Ndoa Ya Waliozini Kwa Mtazamo Wa Ahlus Sunnah Wal Jama'ah
Ndoa Ya Waliozini Kwa Mtazamo Wa Ahlus Sunnah Wal Jama’ah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
Tunachukuwa fursa hii kuweka wazi madhehebu ya Ahlus Sunnah katika maudhui ya kujuzu au kutokujuzu kuoana waliozini.
Sababu iliyopelekea kuandika makala hii ni baada ya kusingiziwa wanavyuoni wa Ahlus Sunnah kuwa wana msimamo sambamba na msimamo wa kiibadhi ambao ni kutojuzu ndoa ya waliozini.
Singizio hili limetolewa na mmoja wa waandishi wa kiibadhi wa makala mbali mbali, kwa kusema “Riwaayah tulizozinukuu humu zote zinatoka katika vitabu vya kisuni, kwa sababu wengine hudhani labda ni msimamo wa Ibadhi tu.”
Haya ni maneno yanayoashiria wazi kuwa Ahlus Sunnah nao huharamisha moja kwa moja kama wanavyoharamisha ibadhi kuoana wale waliofanya zinaa na hili linatokana na suala la muulizaji kama lilivyotangulia.
Na ifahamike kuwa lengo langu si kuelezea dalili za Ahlus Sunnah katika suala hili kwani makala itarefuka mno, na lengo khaswa ni kueleza uhakika wa suala hili katika madhehebu ya Ahlus Sunnah ambayo yanajumuisha madhehebu ya wanavyuoni wakuu wafuatao: Imam Abu Hanifa, Imam Malik, Imam Shafii, Imam Ahmad bin Hanbal na Imam Ibnu Hazm (Allaah awarehemu).
Pia nitaelezea nukuu za Swahaba mbalimbali ambao wamejuzisha ndoa hii kama Ahlus Sunnah ili kuweka wazi kuwa nukuu alizozinukuu mwandishi kutoka kwa Swahaba watatu sio msimamo wa Swahaba wote bali wengi wamejuzisha.
Nasi tutajitahidi kuelezea kile kinachozungumzwa na wenyewe katika vitabu vyao vya madhehebu ili kuondosha wasi wasi.
-
Wamekubaliana wanavyuoni wote wa Ahlus Sunnah kuwa ndoa ya wazinifu inajuzu kimsingi.
-
Kisha wakakhitilafiana juu ya shuruti za kusihi kwa ndoa hiyo, kuna wasioshurutiza jambo lolote kama yalivyo madhehebu ya Shafii, na wengine wameshurutiza papatikane toba ya wazinifu hao kama yalivyo madhehebu ya Imam Ahmad bin Hanbal na Imam Ibnu Hazm Adh-Dhwaahiry, na wengine wakashurutiza lazima mwanamke afanye Istibrai nayo ni badala ya eda kama yalivyo madhehebu ya Imam Malik na pia madhehebu na Hanbal.
Nukuu Za Ahlus Sunnah
1. Kukubaliana Kusihi Kwa Ndoa Ya Wazinifu
a) Amesema Ibn Abdul-Barr “Na wamekubaliana wanavyuoni wa fatwa katika miji (tofauti) ya kwamba si haramu kwa mzinifu kumuoa mzinifu mwenziwe…” Tazama Fat-hul Baariy ya Ibnu Hajar Al-‘Asaalani juzuu 9 uk. 157.
b) Amesema Imam Raazi Al-Jassaas “Na wana fiqhi wa miji mbali mbali wamekubaliana juu ya kujuzu kwa ndoa (ya wazinifu) na kwamba zinaa hailazimishi kumharamishia mume (kuoa) wala hailazimishi kutengana kwa waliokwisha oana.” Tazama Ahkamul-Qur-aan, Imam Jassaas juzuu 5 uk. 108.
