Madhambi Makubwa Na Madogo
Madhambi Makubwa Na Madogo
Madhambi Makubwa:
Madhambi makubwa ni yale ambayo yametajwa katika Qur-aan na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nayo ni yale ambayo mja anapoyafanya huwa na hukmu zifuatazo:
(i) Madhambi ambayo Allaah Anaalaani kitendo chake.
(ii) Madhambi ambayo yamewekewa adhabu kali kama mfano mwenye kuzini na hali ameoa au ameolewa kupigwa mawe hadi kufa au kupigwa bakora 100 kwa asiyeoa au asiyeolewa.
(iii) Madhambi ambayo Anaghadhibika nayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala).
(iv) Madhambi ambayo Allaah Anamnyima Rahmah Yake mwenye kuyatenda.
Hadiyth ifuatayo imeyaelezea baadhi ya madhambi hayo makubwa ambayo yanajulikana Sab'ul-Muwbiqaat (saba yenye kuangamiza).
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟ قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!)) Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni kumshirikisha Allaah, sihri [uchawi], kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika)). [Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, Abu Daawuud]
Madhambi hayo makubwa ni haya yafuatayo ambayo yametajwa katika Hadiyth hiyo juu na mengine mengi ambayo baadhi ya ‘Ulamaa wamejaribu kuyaorodhesha kwa kuyanyambua kutoka katika Qur-aan na Sunnah kulingana na makatazo, makemeo, laana, na adhabu zake, kama vile madhambi 70 aliyoyaorodhesha mwanachuoni mkubwa Imaam Muhammad bin ‘Uthmaan Adh-Dhahabiy kwenye kitabu chake Al-Kabaair:
1-Kumshikirika Allaah
2-Kuua
3-Uchawi
4-Kuacha Swalaah
5-Kutokutoa Zakaah
6-Kuacha kufunga Swawm ya Ramadhwaan bila udhuru
7-Kutokuhiji kwa mwenye uwezo
8-Kutokuwatii wazazi
9-Kuwahama na kuwakata jamaa na ndugu; kutengana nao
10-Uzinzi (kufanya zinaa)
11-Liwati (matendo ya kaumu Luwt; watu kuingiliana nyuma) mwenye kufanya na kufanywa wote wanaingia
12-Kula ribaa
13-Kula mali ya yatima na kumdhulumu
14-Kumsingizia Allaah na Rasuli Wake uongo
15-Kukimbia vitani
16-Kiongozi kuwa mdanganyifu kwa raia wake na kutokuwa muadilifu
17-Kiburi, majivuno na kujitukuza
18-Kutoa ushuhuda wa uongo
19-Kunywa pombe
20-Kamari
21-Kumsingizia mwanamke mtwaharifu tuhuma ya uzinifu
22-Kuiba ngawira za vita
23-Wizi
24-Ujambazi
25-Kutoa kiapo cha uongo
26-Dhulma (Kudhulumu)
27-Chumo la haramu
28-Kupata utajiri kwa njia za haramu
29-Kujiua
30-Kusema uongo (kila mara)
31-Kutohukumu kwa uadilifu
32-Kutoa na kupokea rushwa
33-Mwanamke kujifananisha na mwanamme na mwanamme kujifananisha na mwanamke kimavazi, kutembea, kuzungumza na mengineyo
34-Udayuthi, ukuwadi, na kutokuwa mwaminifu katika ndoa
35-Kumuoa mwanamke aliyeachika kwa talaka tatu ili awe halali kwa mume aliyemuacha kumrudia
36-Kutojilinda kurukiwa na mikojo
37-Riyaa (kujionyesha matendo mema)
38-Kutafuta elimu kwa maslahi ya dunia, na kuificha elimu uliyonayo
39-Kufanya khiyana
40-Kutangazia na kuhesabu mema uliyoyatenda
41-Kupinga Qadar
42-Kusikiliza siri za watu
43-Kuhamisha maneno (umbea)
44-Kulaani wengine
45-Kuvunja ahadi
46-Kuwaamini makuhani, watabiri, wapiga ramli (watazamiaji)
47-Mke kutomtii mumewe
48-Kutengeneza masanamu, vinyago, na picha
49-Kupiga mayowe, kuchana nguo, kujipiga na kujikatakata wakati wa msiba
50-Kutokuwa muadilifu kwa watu
51-Kutokuwa na huruma na kuwafanyia ujeuri mke, wafanyakazi, madhaifu na wanyama
52-Kumuudhi jirani
53-Kuwaudhi na kuwatukuna Waislamu
54-Kuwaudhi na kuwafanyia ujeuri watu
