Kijana Mwenye Taqwa Anasema Yeye Ni Ahlus Sunnah, Anataka Kuniposa Nataka Kujua Kwanza Nani Ahlus Sunnah Wal Jama’ah, Salafi

SWALI:

 

Salaam aleykum

 

Mimi ni msichana, nimepata kijana nataka kuoana nae lakini huyo kijana  hawezi kunioa mpaka nijue nani ni wahhabi na salafi kwa sababu yeye ni ahlul sunna, na mimi ni sunni pia, lakini hawezi kunioa mpaka nijue hayo madhab, sasa na mimi sielewi hao ni watu gani, ningeomba mnifafanulie ili niweze kuelewa kwa upana, huyu kijana ni mcha mungu sana mashaAllah na mimi sitaki kumkosa na yeye hawezi kunioa mpaka nijue hayo mambo, tafadhali kama mtaweza kunijibu haraka ili nimjulishe huyu kijana tupate kuoana.  Mwenyezi mungu awazidishie ameen.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kutaka kuolewa na kijana wa Ahlus Sunnah.

 

Ahlus Sunnah ni Waislamu wenye msimamo wa kufuata Sunnah sahihi za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Jama’ah ni kuwa pamoja na Maswahaba, bila kujali matokeo yake na watakavyosema watu. Kuiga huku kwa kipenzi chao na kielelezo kunawafanya wao wapate ucha Mungu na pia kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Ama jina jingine la Salaf lina maana ya watangu au watu waliopita, na mara nyingi huwa yanatumika maneno mawili pamoja Salafus Swaalih (watangu wema). Kwa ufupi, maneno haya yana maana watu wema waliopita. Na wenye kufuata msimamo huo ni kuwa wanafuata vilivyo nyendo za Maswahaba na watu wema waliojikita katika kutekeleza Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hivyo, Salafus Swaalih na Ahlus Sunnah ina maana moja – kufuata Sunnah vilivyo. Ama Uwahabi au Wahabi ni jina la chuki na kutuhumi wale wenye msimamo madhubuti miongoni mwa Ahlus Sunnah, na waliooneza jina hilo ni kutokana na jina la baba wa mwanachuoni mkubwa aitwaye Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab. Na mwanachuoni huyo Shaykh Muhammad ‘Abdul-Wahhaab alikuwa mkakamavu katika kupinga na kupigana na kila lenye kwenda kinyume na muongozo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, mwenye kuitwa Wahabi ni yule mwenye kufuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vilivyo.

 

Soma zaidi kuhusiana na habari za mwanachuoni huyo hapa:

 

 

Ahlus Sunnah wal Jama’ah Ni Nini? Ipi Historia Yake Na Malengo Yake? Na Zipi Kasoro Zake?

 

 

 

Imaam Muhammad Ibn Abdul Wahhaab - Maisha Yake Na Harakati Zake

 

 

Nani Muhammad Abdul-Wahhaab Na Kundi La Twariqa Ni Kundi Gani?

 

Uwahabi: Ufafanuzi Na Majibu Juu Ya Majungu Dhidi Ya Shaykh Muhammad 'Abdul-Wahhaab

 

Marekebisho Yanayohusiana Na Kuelewa Kimakosa Taariykh (historia) Ya “uwahabi”

 

Kwa hiyo, ikiwa kweli huyo kijana ni Ahlus Sunnah au Salaf au Wahabi basi atakuwa ni kijana mzuri wa msichana kuolewa naye. Hata hivyo, nasaha tunayokupatia ni kuwa hakikisha vilivyo kuhusu ukweli wa habari hiyo kabla ya kuingia katika matatizo. Mwanzo, anza kuswali Swalah ya Istikhaarah, ili kumtaka ushauri Allaah Aliyetukuka. Na pia, jaribu kupata habari kumhusu kijana kupitia kwa wazazi wako au ndugu zako wa kiume.

 

Ikiwa hayo yote utakayoyapata ni kama hivyo basi InshaAllaah mtegemee Allaah na itakuwa ni kheri kwako. Nasi hapa tunakutakia kila la kheri katika kheri hiyo ya ndoa yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share