Vipi Kutia Niyah Ya Ibaada?

 

 

 

SWALI:

 tunatakiwa tufunge sunna mbali mbali kamav vile sunna za jumatatu na alkhamis hususa kwale mabarubaru ili kupunguza matamanio ya nafsi pamoja na kumcha Allah.Je katika funga kama hizo za jumatatu na alkhamis tunatakiwa tunuie vipi? Naomba nia yake kwa matmshi ya kwiswahili

 

 


 

JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Niya ni muhimi katika kitendo chochote cha ibada na hakuna ikhtilaaf baina ya Maulamaa kuhusu hili. Na hii ni rai ya Maalik, Ahmad ibn Hanbal na Abu Daawuud kwa kutoa dalili ya Aayah:

((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ))  

((Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allaah kwa kumtakasia Dini)) [Al-Bayyinah: 5]

 

Kumaubudu Allaah سبحانه وتعالى Pekee kwa ikhlaas ni kitendo katika moyo, nacho ndio nia na amri katika Aayah hiyo inaonyesha kuwa ni fardhi.

Vile vile katika Sunnah Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema katika Haidiyth iliyopokelewa na 'Umar ibnul-Khatwaab رضي الله عنه

((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى))  البخاري  و مسلم

 

((Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) nia na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia))

[Al-Bukhaariy na Muslim]

Lakini inapasa kutambua kwamba niya ya ibada yoyote kama ni kujitia tohara, wudhuu, tayammum, Swalah, Swawm, kutoa Zakaah na kadhalika haitamkwi kwa sauti bali huwekwa moyoni. Niya inaunganika na elimu. Ikiwa mtu anajua anachotaka kufanya basi tayari niya yake imeshaingia moyoni.

Kuitamka kwa sauti itakuwa sio kufuata mwendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  au Maswahaba zake, kwa hiyo kuitamka kwa sauti itakuwa ni Bid'ah (uzushi).  Na kama ingelikuwa ni jambo lililokuwepo katika sheria basi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  angeliwafundisha Maswahaba zake na mafunzo hayo yangelitufikia sisi pia kwani Niya ni jambo ambalo lina uhusiano na kila ibada ya Ummah huu; mchana na usiku kwa hiyo ingelikuwa ni muhimu kutaja kwa sauti asingeliacha kutoa mafunzo.  

Kutamka Niya kwa sauti ni jambo lisokuwa na mantiki, kwani  mtu anapotaka kufanya jambo la kawaida huwa hasemi kwa sauti kuwa "mimi nataka kufanya jambo fulani", bali hutia niya yake moyoni na kujitayarisha kwa kila njia na wakati maalum hadi atimize jambo lake. Kwa mfano mtu anapotaka kutoka nyumbani kwake na tuseme yuko peke yake, basi hatosema kwa sauti kuwa 'Mimi natoka kwenda kwa fulani" Au "natoka kwenda mahali fulani" Na Allaah سبحانه وتعالى  ni Mwenye mifano bora.

Tutatumbue kuwa jambo hili limejulikana sana kutokana na mafunzo yasiyo sahihi tuliyoyapata kutoka kwa wazazi wetu au waalimu kwamba Niya hutajwa kwa sauti. Kama mfano tunapotaka kuswali mtu hutia Niya kwa sauti kwa kusema: "Nawaytu Fardha Swalaat Adh-Dhuhr Arba'a Rakaat LiLLaahi Ta'ala……" na kadhalika. Na kwa wengi wetu tunapoambiwa kinyume na hivyo hushangaa na hata kwa wengine huwa ni vigumu kukubali mafunzo sahihi. Kuna baadhi ya sehemu hadi sasa, wanaona wasipokwenda msikitini mwezi wa Ramadhaan kunuizwa na Imaam (Nawaytu Swawma Ghadin...) basi wanaamini kuwa kesho hawana Swawm kwa kukosa kunuizwa siku hiyo!! Huo ni ujahili wa dini, na ni jambo ambalo linatakiwa liachwe lisizidi kupoteza wengi maskini wasio na elimu ya dini yao.

Basi inampasa Muislamu aliyezoea kuweka niya kwa sauti ajirekebishe na kuweka niya moyoni katika ibada zake zote, kutokana na mafunzo haya sahihi tunayoyaeleza pamoja na dalili zake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share