Mavazi Ya Imaam Na Viungo Katika Kusujudu

 

SWALI:

Asallam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatu;

suala langu lipo katika swala tunazoswali katika misikiti yetu ya hapa Zanzibar  na Tanzania kwa jumla, katika kusali kwetu tunaona maimamu wetu wanaotusalisha wanakuwa na matatizo ya nguo na nguzo katika masuala ya nguo tunakuta kama suruali anayovaa tunakuta inavuka zaidi ya fundo za miguu na katika suala la nguzo tunakuta kwenye sijida kwa namna tulivyofundishwa kuwa kuna sijida saba katika kusujudu sasa tunakuta mbili kati ya hizo hawazikamilishi yaani vidole vya miguu  utakuta vinasimama na havisujudu kama ni kosa kwa faida ya waislamu tujuulishe  tunatakiwa sisi tulio nyuma yaani maamuma tufanye nini tunaomba elimu ya hayo.

Asalam Alaikum.

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran ndugu yetu kwa swali lako hilo. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atutulie tawfiki mambo yetu na Atutengenezee Ibadah zetu zote.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuhimiza tuwe ni wenye kupeana nasaha na hilo ndilo agizo la Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Anatupasha habari ya Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) pale aliposema: Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninakunasihini; na ninayajua kwa Allaah msiyoyajua nyinyi (7: 62).

Na kuhusu Nabii Huud (‘Alayhis Salaam): Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu” (7: 68).

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anausia yafuatayo: Imepokewa kwa Abu Ruqayyah Tamiym ibn Aws ad-Daariy (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dini ni nasiha”. Tukasema: “Kwa nani?” Akasema: “Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, kwa viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida” (Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy).

Imepokewa na Jariyr ibn ‘Abdillah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa amesema: Nilimbai Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kusimamisha Swalah, kutoa Zakah, na kumpatia nasiha kila Muislamu (Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy).

 Je, nasiha maana yake ni nini? Hili ni neno lenye kukusanya mambo mengi. Maana yake ni kumtakia mtu kila la kheri, kwa kuwa na ikhlasi katika rai yako kwake. Hii ni nguzo ya Dini. Nasiha ina masharti yake na ni tofauti na fedheha ambapo kwenye nasiha huwa unamtakia mtu kheri kwa kumpatia kwa siri, kwa njia nzuri na sio kumkashifu mbele ya wengineo. Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akatueleza: “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora” (16: 125).  

Hivyo katika ‘Ibadah yoyote inatakiwa ya kwamba unapomuona Imamu au Muislamu mwenzio ana makosa Fulani inabidi ukae naye kitako na kumueleza ili ajirekebishe. Sasa ikiwa ni kuhusu mavazi ya Imamu hakuna vazi maalumu ambalo limewekwa ili livaliwe na Imamu anaposwalisha, bora liwe lina yale masharti kwa vazi kuwa ni la Kiislamu. Ikiwa atavaa suruali, kikoi au Panjabi likiwa halitaonyesha mwili, halitambana, halitafanana na vazi la kike wala la makafiri na litafunika ‘awrah (uchi) wake basi itakuwa ni sawa tu. Japokuwa katika maeneno yetu ya Afrika Mashariki upo msingi wa sheria ambao unatumika wa ‘Urf (ada na desturi) za huku kwetu ni kuwa Imamu ni lazima avae kanzu. Hilo ni kuelewana na kamati ya Msikiti ambayo itamuambia Imamu atekeleze hilo au muzungumze naye kwa njia nzuri kuhusu hilo.

Ama ikiwa Imamu nguo yake imevuka fundo mbili za miguu, Swalah yenu wala yake haina tatizo ila yeye Imamu Swalah yake itapungua daraja na atakuwa ni mwenye kupata dhambi kwa kuvaa hivyo kwa sababu kunapingana na mafundisho sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ifuatayo: Imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Mwenye kuburuza izari (kikoi) chake kwa kiburi katika Swalah, Allaah hana haja na halali wala haramu yake”. Na Isnadi yake ni Sahihi (Abu Daawuud, kwa Isnadi iliyo sahihi).

Hadiyth nyengine ambayo inakataza kuburuza nguo katika Swalah na kutokubaliwa Swalah yake ni hii ifuatayo: Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) ya kwamba: Alipokuwa mtu mmoja anaswali na huku kikoi chake kinaburuza, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Nenda ukashike wudhuu”. Yule mtu alikwenda akatawadha, kisha akarudi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Nenda ukatawadhe”. Mtu mmoja aliyekuwepo akasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Kuna nini, kwani umemuamrisha akatawadhe kisha umenyamaza?” Akasema: “Hakika yeye alikuwa anaswali na kikoi chake kinaburuza. Na kwa hakika Allaah haikubali Swalah ya mtu anayeburuza nguo yake” (Abu Daawuud kwa Isnadi Sahihi kulingana na sharti ya Muslim.

Na inakuwa ni haramu ikiwa mtu atavaa vazi lenye kuburuza kwenye Swalah kwa kiburi. Na madhambi ya kuvaa kwa fakhari na kiburi ni makubwa zaidi kuliko yule avaaye bila kiburi. Hadiyth zinazothibitisha makatazo ya kuvaa ‘izaar’ (shuka au kikoi) na pia inaingia suruali, kanzu, na mavazi yoyote mengine, ziko nyingi na hapa tunafupisha kwa kuiweka moja tu.

Na kutoka kwa ‘Abdullah bin ‘Amru kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Mwenyeezi Mungu Haitazami Swalah ya mtu mwenye kuburuza kikoi chake kwa kiburi” (Ibn Khuzaymah)

Hivyo, hili ni suala ambalo munaweza kuzungumza na Imamu kuwa si jambo zuri mtu kujizoeza nalo kwani ikiwa unaswali na nguo kama hizo itakuwa ndizo unazovaa nje ya Msikiti na zipo Hadiyth nyingi zenye kukataza. Juu ya yote Swalah yenu inakubaliwa.

Sehemu ya pili ya swali lako:

Hakika ni kuwa hakuna sijda saba kama ulivyosema bali ni kuwa anaposujudu mwenye kuswali ni lazima viungo saba viwe ni vyenye kugusa ardhi kama alivyofundisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), viungo hivyo ni: ni paji la uso na pua, vitanga vya mikono miwili, magoti na matumbo ya vidole vya miguu yashike ardhi na vidole vielekee Qiblah. Mara nyingi watu huwa wanakosea kwa kuvisimamisha vidole vyao vya miguu jambo ambalo si sahihi.

Ambalo linatakiwa kwako kufanya ni kumkumbusha Imamu kuhusu jambo hilo. Inawezekana kuwa labda hawezi kufanya hilo kwa sababu ya ugonjwa au sababu nyengine inayokubalika kisheria. Ikiwa ana sababu basi ataingia katika wito wa Allaah Aliyetukuka: “Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito” (2: 185). Na pia, “Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibraahim” (22: 78).

Jaribuni kubadilisha hayo kwa mazungumzo na Imamu na hata ikiwa ni maamuma wenzenu ambao wana hayo makosa. Tunawatakieni kila la kheri katika kubadilisha jamii na kubadilisha yasiyo sawa.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share