Iyd: Inapoangukia Ijumaa, Nini Hukmu Ya Swalaah Ya Ijumaa?
‘Iyd Inapoangukia Ijumaa, Nini Hukmu Ya Swalaah Ya Ijumaa?
SWALI:
Assalam alaykum
Je, vipi Idi ikiaangukia kuwa ni siku moja na Ijumaa ? Inapasa Waislamu wasali sala zote mbili jamaa?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hili ni swala lenye khitilafu baina ya ‘Ulamaa. Wako walioona kwamba Muislamu aswali Swalaah zote mbili; ‘Iyd na Ijumaa kwa Jamaa’ah, na wako walioona kuwa akiswali Swalaah moja baina ya mbili inamtosheleza. Dalili zifuatazo zimetumika kuhukumu hayo mawili:
Kauli Ya Kwanza: Kuwajibika Kuswali ‘Iyd na Ijumaa kwa Jamaa’ah:
Hii kauli ya ‘Ulamaa wengi. Nao hoja yao ni:
1-Ujumla wa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ
9. Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. [Al-Jumu’ah 62:9].
2-Dalili zilizotangulia kuhusiana na uwajibu wa Swalaah ya Ijumaa.
3-Na kwa sababu Swalaah zote hizo mbili ni waajib (pamoja na kuwa kuna khitilafu kuhusu uwajibu wa Swalaah ya ‘Iyd) hivyo haiwezi kuanguka (kuachwa) Swalaah mojawapo kwa sababu ya nyingineyo, kama vile Adhuhuri pamoja na ‘Iyd. Hivyo basi haianguki mojawapo.
4-Ruhusa imetolewa kutokuwajibika Swalaah ya Ijumaa kwa wanaoishi mbali ya mji kutokana na dalili ifuatayo:
Kutoka na Abu ‘Ubayd mkombolewa wa Ibn Azhar amesema: Niliswali Swalaah ya ‘Iyd pamoja na ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ilikuwa ni siku ya Ijumaa, akaswali kabla ya khutbah, kisha akakhutubia na kusema: “Enyi watu, hakika hii ni siku iliyoungana sikukuu mbili. Hivyo basi atakayependa miongoni mwa wanaoishi mbali asubiri Swalaah ya Ijumaa, na anayependa kurudi kwake ameruhusiwa” [Al-Bukhaariy]
Kauli Ya Pili: Kuanguka Swalaah Ya Ijumaa Na Kuswaliwa Adhuhuri Lakini Imaam Inapendekezwa Awepo Ili Awaswalishe Wanaotaka Kuswali Ijumaa Na Pia Wale Walioikosa Swalaah Ya ‘Iyd
Na hi ni kauli ya Wanachuoni wa Ki-Hanbali na imesimuliwa pia kuwa ni kutoka kwa ‘Umar, ‘Uthmaan, ‘Aliy, Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas na Ibn Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhum).
Kutokana na dalili zifuatazo, kutoka kwa ‘Atwaa ambaye amesema: “Alituswalisha Ibn Az-Zubayr mapema mchana siku ya ‘Iyd iliyokuwa pia Ijumaa. Kisha tukaenda kuswali Ijumaa lakini hakufika yeye. Akatuswalisha mmoja wetu na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuwa Twaaif. Aliporudi akajulishwa hayo. Akasema: “Imetimizwa Sunnah.” Ikamfikia habari Ibn Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: Nimemuona ‘Umar Ibnul-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akifanya hivyo wakati inapoungana sikukuu mbili (‘Iyd na Ijumaa).” [Abu Daawuwd, An-Nasaaiy].
Pia kutoka kwa Abu ‘Abdir-Rahmaan As-Sulamiy ambaye amesema: “Zilikutana sikukuu mbili katika zama za ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawaswalisha watu Swalaah ya ‘Iyd kisha akakhutubia katika kipando chake akasema “Enyi watu, atakayeswali ‘Iyd atakuwa ameshatimiza Ijumaa yake In Shaa Allaah.” [Na katika riwaaya nyingine] “Anayetaka kuunganisha aunganishe, na anayetaka kubakia abakie.” Akasema Sufyaan: “Inaamanisha akabakie nyumbani kwake.” [Swahiyh kutoka kwa Ibn Abi Shaybah, ‘Abdur-Razaaq na Ibnul Mundhir].
Lakini Maimaam katika miji ni bora waimamishe (waswalishe) Swalaah ya Ijumaa ili waswali wenye kupenda kuswali ambao tayari walishaswali Swalaah ya ‘Iyd na pia kwa wale ambao hawakuwahi kuswali Swalaah ya ‘Iyd.
Kutokana na ikhtilaafu hizo, rai iliyojumuishwa ni kwamba atakayeswali Swalaah ya ‘Iyd inamtosheleza Muislamu siku hiyo na hana haja tena kuswali Swalaah ya Ijumaa, bali inamtosha yeye kuswali Swalaah ya Adhuhuri makwao haswa wanaokaa mbali na mji.
Na kuna ‘Ulamaa wengine walioona kuwa yule aliyeswali ‘Iyd hana haja ya kuswali hata Adhuhuri kwani faradhi ya Ijumaa ilishaanguka kwake. Lakini, ni bora mtu kuswali Adhuhuri ikiwa hatoswali Ijumaa ili ajiepusha na utata na nafsi yake iwe tulivu kwa kutoikosa fardhi mojawapo kati ya Ijumaa na Adhuhuri, na pia kwa sababu Swalaah ya Adhuhuri kwa ambaye ameswali Swalaah ya ‘Iyd kisha ikamtosheleza na Swalaah ya Ijumaa, anapaswa kuiswali kwani hiyo ni fardhi isiyoanguka na wala hakuna Swahaba yeyote aliyeiacha kuiswali, kama tulivyoona kutoka kwa ‘Atwaa ambaye alisema: ‘Zilijumuika ‘Iyd mbili (‘Iyd na Ijumaa] katika zama za Ibn Zubayr akawaswalisha Swalaah ya ‘Iyd kisha akawaswalisha Swalaah ya Adhuhuri Rakaa nne.” [Swahiyh kutoka kwa Ibn Shaybah].
Na Allaah Anajua zaidi