Kufuturu Kwa Mchumba Uliyelipa Mahari

SWALI:

 

Kufuturu kwa mchumba ambaye umelipa mahari inaruhusiwa mwezi wa Ramadhani?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kufuturu kwa mchumba ambaye tayari umelipa mahari yake.

Unapaswa kufahamu kuwa huyo bado hajakuwa ni mkeo au haki yako kishari’ah.

Tunaona baadhi ya nchi za Kiarabu na hata Asia huwa kuna tabia ya wachumba ambao hawajafunga ndoa kuvishana pete na kuwa na maingiliano ya wazi yasiyo na mipaka. Hutembea pamoja, hushikana, na hata kuwa faragha. Wanachodhani wao kisichofaa ni kuingiliana kindoa tu! Hayo ni makosa makubwa na haifai na pia ni haraam na hupelekea pia watu kuingia kwenye zinaa kabla ya ndoa na hata wengine kufikia kutooana tena baada ya kuchezeana.

Huwezi kufuturu kwa huyo mchumba wako hadi kuwepo na Mahrimu zake pamoja nanyi. Kukipatikana hilo, basi hakuna tatizo lolote ikiwa kutachungwa mipaka ya kishari’ah. Na sharti kubwa ni kutokaa faragha wewe na yeye tu bila na kuwa na aliye Mahrimu yake kuwa hapo. Kwa muhtasari, ni kuwa unaweza kufuturu kwao kukiwepo na mfano baba yake, mama yake, kaka yake au mtu asiyeweza kumuoa.

Ama wewe na yeye peke yenu hilo haliruhusiwi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share