Kutokana na nukuu hizi tunafahamu kuwa kimsingi ndoa inajuzu na zinaa si kizuwizi cha watu kuoana.
2. Ama Nukuu za kila dhehebu Na Masharti Waliyolazimisha Ni Kama Ifuatavyo:
Madhehebu ya Imam Abu Hanifa.
a) “Lau kama (mwanamme) atamuona mwanamke anazini akaja kumuoa inajuzu (ndoa hiyo) na Mume inajuzu kustarehe nae bila ya kufanya Istibraa huyo mwanamke … na haya ni wazi kuwa inajuzu kumuoa mzinifu mwanamke ..” Tazama Albahru Raik juzuu 3 uk 114. na maneno kama haya ya kujuzisha ndoa ya mzinifu utayapata katika vitabu vya madhehebu yao tazama Adurrul Mukhtar juzuu 3 uk 50, na sherehe ya Fathul Qadiir juzuu 3 uk 246.
b) Na angalia madhehebu yao yalivyo wazi katika nukuu hii “mlango, mwanamme anazini na mwanamke kisha anataka kumuoa. Amesema Abu Hanifa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuhusu mwanamme aliyezini na mwanamke kisha akataka kumuoa kwamba hiyo ndoa haina tatizo lolote..” Tazama Al-Hujja juzuu 3 uk 388.
Na Istibraa ni badala ya eda pamoja na kuwepo khilafu katika wakati wake, yaani haishurutizwi kukaa eda kwa mwanamke ili ijuzu kwa mwanamme kustarehe nae baada ya kumuoa,na hapa tunakuta kuwa madhehebu ya Imam Hanafi yanajuzisha ndoa hii bila ya kujali sharti hii kama walivyoshurutiza madhehebu mengine kama inavyofuata.
Madhehebu ya Imam Malik.
a) “Nimesema (mtunzi): Unaonaje mwanamme akizini na mwanamke itamfalia kumuoa? akasema.. (aliyeulizwa ni mmoja wa wanavyuoni wakubwa wa madhehebu ya Imam Malik) amesema Malik ndio inafaa kumuoa ila hatomuoa mpaka mwanamke afanye Istibraa (ajisafishe) kutokana na maji yake machafu ya uzazi.”
Tazama Mudawwana AlKubra juzuu 4 uk 249.
b) Pia amesema Imam Kurtubi nae ni katika wanavyuoni wakuu wa madhehebu ya Kimalik alipozungumzia sehemu ya aayah ya zinaa “ Na ikiwa itakusudiwa (maana ya La Yankih) ni ndoa (akdi) basi itakuwa maana yake ni kwamba aliyemuoa mzinifu ambaye kazini nae na akastarehe nae kabla ya kufanya istibraa (mwanamke huyo) atakuwa kama mzinifu (huyo mwanamme) isipokuwa hatopigwa mijeledi kutokana na kukhitilafiana kwa wanavyuoni juu ya suala hili ( la kujuzu ndoa na kustarehe nae kabla ya kufanya Istibraa ) . Ama akifunga nae ndoa na akawa hakustarehe nae hadi anapofanya Istibraa basi hiyo ndoa ni sahihi kwa Ijmaa (makubaliano) ya wanavyuoni.” Ahkamil Quraan (Qurtubi) juzuu 12 uk 170.
Madhehebu ya Imam Shafii
a) Amesema Imam Shafii kuhusu aayah ya Suwrah Nuwr inayozungumzia ndoa ya wazinifu “Wamekhitilafiana wanavyuoni wa tafsiri katika aayah hii khitilafu iliyo wazi na ambayo tunayoiunga mkono na Allaah ndie mjuzi, ni ile aliyosema Tabii Imam Said bin Musayyib. Akasema Imam Shafii ametupa khabari Sufyan nae kutoka kwa Yahya bin Said nae kutoka kwa Said bin Musayyib amesema kuwa aayah hii imefutwa (mansuukh) na imefutwa na aayah isemayo:
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ
“Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allaah Atawatajirisha katika fadhila Zake. Na Allaah Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote …” [An-Nuwr: 32]
Basi huyo (mzinifu wa kike) ni katika wajane wa kiislamu, basi hapa ni kama alivyosema Ibnu Musayyib, na zipo dalili zinazounga mkono haya katika kitabu na sunna…”
Tazama kitabu Al Ummu juzuu 5, uk. 148.
