Kudhania Kila Baya Litokealo Ni kurogwa Itakuwa Ni Shirk?

 

Kudhania Kila Baya Litokealo Ni kurogwa Itakuwa Ni Shirk?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asaalam Aleykum Warahmatulah Wabarakatuh. Nawashkuru sana Al-hidaya kwa website hii.

 

jee kudhani kila baya likutokealo umerogwa ni shirki?na nini hukmu yake?Kwakweli tabia hii ya waislamu wenzangu inansikitisha na mtu ukimuelewesha anakutolea hoja kwa kusema lakini kweli uchawi upo na mashekhe wamethibitisha na anasisitiza kama yeye amerogwa hata kama hana uhakika wala ushahidi.Na kwakweli  watu wengi siku hizi hutumia "excuse" hii kwa kusingizia kila kitu,mtu akiachwa kafanyiwa ubaya aachwe,na cha kusikitisha zaidi imefikia hatua mtu ukija kuposwa ukikataa watu wanakwambia atakuroga yule usiolewe tena madam umemkataa kuna kesi mbili za ndugu zangu wawili wamefanyiwa hivohivo,...SUBHANALLAH...

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hakika hili ni swali muhimu katika jamii yetu ambayo ilikuwa inafaa kabisa isiwe ni yenye kufikiria mas-ala hayo.

 

Ni itikadi na Imani ya kila Muislamu kuwa kila litokealo hutokea kwa kupenda na kutaka Allaah Aliyetukuka. Na ndio kwa ajili ya hiyo Imani kuhusu Qadar inafaa ifahamike na kila Muislamu. Kudhania kila linalotokea ni kwa sababu ya kurogwa inampelekea mtu kuingia katika shirki. Hakika Uislamu haukukataza tu kufanya mabaya bali vitangulizi vya mabaya pia vinamfanya mtu kuingia katika madhambi ya baya hilo. Mfano ni uzinzi, Allaah Aliyetukuka Amesema:

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ 

Na wala msiikaribie zinaa. [Al-Israa’: 32]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akatufahamisha kuwa kila kiungo kinazini, mfano ni macho, masikio, mdomo, mikono, miguu na kadhalika. Na pia kila kinachokupeleka katika zinaa nacho ni kibaya na mtu anapata dhambi kwa hilo.

 

Na hivyo, kukatazwa shirki kunakatazwa pia na vinavyompeleka mtu katika shirki. Mfano ni huko kudhania linalotokea ni ulozi au uchawi pia ni dhambi dogo kuliko ushirikina wenyewe. Hivyo, mtu anafaa aache ili aweze kunusurika katika kuingia kwenye shirki yenyewe.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share