Jiepushe Na Moto Wa Jahannam Pamoja Na Familia Yako
Jiepushe Na Moto Wa Jahannam Pamoja Na Familia Yako
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾
Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]
'Aliy bin Abi Talhah amepokea kutoka Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhaumaa) kwamba amesema kuhusu Aayah hii: "Mtiini Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa na jiepusheni na kumuasi Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa na amrisheni familia zenu kumkumbuka Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa ili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awaokoe na moto wa Jahannam". [At-Twabariy 23: 491]
Kutokana na Aayah hiyo, ni wajib wa Muislamu kufundisha familia yake; ikiwa ni mke au mume, watoto, ndugu, wazazi na kadhalika, mambo yaliyo fardhi kufanya na kuwakataza yaliyoharamishwa.
Hadiyth ifuatayo inathibitisha maana ya Aayah hiyo:
عبد الملك بن الربيع بن سَبْرَة، عن أبيه، عن جده قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((مروا الصبي بالصلاة إذا بلغ سبع سنين، فإذا بلغ عشر سنين فاضربوه عليها)) رواه الإمام أحمد، وأبو داود، وقال الترمذي: هذا حديث حسن.
Imetoka kwa 'Abdul-Malik bin Ar-Rabiy' bin Sabrah kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwamba amesema Nabiy (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi Sallam): "Amrisheni watoto kuswali watakapotimia miaka saba, na wapigeni [ikiwa hawatoswali] watakapotimia miaka kumi". [Imaam Ahmad, Abu Daawuud, na kasema At-Tirmidhy Hadiyth Hasan]
Na kuwaamrisha watu wako, mfano watoto kuswali ni kudhihirisha mapenzi yako kwao kwani hutopenda watoto wako waingie motoni, hivyo unapowaonea huruma asubuhi wasiamke kuswali Swalah ya Alfajiri, sio maana kuwa unawependa bali ni kinyume chake, kwa vile unawasababisha wawe miongoni mwa watu wa motoni. Watu wa (Jannah) Peponi watakapowaona watu wa motoni watawauliza sababu ya kuingia kwao huko motoni na sababu mojawapo watasema kuwa ni kutokuswali:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ﴿٣٨﴾إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ﴿٣٩﴾فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ﴿٤٠﴾عَنِ الْمُجْرِمِينَ﴿٤١﴾مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ﴿٤٢﴾قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ﴿٤٣﴾
Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma. Isipokuwa watu wa kuliani. Katika Jannaat wanaulizana. Kuhusu wahalifu. (Watawauliza): Nini kilichokuingizeni katika motoni? Watasema: Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali. [Al-Mudathhir: 38-43]
Hakika kuamrisha familia zetu kuswali ni jambo gumu sana na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipoamrisha jambo hili Alitutaka tuendelee nalo kwani linahitaji kuwa na subira nalo, kama Anavyosema Allaah katika Aayah ifuatayo, ambayo 'Umar ibnul-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akiisoma huku akiamsha familia yake kuswali:
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ
Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo. [Twahaa: 132]
Aayah hiyo ya mwanzo inaelezea hali ya huo moto kuwa:
وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ
Kuni zake ni watu na mawe, [Al-Baqarah: 24]
Watu hao ni sisi wana wa Aadam, na mawe ni masanamu yaliyochongwa yaliyokuwa yakiabudiwa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ
Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Allaah ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu. [Al-Anbiyaa: 98]
Kisha Malaika wanaowaingiza hao watu motoni hawana huruma kabisa kwa watu waliomkufuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hukimbilia haraka kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwaingiza watu motoni bila ya kuchelewa hata upepesi wa macho. Malaika hao wanaitwa Az-Zabaaniya (walinzi wa moto wa Jahannam) kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa:)
سَنَدْعُ الزَّبَانِيَةَ ﴿١٨﴾
Nasi Tutawaita Az-Zabaaniyah (Malaika wa adhabu). [Al-'Alaq: 18]
Basi tujitahidi kutimiza Swalaah zetu kama zinavyopasa na kuamrisha familia zetu pia watimize Swalah ili tujiepushe sote na moto huo mkali wa Jahannam.
***********