Kutokana na maneno haya hatuoni uharamu wowote wala sharti yoyote bali katika vitabu vyote vya madhehebu ya Kishafii , illa tunakuta uhalali wa wazi kama alivyosema mwenyewe kuwa mzinifu anaingia katika jumla ya wajane hivyo hakuna uharamu, na kama tujuavyo ikiwa aayah imefutwa hukumu yake hakuna kufanyiwa kazi tena, haya ni kwa wenye kuthibitisha kufutwa.
Madhehebu ya Imam Ahmad bin Hanhal (Rahimahu Allaah)
Madhehebu ya Imam Hanbal nao wanajuzisha ndoa ya wazinifu kwa masharti mawili nayo ni kutubia waliozini na kumalizika eda yake mwanamke, na tuangalie nukuu zao.
a) “Na ni haramu kwa mzinifu mwanamke kuolewa na mzinifu mwanamme (aliyezini na mwengine) hadi atubie huyo mwanamke na amalize eda yake.” tazama Rawdhul Murabbai juzuu 3 uk 83.
b) “ Na wanavyuoni wamekhitilafiana kuhusu kujuzu kumuoa mwanamke mzinifu kabla ya kutubia kwake katika kauli mbili mashuhuri , lakini Quraan na Hadiyth na mazingatio yanajuulisha kuwa ndoa hiyo haijuzu (kabla ya kutubia).” tazama Majmuu Fatawa Ibnu Taymiya juzuu 32 uk 145 ,na katangulia maneno mfano wa haya uk 141.
Madhehebu ya Imam Ibnu Hazmi Adhw-Dhwaahiry (Rahimahu Allaah)
Nae ni katika wanaojuzisha ndoa ya mzinifu kwa sharti atubie huyo mzinifu.
a) “Mas ala: Na haijuzu kwa mzinifu wa kike kuolewa na mzinifu wa kiume au asiyemzinifu, na akishatubia itamhalalikia kuolewa na asiyekuwa mzinifu ,na haijuzu kwa mzinifu wa kiume muislamu kumuoa mzinifu wa kike au asiyezini mpaka atubie (huyo mwanamme) na akisha tubia itamhalalikia kumuoa muislamu wa kike asiyezini .” Tazama Muhalla juzuu 9 uk 474.
Kutokana na maneno hayo inajuulisha kuwa mzinifu wa kiume ataruhusiwa kumuoa mzinifu wa kike ikiwa wote wawili watatubia, na hili halina shaka kwa mwenye kufahamu maneno ya wanavyuoni.
Na kutubia ni jambo linalofahamika katika sharia yetu na namna ya kutubia na shuruti zake zimeelezwa na wanavyuoni wetu katika vitabu vya na hapa si sehemu yake.
Huu ndio msimamo wa wanavyuoni wa Ahlus Sunnah, na sijuwi wanavyuoni gani huwa wanajulikana kama ni Ahlus Sunnah kama sio hawa waliotangulia, nasi tumejitahidi kutoa nukuu za kila madhehebu kutoka katika vitabu vyao vinavyotegemewa ili kuondosha shaka.
Khulasa
Baada ya kuona nukuu hizo tunafahamu kuwa ndoa ya wazinifu inafaa kwa ujumla, isipokuwa kuna shuruti kwa baadhi ya madhehebu ya Ahlus Sunnah nazo ni sharti mbili kuu kwa baadhi yao, kutubia na kufanya Istibraa, na wengine ni kutubia tu na wengine hawakushurutiza lolote kama yalivyo madhehebu ya Imam Shafii.
