Anataka Kuhiji Lakini Ana Deni La Nyumba Benki

 

Anataka Kuhiji Lakini Ana Deni La Nyumba Benki

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalam Alekum,

 

Swali langu ni: - Mimi nina deni la nyumba bank, hali ninaweza kwenda kuhiji? Ninaomba msaada wenu kwani mimi sina elimu ya kutosaha. Waasalam

 

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ieleweke kuwa Hijjah ni nguzo ambayo inampasa kuitekeleza yule Muislamu mwanamume au mwanamke aliye na uwezo wa kuiendea njia hiyo – kwa kuwa na hela za kutosha kwa safari hiyo, kuwa na usalama katika safari, kuacha masrufu kwa wale wanaokutegemea huku nyuma unapoondoka.

 

 

Katika hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. [Al-'Imraan: 97].

 

 

Na katika Hadiyth ndefu ya ‘Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuhusu Jibriyl (‘Alayhis-salaam) aliyekuja kumuuliza maswali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipoulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Uislamu alisema, "…na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo" (Muslim, At-Tirmidhiy na Abu Daawuud).

 

 

Kawaida ya mkopo wowote inakuwa mkopesha na mkopeshwa na hasa ikiwa ni kutoka Benki wanaandikia kuhusu malipo hayo. Kwa mfano, ikiwa kila mwezi mdaiwa anatakiwa kulipa shilingi 100,000 kwa muda wa miaka kumi. Ikiwa mdaiwa ana pato zaidi ya hilo analolipa akaweza kuweka akiba ya hela kwa kiasi ambacho kinatimiza masharti ya kwenda Hijjah kama tulivyotaja hapo juu kutakuwa hakuna shida yoyote kwake kwenda Hijjah, japokuwa kimsingi ana deni.

 

 

Ikiwa kwenda kwake Hijjah kutamfanya asilipe deni lake analodaiwa au aruke kwa miezi kadhaa itakuwa bado hajakamilisha masharti kwa yeye kufunga safari hiyo ya mara moja katika uhai wake.

 

 

Tanbihi: Tunawapatia nasaha dada na ndugu zetu kuwa mikopo ya Benki za kawaida ina riba ambayo mdaiwa anaipatia banki. Hivyo, kuifanya mikopo aina hiyo kuwa haramu. Mara nyingi watu wamefilisika kwa kukiuka agizo la Muumba, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Tuwe na tahadhari sana katika mas-ala hayo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share