Unavaa 'NIKE', Je, Unajua Maana Yake?

 

Unavaa 'NIKE', Je, Unajua Maana Yake?​

 

Alhidaaya.com

 

 

Sifa zote kamilifu njema anastahiki Allah Aliyetukuka Rabb Mlezi wa wa walimwengu wote ambaye hana mshirika katika Ufalme Wake. Swalaah na salamu zimshukiye kipenzi chetu Muhammad (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) ahli zake, Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ishara ya “NIKE” ikiwa ni kwa alama kama ya kupata kama ilivyo hapo juu au kwa neno lenyewe la “Nike” ambalo hutumiwa mara nyingi kuwekwa kwenye nguo za kuvaa au kwenye viatu vya michezo na mazoezi. Waislamu tunatakiwa kujiepusha kununua bidhaa hii, vile vile tujiepushe na kuivaa kwa wale ambao tayari wameshakuwa nayo majumbani.

 

Hii yatambulikana kama alama iitwayo “Nike” ambayo ni miongoni kwa alama kubwa zijulikanazo ulimwenguni. Hili jina ni jina la mijiungu (miungu) wa Ugiriki wa ushindi.

 

Wanavyuoni wa Kiislamu wanaonelea kwamba utumiaji wa bidhaa hii kwa Muislamu “ni Shirk” Kwani utapoinunua au kuivaa, utakuwa umeamini kwamba “Ninashahidilia ya kwamba, nina miungu mingine mbali na Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaaa) hata kama itakuwa hudhihirishi hilo hadharani, ila itakuwa  ina maana  hiyo. Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuepushe na kumshirikisha na chochote au yeyote kwani hiyo ndiyo dhambi kubwa kuliko dhambi zingine zote. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hayuko tayari Kusamehe dhambi hiyo, ila Yuko tayari Kusamehe dhambi zingine zote kama Asemavyo Mwenyewe katika Kitabu Chake.

 

Hapa chini tutawakilisha Historia fupi ya ishara au alama hii ya “NIKE” Isitoshe tutawakilisha madhara na hukmu kwa Muislamu yeyote ambaye atapuuzia hili na kuitumia ilihali kishafikishiwa hoja ya wazi.

 

Waanzilishi wa kampuni hii ya “Nike” ambao walipendeleza jina hili walikuwa ni Philip Knight na Bill Bowerman. Walichagua jina hili kama ishara ya bahati na matumaini ya ushindi kwa wanamichezo ambaye alikuwa akiivaa hii alama kwa propaganda za kueneza ishara ('Iymaan) ya kijiungu hichi ulimwenguni.

 

Hizi ni habari zinazojulikana vizuri kwenye mitandao mbali mbali. Angalia tovuti ya Wikipedia.org kwenye mtandao. Katika makala juu ya mada hii, ukiangalia kwenye kamusi ya Al-Mawrid inasema hivi:

 

“Nike” alikuwa ni kijiungu cha ‘victory’ (ushindi) katika zama za kale, Allaah ambaye alikuwa akiwakilishwa kwa umbo akiwa na mbawa na ni kijana, akibeba taji kwenye mkono mmoja na mwignine kabeba mitende.

 

Al-Mawrid Qamuus ‘English/Arabic’ (Ukurasa wa 613)

 

Hali kadhalika, tunapata habari hizo hizo kwenye kitabu kinachoitwa Al-Mu'taqadaat Al-Diyniyyah 'inda al-Shu'uub. Kutoka kwa Geoffrey Barrinder, kilichochapishwa kwa lugha ya kiarabu kwenye Silsilat 'Aalam al-Ma'rifah, namba 173 (Ukurasa wa 409)

 

Hili lipo wazi kwamba haifai kwa Muislamu kuvaa (kutumia) ishara hii au kuiga wale wanaoivaa. Waislamu tunaamini Tawhiyd (Kumpwekesha Allaah Mwenyewe bila ya mshirika) na tunaamini ya kwamba ‘victory’ (ushindi), msaada na uwezo unatokana na Allaah (na si vijiungu mbalimbali).