3. Nukuu Kutoka Kwa Swahaba
Ama sehemu ya pili ya makala hii ni kuelezea nukuu za swahaba waliojuzisha ndoa hii kwani mwandishi alikuwa aelezee hizo nukuu za Ahlus Sunnah zinazoharamisha ndoa ya wazinifu, na hakutoa hata kauli moja ya madhehebu yoyote kama tulivyotanguliza ,ila kanukuu baadhi ya Riwaayah zilizopokelewa kutoka kwa swahaba watatu ambao wanasema ndoa hiyo haifai nao ni Imam Aliy, Bibi ‘Aishah na Bwana Abdallah bin Masu’ud (Radhwiya Allaah ‘anhum), na nukuu hizo zipo kweli katika vitabu vya Ahlus Sunnah lakini haimaanishi kuwepo kwa nukuu hizo ndio msimamo wa Ahlus Sunnah ulivyo , bali wamenukuu kwa kuelezea kuwa wapo katika swahaba wanaopinga suala hili na hii ndio amana ya elimu , na mwandishi kaziwacha nukuu kama hizi (ima kwa kusahau au kwa makusudi!) kutoka kwa swahaba wengine wakuu ambao wanajuzisha ndoa hii nao ni wengi kuliko hao wanaoharamisha, na tuangalie nukuu zenyewe.
Nukuu za Swahaba Wanaohalalisha Ndoa ya Wazinifu.
-
Amesema Imam Jassas“ Na wamekhitilafiana wanavyuoni wa salaf (waliotangulia) katika kuolewa mzinifu , na imepokewa kutoka kwa Abu Bakr na ‘Umar na Ibnu Abbas na Ibnu Masu’ud na Ibnu 'Umar na Mujahid na Suleyman bin Yasar na Said bin Jubeyr katika mataabiina wa mwisho ya kuwa mwenye kuzini na mwanamke au mwanamke kazini na mwanamme mwengine basi inajuzu kwake kumuoa mwanamke huyo.
- Na imepokewa kutoka kwa Imam Aliy na Bibi ‘Aishah na Bwana Albarra na moja katika Riwaayah mbili za Ibn Masu’ud kwamba hao (wakiooana) watakuwa ni wenye kuzini muda wanapokutana.” Tazama Ahkamul Qur-aan (Jassas) juzuu 5 uk 108.
-
Na nukuu nyengine amesema Ibnu Wahbi (katika wanavyuoni wa Kimalik) kuhusu ndoa ya mzinifu “ Na wamenipa khabari watu wa elimu kutoka kwa Muadh bin Jabal na Jabir bin Abdallah na Al Musayyib na Nafii na Abdallah bin Masu’ud na ‘Umar bin Abdul Aziz na Hassan bin Muhammad bin Aliy bin Abi Talib kwamba hao wamesema Hakuna tatizo kumuoa .”
Hawa ni Swahaba waliohalalisha ndoa hii nao ni Khalifa Abu Bakr, Khalifa ‘Umar, Ibnu Abbass, Ibnu ‘Umar, Muadh bin Jabal na Jabir bin Abdillah (Radhwiya Allaahu ‘anhum).
Na walioharamisha ni watatu tu Imam Aliy, Bibi ‘Aishah na Bwana Al Barra (Radhwiya Allaahu ‘anhum).
