Mume Anapokuwa Safarini Kwa Muda, Mke Afanyeje Abakie Katika Taqwa Na Stara?
SWALI:
swali: kwa mwanamume aliye safari akaacha mkewe kwa muda wa miaka miwili au zaidi, mke anapokuwa na hisia za kimapenzi anatakiwa kufanya nini na mumewe hayupo?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwa mbali na mumeo ambaye yuko safarini. Hakika hili ni tatizo sugu katika jamii yetu kwa wanawake kuachwa kwa muda mrefu ikiwa mume yuko katika kutafuta maisha kwa ajili ya familia yake.
Tatizo hili haliwezi kutatuliwa bila Imani ya nguvu kwani bila hivyo matamanio yanakuja kwa haraka kwa mwanamke na inabidi apate cha kumtuliza ili aone wepesi wa moyo na mwili. Imani ya Muislamu huzidi na kupungua kutegemea na mambo mengi katika maisha yake. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aayah Zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao. Hao ambao wanashika Swalaah na wanatoa katika yale tunayowaruzuku” (al-Anfaal [8]: 2 – 3).
Kwa hali hiyo, mwanamke au mwanamme ambaye anataka kujitenga na uchu wake ni muhimu afanye mambo yafuatayo:
- Aizidishe Taqwa yake kwa kufanya aliyoamrisha Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Ajiweke katika Ibaadah za faradhi na Sunnah, kama Swalaah, Zakaah, Funga na mengineyo.
- Leta Adhkaar (kumtaja Allaah Aliyetukuka) kwa wingi kwa fadhila zake ni kubwa. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Allaah. Hakika kwa kumkumbuka Allaah ndio nyoyo hutua (hupata utulivu)!” (ar-Ra’d [13]: 28).
- Kuwa na marafiki wema ambao watakusaidia katika kuketi katika wema na njia nzuri. Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amepigia mfano wa rafiki mwema kama kufanya usuhuba na muuza manukato, ambaye ima atakupatia hadiya manukato au atakutia na hivyo kunukia vizuri.
- Katika Ibaadah, Funga ni moja ambayo inashusha sana matamanio ya mwanadamu.
- Ukifikiria kufanya dhambi la uzinzi au dhambi lolote lile, usifikirie tu ukubwa wa dhambi bali fikiria unamkosea nani na utukufu Wake.
- Punguza wakati wa faragha kwa kujishughulisha na masomo ya Dini na kuhudhuria mihadhara ambayo itakupatia moyo wa kuweza kujizuilia kwa kiasi kikubwa.
- Kithirisha kumuomba Allaah Aliyetukuka Akuhifadhi na zinaa na madhambi mengine, kwani Yeye Aliyetukuka Anatusikia na Anatujibu.
- Suluhisho kwa tatizo hili, ni kuzungumza na mumeo akuchukue nawe huko aliko ili muishi pamoja. Hiyo ni dawa kabisa ya tatizo hilo, kuwa pamoja nyinyi wanandoa.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuhafadhi sote na kumuasi hapa duniani ili Atuingishe Peponi Kesho Akhera na Atulinde na madhambi hapa ulimwenguni.
Na Allaah Anajua zaidi.