Ikiwa Haifai Mtu Kupita Mbele Ya Mwenye Kuswali, Mbona Makkah Watu Wanapita Mbele Ya Wanaoswali?
SWALI:
asalamun alaykum
natumai nyote hamjambo na poleni kwazi zenu.
mm nilikua anwauliza hivi nilisoma kuhusu lile suali mtu aliyeuliza kumpitia mtu aneswali mbele yake je inafaa au haifai? Na nyinyi mkamjibu kua haifai sasa nimi nauliza kule makka hua inakuaje? Ikiwa watu wanasali na wengine wanawapitia mbele yao? Naomba hili suali langu la mara hii mnijibu kwani nimewauliza suali langu lakini mpaka sasa hamkunijibu basi naomba ufafanuzi wenu.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusiana na mtu kupita mbele ya mwenye kuswali akiwa Makkah.
Awali ya yote tungependa kukufahamisha kuwa maswali huwa hayachelewi kwetu kwa kupenda kwetu. Maswali yanajibiwa kama yanavyopokewa, ikiwa swali lako limechelewa kujibiwa ni kwa sababu ya kuwa kulikuwa na maswali mengi yaliyotufikia kabla ya maswali yako. Kwa ajili hiyo, yanajibiwa yaliyokuja mbele kabla ya kujibiwa yale yaliyofika kwetu baadaye.
Kama kila Muislamu anavyofahamu kuwa matendo yetu sote katika kila jambo yaambatane na shari’ah ya Kiislamu. ‘Ibaadah zetu, kazi tunazofanya, mazungumzo yetu na ‘amali zetu zote. Kufaa jambo lolote au kukatazwa yote hayo ni lazima yafuate kanuni za kawaida za Kiislamu. Kufaa jambo lolote lazima litoke katika nyenzo za shari’ah na kutofaa pia ni lazima iende sambamba na kanuni hiyo.
Huenda kufaa jambo lisieleweke katika mizani ya akili ya mwanaadamu au kutofaa pia kusieleweke katika mantiki yake finyu. Hata hivyo, Muislamu mwenye Imani barabara anakuwa ni mwenye kutii na kukubali kwa unyenyekevu yale yote yaliyothibiti kutoka katika Qur-aan na Sunnah sahihi, Allaah Aliyetukuka Anasema:
“Yeye ndiye Aliyekuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aayah Muhkam (zenye maana wazi na nyepesi kufahamika). Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine Mutashaabihaat (zinababaisha zisizo wazi kufahamika). Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za kubabaisha kwa kutafuta fitna na kuharibu watu, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Allaah. Na wale wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili” (Aal-‘Imraan 3: 7).
Mas-ala ambao wamekosa kufahamu hikma ni mengi kuwafanya watu warudi nyuma katika Dini yao au kutiwa tashwishi na watu wenye kupenda fitna katika Ummah. Watu wamekuwa ni wenye kusuali vipi punda wa mjini ni haramu ilhali punda milia ni halali na inaonekana kuwa wamefanana sana te na sana. Muislamu akishaanza kufikiria hayo basi mara moja hudhoofika Imani na kuingia katika mashaka na matatizo bila kutarajia au akatiwa katika hayo na watu wasioupenda Uislamu japokuwa wanajiita kuwa wao ni Waislamu.
Tukija katika kadhiya unayoitaja si Makkah tu bali unaweza kupata Misikiti mingine mikubwa yenye kjuingiza idadi kubwa ya watu. Na kuhusu hilo ni kuweza tu kuelewa kanuni za Swalah na za sutrah. Na uhakika ni kuwa anaposwali Imaam na akaweka kizuizi (sutrah) mbele yake hatahitaji maamuma kuweka kizuizi, kwani sutra ya Imaam ndio sutrah ya maamuma, na palikuwa panasimikwa kijimkuki kama sutrah kwa ajili ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akiswali kuelekea pale na hakuamrisha yeyote aliye nyuma yake kuweka sutrah nyingine (al-Bukhaariy na Muslim). Kwa ajili hiyo, hata katika Misikiti mingine sio Makkah peke yake ikiwa Imaam amefunga Swalah tayari yeye amekuwa ni sutrah kwa wengine, maamuma, hivyo, ikiwa mtu atapita mbele ya maamuma kwa dharura yoyote basi hatoharibu Swalah ya mwenye kuswali. Lakini haifai hata hivyo pamoja na kuruhusika huko, mtu kujipitia pitia ovyo bila dharura wala sababu za msingi kwani vilevile atakuwa anawatia watu tashwishi na kuharibu khushuu yao.
Na endapo mtu anaswali Swalah isiyo ya Jama’ah basi mtu anatakiwa aweke sutrah (kizuizi) mbele yake na inatakikana mtu mwengine asipite mbele yake hata kama ni Makkah, kuwepo Makkah si udhuru wa kuvurugwa watu Swalah zao za fard (isiyo Jama’ah) kwani Mtume wetu amelikataza vikali hilo kama inavyoeleza Hadiyth hii:
Imepokewa na Abu Juhaym bin al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Lau angejua mwenye kupita mbele ya mwenye kuswali madhambi anayopata, ingekuwa bora kwake kusimama (asipite mbele yake) arobaini kuliko kupita mbele yake” (Al-Bukhaariy na Muslim). Na katika riwaya ya al-Bazzaar inasema: “Miaka arobaini”. Hadiyth hii inatuonyesha dhambi kwa mtu kupita mbele ya mwenye kuswali.
na wala kuona kwako kwenye Televisheni au kwa kuzuru kwako na kuona hali hiyo, sio ikwa ndio dalili au ushahidi wa dini kuwa jambo kama hilo linapendeza au kukubalika! Ni sawa na wale unaowaona wanaparamia Al-Ka’abah na kuibusu au kujipangusia Baraka za Kitambaa kilichofunikiwa Al-Ka’abah, au kukibusu na wakawa wanasababisha msongamano mkubwa kwa kung’ang’ania kwao kama popo au tumbili kwenye kuta hizo! Kwa hiyo matendo yanayofanywa na watu japo ni wengi au japo kwenye sehemu tukufu, haimaanishi ndio shari’ah au ndio dalili ya kusihi au kukubalika jambo.
Na Allaah Anajua zaidi