Vipi Awazoeshe Watoto Kuswali Kila Kipindi?
SWALI:
ASSALAM ALAYKUM WARAHMATULLAH TA'ALA WABARAKATU
NAULIZA JINSI GANI WATOTO WANGU WENYE UMRI WA MIAKA KUMI MBILI NIWASHURUTISHE KUHUSU KUSWALI KWA KILA KIPINDI. KWANI MUDA WA KUSWALI WANAO ILA HUWENDA WANASAHAU AU WANA MCHEZO MWINGI. MIMI NI MAMA NINAETOKA ASUBUHI NA KURUDI JIONI SAA 12 NIMEANZA KUWASHIRIKISHA KUSWALI TANGU WANA UMRI WA MIAKA SITA MPAKA LEO LAKINI BADO HAWAJAIKUBALI SALA. NAOMBENI PIA USHAURI - NAOMBA JIBU KUPITIA EMAIL ADDRESS YANGU. NA NINAOMBA RADHI KAMA NITAKUWA NIMEKOSEA.
WA ALAYKUM SALAAM.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu njia ya kuwazoesha watoto wako juu ya kuswali.
Swalah ni muhimu sana kwa kiasi ambacho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Wafundisheni watoto Swalah wakiwa na miaka saba na wapigeni wakitoswali wakiwa na miaka kumi” (Abu Daawuud).
Na AlhamduliLlaahi, inaonyesha ulitekeleza hilo kwa kuwazoesha kuswali watoto wako kuanzia walipokuwa na miaka sita. Hata hivyo, inaonyesha kuwa hukuwatia adhabu wakiwa na miaka kumi. Jambo ambalo ni muhimu kwa watoto kuweza kutekeleza ‘amali muhimu kama Swalah kwa kupitia mazoezi yafuatayo:
1. Wapate kielelezo chema kutoka kwa wazazi (baba na mama) kwa kuonekana wazazi hao nao wanaswali. Na hasa mama ndiye Madrasah ya kwanza ya mtoto. Na ikiwa unakwenda Msikitini kwa ajili ya Swalah au baba yao anakwenda wawe wanachukuliwa ili kuwazoeza kimatendo Swalah.
2. Wapelekwe katika Madrasah ili waweze kufundishwa Uislamu, Ibaadah, maadili yake na mengineyo.
3. Kuwahimiza kusoma Qur-aan, kujua maana yake na kufanya juhudi katika kufuata maagizo yaliyo ndani.
4. Wahimizwe kuwa na marafiki wema ili waweze kuwahimiza katika mambo ya Kidini.
5. Kuwanunulia vitabu vya Dini na kuwasisitiza kuvisoma na kufuata yaliyo ndani yake.
6. Kuwa na kanda, DVD, VCD na ala nyinginezo za kuweza kuwafundisha watoto yake mambo ya Kidini.
Kwa maelezo yako, inaelekea baba yao hayupo, na kurudi kwako jioni kutokea asubuhi ni tatizo kubwa sana kuweza wewe kufanikisha hizo taratibu tulizokutajia hapo juu, kwani vipindi vingi vya Swalah vitakuwa vinawapita kwa kuwa hakuna wa kuwasimamia!
La kufanya kwa hali hiyo, unatakiwa unaporudi uwe nao na ikiwa mnaswali nyumbani uwe unaswali nao na kuwasikiliza kwa yale wanayosoma. Na InshaAllaah kwa kufuata maelekezo hayo tunatarajia kuwa watabadilika.
Na Allaah Anajua zaidi