Kuvaa Nguo Ya Kijani Katika Kutimiza Fardhi Ya Hajj Ni Sunnah?

 

Kuvaa Nguo Ya  Kijani Katika Kutimiza Fardhi Ya Hajj Ni Sunnah?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali: 

 

Asalam aleykum

 

Mimi nakwenda Hajj mwaka huu, napenda kuuliza kuhusu nguo ya kijani, maana nimeambiwa kuwa nivae nguo ya kijani baada ya kumaliza hajj yaani siku ya sikukuu, na hivyo ndivyo wanavyofanya watu wetu wanaokwenda hajj kuwa wote wanavaa nguo ya kijani siku ya sikukuu. Je, hii ni Sunna kufanya hivyo?

 

Nitafurahi kupata jibu mapema

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakuna dalili yoyote inayutupa mafunzo kuwa tuvae nguo za kijani katika ibada ya Hajj.  Imetajwa tu rangi ya kijani  katika Qur-aan kuwa ni nguo ambazo watakazovishwa watu wa peponi:

عَالِيَهُمْ ثِيَابُ سُندُسٍ خُضْرٌ وَإِسْتَبْرَقٌ ۖ وَحُلُّوا أَسَاوِرَ مِن فِضَّةٍ وَسَقَاهُمْ رَبُّهُمْ شَرَابًا طَهُورًا﴿٢١﴾

Juu yao wana nguo za hariri nyororo za kijani na za hariri nyororo za makhmel na watapambwa vikuku vya fedha; na Rabb wao Atawanywesha kinywaji cha kitwaharifu. [Al-Insaan: 21]

 

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aa'aal anatuambia:

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿٣٠﴾أُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِّن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ ۚ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٣١﴾

Hakika wale walioamini na wakatenda mema, hakika Sisi Hatupotezi ujira wa anayetenda ‘amali nzuri kabisa. Hao watapata Jannaat za kudumu milele zipitazo chini yao mito, watapambwa humo vikuku vya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri laini na hariri nzito nyororo; wakiegemea humo kwenye makochi ya fakhari. Uzuri ulioje wa thawabu na mahali pazuri palioje pa kupumzikia. [Al-Kahf:30-31]

 

Juu ya hivyo, kuvaa nguo za kijani baada ya kumaliza Hajj kunaleta picha kwamba Mahujaji hao wamekubaliwa Hijjah zao na kuwa wameshakuwa ni watu wa Peponi. Hivyo sio sawa kwani Muumini  anatakiwa anapotenda vitendo vyema awe baina ya khofu na mategemeo (ya kukubaliwa vitendo). Na khofu iwe zaidi kuliko mategemeo kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾

Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao. [Al-Muuminuwn: 60] 

 

Na katika Hadiyth:

 

حَدَّثَنَا أَبُو بَكْرٍ، حَدَّثَنَا وَكِيعٌ، عَنْ مَالِكِ بْنِ مِغْوَلٍ، عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ سَعِيدٍ الْهَمْدَانِيِّ، عَنْ عَائِشَةَ، قَالَتْ قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَهُوَ الرَّجُلُ الَّذِي يَزْنِي وَيَسْرِقُ وَيَشْرَبُ الْخَمْرَ قَالَ ‏"‏ لاَ يَا بِنْتَ أَبِي بَكْرٍ - أَوْ يَا بِنْتَ الصِّدِّيقِ - وَلَكِنَّهُ الرَّجُلُ يَصُومُ وَيَتَصَدَّقُ وَيُصَلِّي وَهُوَ يَخَافُ أَنْ لاَ يُتَقَبَّلَ مِنْهُ ‏"‏ ‏.‏

 

'Aaishah (رضي الله عنها) alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):  Ee Rasuli wa Allaah:

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾

Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao. [Al-Muuminuwn: 60] 

 

Je, huyo ni mtu ambaye anazini, anaiba na anakunywa pombe? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akajibu: “Sio ee bint wa Abubakar, (au) binti wa As-Swiddiyq! Lakini huyo ni mtu ambaye anafunga (Swiyaam), na anatoa swadaqa, na anaswali na huku anakhofu asitaqabaliwe. [Sunan Ibn Maajah].

 

Hayo yote ni kujikalifisha tu kutafuta nguo haswa ya kijani, kwani kama mtu hana, inambidi ahangaike kutafuta na hali mtu anaweza kuvaa nguo yoyote ile.  Dini yetu ni nyepesi lakini sisi wenyewe tunajikalifisha kwa kufanya mambo yasiyo na dalili.  

 

Kwa maelezo zaidi bonyeza hapa kwenye Swali lenye kuhusu maudhui hii:

 

Nguo Za Rangi Ya Kijani Zina Maana Gani?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share