 

Uvaaji wa alama hii ni kinyume na imani ya Muislamu. Kama Muislamu huyo hana chaguo (hana budi) bali kununua bidhaa za kampuni hii au katenzwa nguvu namna fulani, basi angalau anapaswa kufuta/kutoa alama yao na jina hivyo basi isionekane juu ya kifua, mguu wake n.k. Na kwa hali hiyo basi ‘Aqiydah yake ya dini au itikadi yake itakuwa salama.

 

Na tusisahau kwamba mafanikio yetu sisi hapa Dunia na huko Aakhirah ni Tawhiyd.

 

Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kasema:

 

“Kuhusiana na picha, kama picha ambayo huonekana kwenye nguo za watu wazima na watoto, hali kadhalika. Si halali kwa mtu kuvaa kitu na picha juu yake (ya kiumbe mwenye roho), au kuwavalisha watoto wake wavulana au wasichana, kitu chochote ambacho kiko na picha juu yake”

 

Kuhusiana na maneno yameandikwa juu ya mavazi, kama vile kuandikwa hivi "Mimi ni Mkristo " juu ya koti, au "Mimi ni Myahudi," au "Mkristo" au "Mtu wa ngono" au kuandikwa alama au maneno ya kijinsia ima ya kike au kiume ambayo ni ishara ya maadili mabaya, na pia kuandikwa "Mungu wa upendo wa Kigiriki wa kale" au "Mpenzi wa pombe" au jina la mwanaume na mwanamke, au "Christmas" - yote haya haikubaliki katika Uislamu na yanakwenda kinyume na maadili yetu ya Kiislamu.

 

Jambo muhimu la kufanya kwa sisi waislamu, ni sisi kususia hizi nguo zote zenye ishara/alama au maneno kama tulizowakilisha hapo juu kukiwemo ishara ya “Nike”.

 

Inasikitisha sana kuona kwamba kuna vijana wa Kiislamu wanaume na wanawake wakiwa na nguo au bidhaa mbali mbali zikiandika maneno kama yafuatayo “Mimi ni mkristo” au “Mimi ni myahudi” nk. Kwanini Waislamu tumekuwa wajinga kiasi hichi na kutofakharisha dini yetu ya Kiislamu na kuipatia thamani? Hao hao wanaotupiga vita na kutuuwa usiku na mchana ndiyo tunaowafanya vipenzi wa karibu na kuwaiga kwa machafu yote wanayokuja nayo bila ya kuangalia khatari au nini lengo khaswa ya kuleta uchafu kama ule.

 

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kumfikishia muislamu khatari ya kuigiza ishara kama hizi, na vilevile kumkumbusha yule aliayeghafilika na kumuonesha madhara ya kuiga ishara kama hizi khaswa ya ‘Nike’. Na kwa wewe ambaye umefikiwa na mawaidha haya kwa njia yoyote ile na ukaikaa kimya kwa kupuuzia kutotanabaisha wenziwe, basi jua ya kwamba utaulizwa hilo siku ya Qiyaamah kwa jambo hili zito ambalo ni sawa na kumshirikisha Allaah. Jambo ambalo Allaah Anaonesha hukmu na uzito wake ndani ya Qur-aan pale Aliposema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa :48]

 

Allaah Anazidi Kukariri na kuonesha khatari ya Shirki, pale Aliposema:

 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

Siku hayatofaa mali wa watoto. Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu'araa : 88-89]

 

Ole wao wale ambao watafikiwa na darsa hili zito la Tawhiyd, wakawa kama wenye kudharau na kutoona uzito na madhara yake. Na ole wao wale ambao watafikishiwa na wakawa na uzito wa kufuata haki na kupuuzia na kujipatia matumaini ya kufikiria kwamba hii ni dhambi ndogo tu na kuna makubwa ya kuangalia mbali na hili kama wasemavyo wengi.

