Facebook Au Fitnabook?
Facebook Au Fitnah-Book?
Kwanza kabisa, ijulikane wazi kwamba kusudio la makala hii si kutoa fatwa wala hukumu. Lengo ni kuweka wazi manufaa na madhara ya Facebook ili mtu binafsi atoe hukumu yake mwenyewe.
Je, ni Facebook au Fitnabook? Hili ni suali ambalo watu wengi wameanza kujiuliza baada ya kujionea vitimbi na kashfa kadhaa katika huu mtandao ambao unazidi kujipatia umaarufu kila pembe ya dunia. Naam, kuna vitimbi kadhaa vinafanyika kwa jina la Facebook. Na ndio kuna vijana wengi ambao wametumbikia katika janga la fitna katika Facebook lakini nini suluhisho la hili? Kabla hatujatazama hebu kwanza tuangalie manufaa na madhara ya Facebook.
Manufaa
Kama ilivyo kawaida ya vitu vingi, Facebook ina faida yake. Lakini je, hizo faida ni nyingi kuliko madhara? Katika sehemu hii tutaja manufaa ambayo yanasemwa na watumiaji wa Facebook. Manufaa hayo ni kama yafuatayo:
1. Kufanya Da’wah (kuwalingania watu kwenye Uislam)
Madaa’iyah kadhaa pamoja na baadhi ya Mashaykh hutumia Facebook kwa kazi za da’wah. Huwekwa na kutumwa vitu mbalimbali vya kufikisha mafunzo mbalimbali ya Dini kama: mawaidha, makala za Kiislamu na njia mbalimbali za kunufaisha wasomaji.
2. Kutangaza shughuli na harakati za Kiislam
Mambo mbalimbali yanayowahusu Waislamu mara nyingi huwa yanatangaziwa kwa kutumia Facebook.
Madhara
Ijapokuwa kunaonekana kuna baadhi ya manufaa kadhaa juu ya utumiaji wa Facebook, kuna madhara mengi na fitnah nyingi hupatikana humo, kadhalika watu wengi wanaitumia kwa njia mbaya. Katika madhara ya Facebook ni haya:
1. Kukashifiwa Mtume na Uislam.
Kubwa zaidi na baya zaidi na la hatari zaidi, ni hili lililotokea siku za nyuma, la kukashiwa kwa Mtume kwenye Facebook, jambo ambalo limewasikitisha wengi wetu na tuna kila haki ya kuhuzunika juu ya hilo. Picha mbalimbali za kashfa na za kumlinganisha Nabiy wetu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mambo maovu na machafu, zimewekwa huko kwa kuchorwa vikatuni vinavyodaiwa kuwa ni yeye. Na yamejitokeza makundi tofauti yaliyoungana huko kwenye Facebook ili kuukashifu Uislamu na Waislamu na kumdhalilisha Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Haya yote ni matunda ya hiyo Facebook.
2. Kuweka mapicha na kujitangaza na kujionesha na zaidi ni Riyaa ima kwa kukusudia au kutojitambua. Haya yanafanywa hata na wanaoonekana wana elimu ya Dini kama Madu’aat na Masheikh.
3. Mchanganyiko wa wanaume na wanawake.
Ada kuu iliyoshamiri na kuenea kati ya watumiaji ya Facebook ni kutazama na kuongea na watu wasio Mahram zao.
4. Utakuta hata wanaojiita Madu'aat au kujinasibisha na ulinganiaji, wanapiga soga na wanawake wasio mahram zao, kuwepo mapicha ya wanawake tena yasiyo na stara na wakiwa ni marafiki wa hao Madu'aat!! Wa Allaahul Musta'aan.
5. Mijadala isiyo na tija. Kunazuka mijadala mingi ya kiitikadi, kimadhehebu na mfano wake, na makundi potofu na watu wa bid'ah na hawaa. Matokeo ni ubishi usio na tija na hakuna faida inayopatikana, ila kinachoshuhudiwa aghlabu ni matusi na kukufurishana.
6. Kupoteza muda kwa mambo ya upuuzi.
Watu wengi hasa vijana hupoteza masaa juu ya Facebook wakati wangeliutumia muda ule kwa kufanya kitu cha muhimu
7. Kutokuwepo kwa hayaa na heshima.
Uislamu umekuja kulinda heshima ya binaadam lakini cha ajabu vijana wengi wa Kiislamu hutokwa na hayaa na huvuruga heshima zao kupitia Facebook. Wasichana wangapi wameweka picha zao bila ya hijaab kwenye Facebook kwa kutaka kujionyesha? Wanawake wangapi wameharibu heshima zao na za familia zao kwa kutuma maasi yao kwenye Facebook?
Suluhisho
Baada ya kujionea na kutafakari juu ya madhara na manufaa yaliyomo kwenye Facebook, lilobakia ni kujiamulia mwenyewe. Ikiwa utaona kwamba Facebook madhara yake ni makubwa kuliko faida, basi ni juu yako kujihadhari juu ya kuitumia na bora zaidi kujiepusha nayo.
Ikiwa utaona kwamba manufaa yamezidi basi ni pia juu yako kujichunga na madhara yaliyomo huko. Inawezekana kitu ukakiona kina manufaa kadhaa lakini madhara yake ni mengi zaidi. Allaah Anasema kuhusu ulevi na kamari.
يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَآ أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا
Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. [Al-Baqarah: 219]
Isitoshe, pahala ambapo anatukanwa Allaah au Nabiy Wake, au Qur-aan au Sunnah au jambo lolote la Dini, basi sehemu hiyo inapaswa kuhamwa au kutengwa hadi itakapojirudi au kuomba radhi na kubadili mwelekeo wako. Na ikiwa Facebook imeomba radhi kwa matendo yake ya kumtusi na kumdhalilisha Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hapo tena Muislamu ana khiyari ya kutumia ukumbi huo kwa manufaa yaliyotajwa au kuuacha na kuutenga kwa madhara yaliyoelezwa. Na bila shaka madhara na uadui waliouonyesha kwa Uislamu na Waislamu, unamtosha Muislamu kuwa mbali na ukumbi kama huo au mwengine wowote unaofanana na huo.
Kwahiyo, tujihadhari, hasa katika mambo ambayo yana utata ili tuweze kulinda Dini yetu na heshima yetu.
Imeandaliwa na: Iliyaasah.