Tabia Gani Zilizotajwa Katika Hadiyth Katika Kutafuta Mume? Na Fitnah Gani Zilokusudiwa?

SWALI:

 

Mtume s.a.w amesema idha atakum man tardhaunahu dinahu wa khulukhahu fazawwijuhu! Tabia nikamagani na dini alokusudia ni ya kivipi? Mwisho wahadith sikuimaliza lakin yasema ama itawafika fitna ni fitna ya kivipi???


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Hadiyth uliyoitaja ambayo imenukuliwa na Imaam at-Tirmidhiy na Ibn Maajah.

Maana ya Hadiyth ni, “Atakapokujieni mnayemridhia Dini na maadili yake, muozesheni kwani msipofanya hivyo kutakuwa na fitnah katika ardhi na ufisadi mkubwa”.

 

Dini ni kuwa mwanaume aliyekuja kuleta posa awe ameshika Uislamu inavyotakiwa. Awe ni mtu wa Swalah tano, funga, mtoaji wa Zakaah ikiwa ana uwezo na ‘Ibaadah zote anazohitajika kufanya Muislamu. Pia awe ameepukana na ‘amali za madhambi ambazo zinampeleka mahali pabaya. Ama tabia au maadili ni ujumla wa tabia za Kiislamu kama kuwa mkweli, mwaminifu, uadilifu, upole, ulaini, mvumilivu, mtekelezaji ahadi, mwenye kushauri, mwenye msimamo na kadhalika.

 

Mwisho wa Hadiyth Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatutahadharisha kuwa lau hatutafanya hivyo. Hivyo ni vipi, yaani ikiwa hatukuwa ni wenye kuwaozesha binti zetu kwa waume wenye Dini na maadili basi kutakuwa na fitnah.

 

Fitnah ina maana ya mtihani. Mtihani huu kwa wazazi, binti na waume ni kuwa watoto watawaasi wazazi wao na huenda wakatoroshana, wakazini na kuzaa watoto ambao si wa halali. Kufanyika hivyo kutaleta uharibifu kwani mapenzi hayo hayatadumu. Kutodumu kwa hayo mapenzi kutaleta watoto ambao hawana baba wakilelewa na mama zao tu, hivyo kuleta mkurupuko wa wizi, uasherati zaidi, utovu wa nidhamu ambao utavuruga amani katika dunia na kuleta uharibifu usio kifani.

 

Hali kadhalika pia inaweza kuwa na maana ya kuja kuozeshwa kwa waume wasio na Diyn na wenye maadili mabaya kwa sababu tu ya pesa walizonazo, au umaarufu au ukoo mkubwa wenye jina, au wa kabila lake kwa sababu wao ni wabaguzi hawataki makabila mengine n.k. Na mwisho wake wakaishia kwenye maasi, mume mlevi. Muuza madawa ya kulevya, mvuta bangi, mla mirungi, mzinzi, asiyefanya ‘Ibaadah kama kuswali n.k.

 

Kwa hali zote na mifano yote, hiyo ndiyo fitnah iliyokusudiwa kwenye Hadiyth hiyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share