Kuhudhuria Shughuli Za Mazishi Za Wasio Waislamu Inafaa?
Kuhudhuria Shughuli Za Mazishi Za Wasio Waislamu Inafaa?
Swali:
Assalaamu alaikum warah matullahi wa barakaatuh.
Shukurani kwa juhudi mnayoifanya kutuelimisha kuhusu dini yetu. Allaah awalipe wema na awahifadhi. Swali langu ni hili: Je sheria ya dini yetu ya uislamu inaturuhusu kuweza kuhudhuria shughuli za kuzika asiyekuwa muislamu? Wengine wanasema eti unaweza kuhudhuria shughuli nyingine lakini usiende tu na jeneza makaburini, wengine wasema unaeza kwenda hata makaburini. Naomba muniweke wazi In shaa Allaah. Asanteni.
Jibu
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Uislamu hautaki kabisa kuvunja na kuharibu mahusiano na jamaa hata wakiwa si Waislamu. Uislamu umeweka umuhimu mkubwa kuwa na uhusiano bora na wazazi na jamaa. Na kwa hiyo, ukamuamrisha Muislamu awafanyie wema wazazi na jamaa hata wakiwa si Waislamu. Hivyo, Muislamu anaruhusiwa kuhudhuria mazishi ya wazazi na jamaa wasio Waislamu ila haruhusiwi kushiriki katika ‘amali za kidini au zinazo kwenda kinyume na Uislamu.
Uislamu unataka wazazi waheshimiwe kwa kiasi kikubwa. Hivyo, Allaah Aliyetukuka Amesema:
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾
Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima. [Al-Israa: 23].
Pia Amesema Aliyetukuka:
وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾
Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani, na fuata njia ya anayerudi kutubia Kwangu. Kisha Kwangu ndio marejeo yenu, na Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. [Luqmaan : 15].
Jukumu la ukarimu na mahusiano mema huhimizwa nyakati za furaha, shida na majanga, kubwa ikiwa ni kifo. Kifo ambacho kinawaleta jamaa pamoja wanapohuzunika kwa kuondokewa na mmoja wao. Mwanadamu anakuwa ni mwenye kuonyesha hisia zake kwa aliyekufa sawa akiwa ni jamaa au rafiki wa karibu. Kwa ajili ya hiyo, tunasoma katika Hadiyth iliyo sahihi kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizuru kaburi la mama yake na kulia na kuwafanya waliokuwa naye pia kulia, akasema:
"Nilimuomba Rabb wangu Mlezi Aniruhusu kumuombea msamaha mama yangu, lakini Alikataa kunipatia idhini kwa hilo. Kisha nikamuomba ruhusa kulizuru kaburi lake, naye Akanipatia ruhusa. Hivyo, zuruni makaburi kwani yatamkumbusha mmoja wenu kifo" [Muslim, Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah].
Ziada ya hayo, Uislamu unaita na kusisitiza katika kumheshimu mwanaadamu yeyote, ikiwa ni Muumini au asiyekuwa Muislamu, katika uhai wao na baada ya kuaga dunia.
[Imenukuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim] katika Hadiyth kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama pindi jeneza ya Myahudi ilipokuwa ikipita mbele yake. Mtu mmoja akamuarifu kuwa aliyekufa ni Myahudi tu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Je, hiyo si nafsi?"
Hivyo, nafsi ya baba, mama au jamaa wa karibu anahitaji kuheshimiwa. Kwa hiyo, Muislamu anaweza kuhudhuria mazishi ya wazazi ambao si Waislamu, au jamaa zake, maadamu hatoshiriki katika maombi, ‘amali za kidini na nashati nyingine za kidini. Pia anaweza kushiriki katika mazishi, na katika yote hayo ni lazima nia yake iwe ni kutekeleza wema kwa wazazi na kuweka mahusiano mazuri na jamaa na marafiki kwa msiba uliowakumba na kudumisha mahusiano mema. Lile ambalo linakatazwa ni kuwaombea wasiokuwa Waislamu hata kama ni wazazi.
Kadhalika imepokewa kuwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema, "Alipofariki Abu Twaalib, nilimjia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na nikamwambia, "’Ami yako, mzee aliyepotoka, amefariki." Akasema, "Nenda kamzike." [Abu Daawuud, An-Nasaaiy].
Na Allaah Anajua zaidi