 

Sidhani kwamba kuna ushirikina mbaya kushinda huu, wa kujua kwamba ishara/alama hii ya Nike ni kijiungu cha hapo kale kilichokuwa kikiabudiwa. Ila wewe kwa ubishi wako na jeuri ukawa hutolipatia uzito kwa kutolihadhari Waislamu utapoliona, au kutolifikisha kwa wengine kwa kuhofia wasije tumbukia kwenye shirki kama hii.

 

Sisi waislamu wajibu wetu tunaoweza kufanya ili kujitenga mbali na hili, kwanza ni sisi kususia bidhaa zote zenye alama (Ishara) kama hii ya ‘Nike’, na kutotumia pesa zetu kwa mambo ambayo ni khatari kwetu wenyewe. Khatari kubwa ni kwa mzazi kumnunulia mtoto wake nguo kama hizi zenye ishara na meneno kama haya ya kishirikina. Na mtoto kutokana na akili zake finyu, akakulia kwenye imani ile ile ya ushirikina mpaka hapo atakapokufa, na chanzo ni wewe mzazi ambaye ulikuwa huliwekei uzito na kulikemea tangu hapo mwanzo.

 

Allaah Anasema ndani ya Kitabu Chake kuonesha khatari na madhara ya kuwafanya makafiri na mayahudi marafiki na vipenzi.

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ ۘ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٥١﴾فَتَرَى الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ يُسَارِعُونَ فِيهِمْ يَقُولُونَ نَخْشَىٰ أَن تُصِيبَنَا دَائِرَةٌ ۚ فَعَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَ بِالْفَتْحِ أَوْ أَمْرٍ مِّنْ عِندِهِ فَيُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا أَسَرُّوا فِي أَنفُسِهِمْ نَادِمِينَ ﴿٥٢﴾

Enyi walioamini! Msifanye Mayahudi na Manaswara marafiki wandani. Wao kwa wao ni marafiki wandani. Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu.Basi utawaona wale ambao katika nyoyo zao mna maradhi (ya unafiki) wanakimbilia kwao wakisema: Tunakhofu usitusibu mgeuko. Basi asaa Allaah Akaleta ushindi au jambo (jengine) litokalo Kwake; wakawa wenye kujuta kwa waliyoyaficha katika nafsi zao. [Al-Maaidah: 51-52]

 

Kwa kumalizia tunakariri na kukumbusha Waislamu tena kugomea bidhaa/maneno haya ya kikafiri. Na kwa wale Waislamu ambao wanafanya biashara ya kuuza bidhaa kama hizi, ni wajibu kwetu kuonana nao na kuwakumbusha wamuogope Allaah, na kutoa tahadhari ya hilo. Kwa sababu baadhi ya wachuuzaji hawajui Kingereza na hawajui nini kinachoandikwa kwenye maguo kwahiyo wanavamia tu kununua na kuanza kuuza.

 

Muislamu huwezi kufilisika mali yako au biashara yako ikiwa utamtegemea Allaah na kususia kuuza bidhaa zote zenye ukafiri na ushirikina kama huu.  Badala yake ukifanya au kuacha kitu kwa ajili ya Allaah, basi Allaah  Anakupatia lililo bora na zuri kuliko lile la mwanzo.

Hata majina ya waimbaji wana muziki na wanasoka (mpira) nyota na wengine ambao si Waislamu, na kuvaa mavazi yenye majina au picha au nembo ya mambo haraam kama pombe, kamari, muziki, na matangazo yoyote ya haramu au ya uharibifu wa maadili, yote hayo Muislamu anatakiwa kujiepusha kuyatumia, kuvaa na kununua au kuuza.

 

Tunamuomba Allaah  Atuepushe na Ushirikina na kutumbukia katika Ukafiri kwa kujua au kutokujua. Na tunamuomba Allaah Awawekee wepesi katika kupokea yale yatakayokuwa mazuri ndani ya makala hii na kuyafanyia kazi kwa ajili ya kutarajia radhi Zake (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

 

Share