Ijumaa: Kukosa Rakaa Swalaah Ya Ijumaa Uswali Vipi?
Kukosa Rakaa Swalaah Ya Ijumaa Uswali Vipi?
SWALI:
Aaww,
Nahitaji kujua ikiwa umechelewa kufika msikitini wakati wa swala ya ijumaa na ukakosa rakaa ya pili unatakiwa kufanya nini.
1. Je inatosha kumalizia rakaa ya pili peke yako?
2. Au unatakiwa kuswali swalat dhuhur?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.
Tungependa sana awali ya yote kuwanasihi sana ndugu zetu wawe na hima kubwa sana kufika mapema kwa ajili ya Swalaah ya Ijumaa. Umuhimu wake ni mkubwa mpaka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akatuamrisha tufunge biashara zetu na tuache kazi wakati kunapoadhiniwa kwa ajili ya Swalaah hiyo.
Swalaah hiyo inatupatia fursa sisi ya kuweza kujumuika na kusikiliza mawaidha ambayo yatatuweka sisi pazuri katika dunia yetu na Aakhirah. Pia kutupatia muongozo katika mas-ala tofauti.
Ama tukiingia katika suala lako tunasema kuwa ikiwa utapata rakaa moja ya Swalaah ya Ijumaa basi utakamilisha ya pili kama walivyotoa fatwa Maswahaba wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Amesema Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa):
"Mtu akipata rakaa siku ya Ijumaa, atakamilisha ya pili. Akiwakuta wameketi ataswali nne" ['Abdur-Razzaaq, Ibn Abi Shaybah na al-Bayhaqiy. Isnadi yake ni sahihi]
Pia imepokewa kutoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu):
"Mwenye kupata rakaa basi amepata Ijumaa, na anayekosa Ijumaa basi aswali rakaa nne" ['Abdur-Razzaaq, Ibn Abi Shaybah na al-Bayhaqiy. Isnadi yake ni sahihi].
Ameitaja hiyo Shaykh al-Islaam, Ibn Taymiyyah kama hivyo kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu):
"Wala haijulikani kutoka kwa Maswahaba kwenda kinyume na hilo. Wamezungumza zaidi ya mmoja kuwa kauli hiyo ni Ijmaa' ya Maswahaba".
Hii ndio kauli ya Jamhuri: Maalik, ash-Shaafi'iy, Ahmad na wengineo.
Kwa hiyo, ukiwa umefika msikitini ukakuta Rakaa basi utakuwa umeipata Ijumaa, la, ikiwa umekuta watu wameshanyanyuka kutoka katika rukuu ya rakaa ya pili au umekuta wamekaa kwenye Tashahhud (Tahiyyaat) basi utakuwa umekosa Ijumaa lakini utajiunga nao na akitoa salaam Imaam basi utanyanyuka na kuswali Adhuhuri rakaa nne.
Na Allaah Anajua zaidi