Kupatikana Ugumu Baada Ya Mvulana Na Msichana Kupendana Na Sherehe Ya Harusi Imekaribia

 

SWALI:

 

Salaam,

 

Mvulana na msichana wamepandana kwa muda mrefu kwa njia inayotakikana.  imefika wakati wa kuoana (harusi kupangwa) mambo mengi yanatokea kama kwamba harusi isiendelee ama wasioane. katika kila jambo ambalo wameliona ni gumu kwao basi wanaomba uongozi kutoka kwa Allah (SWT) na awatatulie. Je hii ni ishara ya kwamba ni kheri ama kazi ya shetwani kuingilia? Je wanafaa kufanya nini zaidi?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mvulana na msichana kupendana. Hakika tumeona swali lako lakini sentensi ya kwanza imetushangaza kwa kusema mvulana na msichana walipendana kwa njia inayotakiwa. Sijui ni njia gani hiyo kwani hakuna kupendana katika Uislamu nje ya ndoa. Kupendana inalazimu kwa watu wawili kukutana, kutembea pamoja, kujuana na kadhalika. Yote hayo ni njia miongoni mwa njia za uzinzi ambao tumekatazwa kuikaribia na Qur-aan.

 

Wakati wote mmependana tu hata bila ya kupeleka posa hili ni jambo ambalo halikubaliki kisheri na inatakiwa sisi kama Waislamu tuwe waangalifu sana tusiwe tunaiga mila za wengine kwa kujua au kutojua.

 

Jambo kuwa gumu ni ishara ya kwamba ima hakuna kheri katika ndoa yenu au kuna kheri pamoja na mitihani mingi kwa sababu ya kiungia shetani kati yenu. Mara nyingi ndoa ambazo zinakuja kufanyika au kuandaliwa baada ya kwamba waliotaka kuoana wamekutana kwa muda mrefu huwa zina matatizo na changa moto zake. Na nyinginezo huenda  zikageuka kuwa za kheri ikiwa watabakia kuwa katika ucha Mungu. Allaah Ndiye Mwenye Kujua ya ghaibu.

 

Jambo ambalo tungependa kuwausia nyote wawili ni mwanzo murudi kwa Allaah Aliyetukuka kwa ajili ya makosa mliyoyafanya. Ombeni msamaha kwa dhati kwa kujiondoa katika maasiya ya kukutana na mengineyo, kujuta na kuazimia kutorudia tena suala hilo. Baada ya kutengana kwa muda wakati huo unafaa utumike kumtaka shauri Allaah Aliyetukuka kwa kuswali Swalaah ya Istikhaarah. Allaah Aliyetukuka Atawatolea uamuzi wa kuendelea na harusi au kusahau mambo ya harusi ili kila mmoja wenu angojee mwingine ambaye wanaweza kufaana katika kuishi pamoja.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

 

 

Share