- Ama sahaba Ibnu Masu’ud kuna Riwaayah mbili kutoka kwake, moja inaharamisha kama alivyoelezea mwandishi na ya pili ya kuhalalisha ikiwa ametubia, ambayo baadhi ya wanavyuoni wamezijumuisha Riwaayah mbili hizi na kusema kuwa hakuna mapingano tuangalie maneno yafuatayo:
- “Riwaayah Ibnu Masu’ud kuwa watakuwa ni wazinifu , aliulizwa Salim bin Abdallah bin ‘Umar kuhusu mwanamme anazini na mwanamke kisha akamuoa, akasema Salim aliulizwa suala hili Ibnu Masu’ud akasema “ Nae (Allaah) ni mwenye kupokea toba kutoka kwa waja wake .” na amesema Abu Muhammad (mtunzi wa kitabu hiki) : kauli mbili hizi kutoka kwake (Ibnu Masu’ud) ni zenye kukubaliana kwani amehalalisha ndoa yao baada ya kutubia, imepokea kutoka kwa Katada kutoka kwa Jabir bin Abdallah amesema “ ikiwa watatubia na wakawa wema basi hakuna tatizo (kuoawana) …” Tazama Muhalla juzuu 9 uk 475.
Na kauli hii kwamba hadi atubie ndio kama ilivyo kauli ya madhehebu ya Imam Hanbal wala hakuna tofauti, hivyo tunafahamu kuwa Sahaba Ibnu Masu’ud atakuwa ni mwenye kujuzisha ndoa ya wazinifu.
- Bali imepokewa kutoka kwa Imam Aliy pia kuwa nae anajuzisha, amesema Imam Shawkani.
“Na amesimulia katika kitabu Albahr kutoka kwa Aliy , na Ibn Abbas na Ibn ‘Umar na Jabir na Said bin Musayyib na Urwah na Azzuhary na Itrah (ahli bayt)na Malik na Shafii na Rabiah na Abi Thawr ya kuwa haharamiki mwanamke aliyezini na mwanamme (kuolewa) kutokana na aayah inayosema:
ۚ وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ
“…. Na mmehalalishiwa wasiokuwa hao…” [An-Nisaa: 24]
na kwa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) “Haramu haiharamishi Halali”, amepokea [Ibnu Majah ]kutoka kwa [Ibnu Omar ]..” Tazama Naylul Awtar juzuu 6 uk 283.
Hivyo Imam Aliy nae atakuwa na kauli mbili ikiwa mapokezi haya nayo ni sahihi.
Hizi ni nukuu za swahaba na kila mmoja ana tukio lake na namna walivyofutu , na imepokewa kutoka kwa Shuuba Maula Ibnu Abbas (ameachwa huru na Ibnu Abbas) kwamba amemsikia mtu anamuuliza Ibnu Abbas akisema , nilikua namfatilia mwanamke nikafanya nae mambo aliyoharamisha Allaah (zinaa) kisha Allaah akaniruzuku kutubia kutokana na tendo hilo nikataka kumuoa wakasema watu, hakika mzinifu hamuoi isipokuwa mzinifu mwenziwe (wanakusudia aayah ya zina ya Suwrah Nuwr) akasema Ibnu Abbas hii maudhui sivyo inavyokusudia aayah hii nenda kamuowe na kama kuna dhambi juu ya hili basi nizipate mimi.! Tazama Mudawwana Alkubra juzuu 4 uk 249.
Tahadhari
Baada ya kuona nukuu hizi napenda kutoa tahadhari ambayo wanavyuoni huitoa mara kwa mara , nayo ni kwamba kujuzu kwa ndoa baada ya kuzini haimaanishi kuwa zinaa ni halali bali hakuna hata mwanachuoni mmoja aliyesema hivyo, na kila mmoja kaharamisha zina kwani ni katika mambo ambayo mtu akipinga anakuwa kafir , hivyo kwa wanaokusudia kufanya zina wajuwe kuwa uharamu wa zina upo pale pale na dhambi watapata na adhabu kutoka kwa Rabb wao zinawasubiri ,naam ikiwa atatubia basi Allaah ndie anayejuwa nani wa kumsamehe ama hapa duniani ukisikikana umetubia na kutimiza masharti tutakuhesabu kuwa umetubia lakini mbele ya Allaah hatuna uwezo wa kusema kuwa ushasamehewa hili ni lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hivyo watu wawe na tahadhari na suala la zinaa na wengi hulifanya jambo hili kuwa jepesi lakini mwisho wake ni mbaya kwani wenye kuzini laana ya Allaah huwa juu yao, Allaah atuepushe na zinaa.
