeleza kama ni wenye kuchukizwa na Yeye:
Yote hayo, uovu wake umekuwa ni wa kukirihisha mbele ya Rabb wako. [Al-Israa: 38]
[13] Aina ya uulizaji usio kuwa na maana yoyote.
[14] Madhaahib: Wingi wa Madhhab, au dhehebu la fikra fulani.
[15] Fuqahaa: Wingi wa Faqiyh, au mwanachuoni wa Fiqh, au Maarifa ya Shari’ah za Kiislamu.
[16] Fikra zinazojinasibisha na Abu Haniyfah (Rahimahu Allaahu).
[17] Masaajid: Wingi wa Masjid. Sehemu maalumu ya kuswalia iliyojengwa kwa kumuabudia Allaah.
[18] Ar-Ruum: Sehemu ambayo sasa ipo Turkey na sehemu nyenginezo inayoizunguka.
[19] Misri: Ardhi ambayo sasa inajulikana kama Egypt.
[20] Hijaaz: Sehemu za magharibi ambazo sasa zinajulikana kama Saudi Arabia.
[21] Fikra inayojinasibisha na Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaahu).
[22] Marfuu': Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au Hadiyth ya Swahaba ambayo inapewa hukumu sawa, kwa sababu ya ukweli kwamba amemtaja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au kutowezekana kwake kusemwa kuwa ni ya kulingana.
[23] Fikra inayojinasibisha na Muhammad bin Idriys ash-Shaafiíy (Rahimahu Allaahu).
[24] Dimishq: Mji unaojulikana hivi leo kama ni Damascus.
[25] Fikra inayojinasibisha na Maalik bin Anas (Rahimahu Allaahu).
[26] Imaamah: Jukumu la uongozi ndani ya Swalaah.
[27] Al-Haramayn: Kilugha: sehemu mbili tukufu: Makkah na Madiynah.