Kiwango Cha Zakaah Ya Dhahabu

 

SWALI

 

Assalaam aleykum,
Kwanza kabisa namwomba Mola awajaze heri nyinyi na sisi katika kuhangaikia dini ya Allah. Nimevutiwa mno na jibu lenu juu ya mwenye kuchagua Ibada ya faradhi.
Kuna kauli inasema kiwango kifikie gram 82.5 za dhahabu, na kuna kauli nyingine inasema kiwango kifikie dirhamu 200, kisha nikaona tena katika gazeti la An Nur limetaja kiwango cha laki tano kwa pesa za Tanzania Naomba uchambuzi wa kukinaisha
Wabillahi Tawfiq
Ndugu yenu katika imani

 

 

 


 

 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa ndugu yetu aliyetaka kutatuliwa utata aliokuwa nao katika mas-ala ya Zakaah, lakini hakika ni kuwa hakuna utata aina yoyote katika hilo.

Katika mas-ala haya yapo mambo ambayo ni thabiti na yasiyobadilika. Na moja katika hilo ni wizani wa dhahabu au fedha lakini hela za kila nchi zitabadilika. Jambo ambalo halibadiliki ni ile kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliposema:

 

“Haipasi Zakah mali iliyochini ya wakia 5” (Al-Bukhariy).

 

Kulingana na Hadiyth hii ni lazima uwe na wakia 5 ya mali ambayo itapitiwa na mwaka kulingana na kalenda ya mwezi mwandamo ndio utoe Zakah. Sasa hizi wakia 5 ni kima gani katika madini ya dhahabu na fedha?

 

Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  pesa aliyokuwa akitumia ni dinari (yaani ya dhahabu - gold) na dirhamu (ambayo ni ya fedha – silver). Ikiwa ni kwa dinari basi ni 20 na dirhamu ni 200. Kwa hivyo hao waliotumia dirhamu ndio wameandika kima hicho cha 200. Kwa wakati wetu huu hela hizo hazitumiki kwa hivyo wanazuoni wamejaribu kuzibadilisha kwa kipimo cha gramu ndio wakatupatia viwango ikiwa ni dhahabu basi ni baina ya gramu 82.5 mpaka 88.  Hii ni kuonyesha wanazuoni wametafautiana na ndiyo ikachukuliwa kile kiwango cha chini cha gramu 82.5.

 

Ingawa kuna Maulamaa wamechagua kiwango cha kati ambacho ni gramu 84 au 85 na kuonelea ni bora zaidi kwani hakitakuwa chini wala juu. Na ikiwa ni katika fedha basi nisaab ni gramu 595.

 

Kwa Tanzania gramu moja ya dhahabu ni shilingi 15,000 na kwa hiyo Nisaab itakuwa ni shilingi 1,237,500. Na kwa Kenya hivi sasa gramu moja ya dhahabu ni shilingi elfu, hivyo nisaab ni shilingi 82,500, hivyo kwa uhakika ni bora kwenda kwa sonara na ukauliza bei ya gramu moja ukishapata utaijumlisha na 82.5 na hapo utapata kima kwa fedha za huko.

 

Na ikiwa mtu yupo nchi yoyote katika ulimwengu hesabu itakuwa hivyo hivyo, atazidisha bei ya gramu ya dhahabu kwa 82.5.

 

Na baada ya kupata kujua kiwango cha Nisaab, basi unatakiwa katika kiwango hicho utoe 2.5% ya fedha zote. Yaani katika hiyo shilingi 1,237,500, aslimia mbili nukta tano ni shilingi 30,937 na senti 50 za Tanzania. Na ikiwa utafuata rai ya Maulamaa wengi ya gramu 85, basi utapata jumla ya shilingi  1,275,000. Kwa hiyo 2.5% ya hiyo ni shilingi 31,875 za Tanzania

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share