Tanbih
Mwisho napenda kutoa tanbih kwa kila anaeandika kuhusu kadhia ya kiislamu khaswa, awe muangalifu na kuhakikisha kile anachokiandika na hili linanihusu hadi mimi kwani kumsemea mwanachuoni kuwa kasema kadhaa hali ya kuwa hakusema ni jambo linalokatazwa kisheria , na zaidi kwa msomi wa dini, pia ijulikane kuwa kila dhehebu huwa na dalili zao kwa lile wanalosema na kila mmoja kati yao ni mwenye kupata thawabu kutokana na Jitihada aliyochukuwa ,ijapokuwa mwenye kuangalia dalili zao huenda akaona upande fulani umekosea ,na hili lipo kwa wanavyuoni kwani hakuna asiye na makosa ila Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) , na hakuna kosa kwa mwenye kufata madhehebu fulani na kujilazimu kwayo khasa katika mambo ya Fikhi (furuu), na kila mmoja afate vile madhehebu yake yanavyosema bila ya kuona aibu, muhimu tu awe ana kitulizano kwa anachokifata , kwa msingi huu ibadhi na wafate fatwa za wanavyuoni wao na wawaache Ahlus Sunnah wawafate wanavyuoni wao bila ya kusingiziana kwani hili halileti sura nzuri .
Pamoja na haya hakuna pingamizi pia kupinga dalili wanazotumia madhehebu yoyote muhimu kupinga huko kuambatane na misingi ya kielimu sio kwa kufata matamanio ya nafsi bali iwe kwa kuchukuwa dalili za kila upande na kuzitia katika wizani wa elimu na kutolea hukumu ,na pia hukumu hiyo itabaki ni rai yako binafsi wala si lakima kwa mwenye madhehebu hayo aifate rai hiyo.
Mwisho
Yapo mengi ya kuyaelezea kuhusu maudhui hii, yakiwemo tafsiri za wanavyuoni mbali mbali kuhusu ayaah hii, na hadiyth tofauti zilizopokewa, na kauli mbali mbali za wanavyuoni juu ya suala hili , lakini kama nilivyotangulia kusema lengo la makala hii ni kuthibitisha kuwa madhehebu ya Ahlus Sunnah ni yenye kujuzisha , wala sikusudii kuelezea dalili za kujuzisha huko kwani nikifanya hivyo makala itazidi kuwa kubwa na kuwachosha wasomaji, pia sikuirudi dalili yake ya Qiyasi kwani haikuwa lengo langu hilo na pengine Allaah ataniruzuku wasaa wa kuelezea dalili za suala hili pekee. Hivyo na tuishie hapa baada ya kuona ukweli wa fatwa za Ahlus Sunnah na sio kama alivyodai mwandishi wa Kiibadhi kuwa Ahlus Sunnah wanaunga mkono Maibadhi katika suala hili na kuliwacha suala liwazi bila ya kuelezea shuruti au kauli hata moja ya Imam wa Ahlus Sunnah.
Na kabla hatujafunga makala hii na tujiulize ikiwa hawa wazinifu hawaruhusiwi kuoana, au hairuhusiwi kumuoa mzinifu, nani atakaewaowa hawa? Jee wabakie hadi kufariki kwako bila ya kuwa na waume? Na jee waendelee na zinaa zao? Au jee waolewe na wasiowahi kuzini kabisa? Hapa ndipo wanavyuoni wetu wakasema inajuzu kuwaoa kwani Uislaam haubomoi bali unajenga, na Uislaam umekuja kupinga zina ukahaba na kuleta ndoa ya kisheria.