Zingatio: Unapopata Mitihani Subiri

 

Zingatio: Unapopata Mtihani Subiri

 

Naaswir Haamid

 

 Alhidaaya.com

 

 

Muombe Rabb wako Akujaalie katika wale ambao wanapopewa mtihani wanasubiri, kwani wengi wanaporomokea kwenye maasi kwa sababu ya kushindwa kusubiri kwa mitihani waliyopewa.

 

Basi kwa hakika, kila Muislamu ni mwenye kukumbwa na mtihani. Bali sio hao tu, hata wanyama na mimea wanakumbana na matatizo. Isipokuwa wanaadamu wanalipwa kutokana na subira yao mbele ya Hisabu. Tumuombe sana Rabb wetu kuwa miongoni mwa wenye kusubiri.

 

Mitihani yaweza kuja katika sura tofauti. Yawezekana ukazushiwa mambo kutoka kwa walimwengu ambayo hujayafanya. Pia mtihani upo katika mwili, huenda ukakumbwa na maradhi ikawa maji ya kunywa unapenyezewa kwa mirija, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Asitufikishe huko. Halikadhalika, mtihani mwengine ambao wengi wao unawakumba lakini hawauelewi kwamba ndio mkubwa ni mali. Nayo mali ipo kwa watoto, wake na fedha. Vyote hivyo ni fitnah na kila Muislamu ana wajibu wa kuvitumia namna Alivyoelekeza Rabb Mlezi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٢٨﴾

Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni jaribio, na kwamba kwa Allaah uko ujira adhimu.  [Anfaal: 28]

 

Subira ya mtihani wa mali sio tu wakati wa kuihodhi, bali hata pale inapopungua, kuondoka kabisa ama kutoipata basi Muislamu anastahiki kusubiri. Mola wetu Mlezi Hayupo pamoja na wanafiki, mafisadi, makafiri wala mabadhirifu. Bali Allaah Yupo pamoja na wenye kusubiri na kwa hakika hilo ndio kundi lililofuzu:

إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿١١١﴾

Hakika Mimi Nimewalipa leo (Jannah) kwa yale waliyokuwa wakisubiri; hakika wao ndio wenye kufuzu. [Al-Muuminuwn: 111]

 

Kufariki kwa mtu wa karibu pia ni mtihani, nao waweza kumfanya Muislamu kuingia katika shirki kwa kuomboleza hadi kwenda kwa waganga kupiga ramli. Kwa hapa omba uwe miongoni mwa wale ambao wanapofariki vipenzi vyao wanasema:

 

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾

Wale ambao unapowafika msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. [Al-Baqarah: 156]

 

Kwa hakika hakuna mtihani ambao unatukuta, isipokuwa umeandikwa katika Lawhul-Mahfuudh. Hivyo ni wajibu wetu kusubiri.

 

Share