Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja
Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja
SWALI:
Assalaam alaykum.
Naomba kuuliza:
1. Ikiwa hairuhusiwi kumfanyia khitima aliyefariki, je, inaruhusiwa kuchinja mnyama au kutoa sadaka kwa ajili ya kumuombea dua aliyefariki? Yaani nikakusudia mathalani kufanya sadaka ya chakula/ kichinjo kwa makusudio kuwa thawabu za sadaka hiyo iwe ni dua kwa aliyefariki.
2. Ikiwa sadaka hiyo inruhusiwa, je ni sahihi kuwakusanya waislamu kwa ajili ya dua na sadaka hiyo?
Naomba mjibu In shaa Allaah niweze kuelimika.
Wabillah Tawfiq.
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kwa ujumla, ikiwa mtu anataka kumfanyia mzazi wake aliyekwishafariki vitendo ambavyo vitamfikia thawabu zake, ni lazima atende vitendo ambavyo vimepatikana dalili zake katika Sunnah. Kufanya kinyume na hivyo ni kupoteza mtu muda wake, mali yake kwa jambo ambalo halina thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري
"Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa". [Al-Bukhaariy]
Shaykh Al-Fawzaan alipoulizwa kuhusu vitendo gani vyema ambavyo aliye hai anaweza kumfanyia maiti alijibu:
"Maiti anaweza kunufaika kwa vitendo vya walio hai ambavyo vinatokana na dalili sahihi inayodhihirisha kuruhusiwa kama; kumuombea du'aa, kumuombea maghfira, kumfanyia sadaka, kumfanyia Hajj na 'Umrah, kumlipia madeni yake na kumtekelezea mirathi yake ya Kiislam. Vitendo vyote hivyo vimethibiti kisheria. Na baadhi ya Maulamaa wameunganisha na hayo pia vitendo vyote vengine vya ibada ambavyo Muislamu hutenda kwa ajili ya Muislamu mwengine ambaye yu hai au amefariki. Lakini, iliyo sahihi ni kujiweka katika mipaka ya yale yaliyoruhusiwa yakiwa na dalili sahihi, kwani hivyo itakuwa ni kutokana na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:
وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾
Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi. [An-Najm: 39]
[Shaykh ibn Fawzaan - Al-Muntwaqaa min Fataawa Shaykh ibn Fawzaan – Mjalada 2, Uk. 161, Fatwa Namba 139]
Mas-alah Ya Kuchinja
Kwa vile haikupatikana dalili kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kwa ajili ya maiti yeyote kwa nia ya kumfikia thawabu, hivyo kitendo hicho hakipasi kumtendea maiti.
Mas-alah Ya Kuomba Du'aa Pamoja
Aghlabu ya watu hukusanyika katika shughuli kama hizo na nyinginezo na huomba du'aa kwa sauti pamoja, jambo ambalo halikupatikana dalili katika mafunzo ya dini yetu.
Muislamu anaweza kumuombea du'aa mzazi wake akiwa pekee na hii ni dalili kutoka katika Hadiyth ifuatayo:
((إذا مات ابن آدم انقطع عمله إلا من ثلاث: صدقة جارية، أو علم ينتفع به، أو ولد صالح يدعو له)) رواه النسائي و الترمذي
"Anapokufa binaadamu hukatika vitendo vyake (vyema) isipokuwa (vitendo) vitatu; sadaka inayoendelea, elimu inayoendelea kunufaisha au mtoto mwema anayemuombea." [An-Nasaaiy na At-Trimidhiy]
Hii kwa maana amuombee yeye mwenyewe peke yake na sio kujumuisha watu kumuombea kwani Hadiyth iko wazi kuwa ni 'mtoto mwema anayemuombea'.
Kuhusu Khitmah
Nalo ni jambo lisilokuwa na dalili katika mafunzo ya dini yetu, kwani hakuwahi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumsomea khitma mtu yeyote katika maisha yake. Watoto wake na Swahaba walifariki katika uhai wake na hakuna hata masimulizi yoyote yale kuwa alikusanya watu kuwasomea Khitma; alifiwa na wanawe, ‘ami zake, baba, mama na hata marafiki zake Swahaba, lakini hakuwahi kuwafanyia Khitmah. Pia alipofariki yeye, wapenzi wake kama kina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na hata binamu yake ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum), hawakuwahi kumfanyia jambo kama hilo au hata lenye kufanana na hilo! Nao walikuwa wanampenda sana na pia kuwa na uchungu naye kuliko sisi. Hivyo kutenda ibada hiyo ni kuzusha katika dini jambo ambalo amelikemea sana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani alikuwa akitanguliza maonyo katika khutba zake:
(( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار)) أخرجه مسلم في صحيحه
"Maneno bora ni Kitabu cha Allaah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni motoni)". [Muslim katika swahiyh yake
Bonyeza hapa usome kuhusu mas-alah ya Khitmah na hukmu yake:
KHITMAH: Kutokufaa Na Madhara Yake
Na Allaah Anajua zaidi