55-Isbaal (mwanamme kuvaa nguo ndefu inayovuka viwiko vya miguu kwa kiburi au ufakhari)
56-Mwanaume kuvaa hariri
57-Mtumwa kumkimbia bwana wake
58-Kutokuchinja mnyama kwa ajili ya Allaah
59-Kumwita mtu kwa ubini wa baba asiyekuwa wake huku unajua (kwa makusudi)
60-Kugombana na kupigana
61-Kuzuilia (watu) maji
62-Kupunja kipimo
63-Kujilinda na Aliyoyapanga Allaah
64-Kuwaudhi waja wema vipenzi vya Allaah
65-Mwanaume kuacha kuswali Swalaah ya jama’aah (Msikitini) na kuswali pekee bila udhuru
66-Kuacha kuswali Ijumaa kwa makusudi au kutotilia umuhimu na kupuuzia
67-Kubadilisha wasiyyah (aloacha mtu)
68-Kupanga njama na kufanya hila
69-Kuwapeleleza Waislamu kwa ajili ya makafiri na maadui
70-Kuwatukana Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum)
Hayo ni madhambi 70 aliyojaaliwa Imaam Adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) kuyakusanya kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Madhambi makubwa mengineyo:
71-Kusherehekea sikukuu za makafiri
72-Kunyoa nyusi
73-Kuunga nywele za bandia
74-Kujichora tattoo
75-Kuvunja mkataba (bila sababu ya ki-shariy’ah)
76-Kula nguruwe, nyamafu na damu
77-Kutoa kiapo cha uongo kwenye biashara
78-Kudharau na kuzikebehi Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ndevu, mswaki wa mti, kupunguza nguo isiburuze kwa wanaume n.k.
79-Kuwakebehi na wakuwapa majina mabaya wale wanaozifuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
80-An-Namiymah (Kufitinisha watu)
81-Ghiybah (kusengenya)
82-Kuamini nuksi (superstition), na kutabiri kwa nyota (horoscope), kutundika vitu na kuvaa kwa kuitakidi kuwa vinamlinda mtu na shari
83-Bid-ah za aina zote katika Dini
84-Kudanganya watu kupata maslahi ya kidunia
85-Kufanya israfu ya chakula na israfu katika sherehe ambayo inadhihirisha riyaa (kujionyesha kwa watu)
86-Kukufuru neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
87-Kuisoma Qur-aan kimakosa kwa kubadilisha maana za Maneno ya Allaah
88-Kuapa uongo kama kuapia kwa ajili ya kumvutia mteja biashara
89-Kughushi katika biashara kama kupunja au kuuza bidhaa mbovu
90-Mwanamke kutokujisitiri vizuri kwa hijaab ya ki-shariy’ah
Madhambi Madogo:
Madhambi madogo ni yale ambayo hayamo katika fungu hilo hapo juu nayo ni yale ambayo yamekusudiwa katika kauli ya Allaah (Subhanaahu wa Ta'aalaa):
الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ
Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogo-madogo. [An-Najm: 32]
Madhambi hayo ambayo Allaah Humghfuruia mja maadam mja hatoendelea kuyatenda kila mara kwani kuyaendeleza husababisha kugeuka kuwa ni madhambi makubwa. Mfano kuchanganyika wanawake na wanaume, mtu kuzungumza na asiye Mahram wake bila ya sababu ya ki-shariy’ah, husababisha kukaribia zinaa na huenda yakampeleka mja kutumbukia katika maasi hayo makubwa.
Madhambi madogo kama ilivyo dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba kila jema alifanyalo mja hufuta ovu lake kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾
Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka. [Huwd: 114]
Mfano kufanya wudhuu vizuri, madhambi madogo hupuputika.
Madhambi hayo pia yanaweza kuwa ni kama, kutazama picha na sinema chafu zisizofaa, kusikiliza maovu, kusikiliza na kuimba muziki, kutamka maneno maovu kama kutukana, kuwa na ghadhabu, na mengi mengineyo ambayo hayakuwekewa adhabu kali au laana, au ghadhabu ya Allaah.