Fidia: Kulipa Fidia Kwa Ajili Ya Asiyeweza Swiyaam
Fidia: Kulipa Fidia Kwa Ajili Ya Asiyeweza Swiyaam
SWALI:
Ni vipi namna ya kutoa vibaba kwa ajili ya mtu asiyeweza kufunga. Unatoa kiasi chote kinachostahili kwa mara moja au unatoa kila siku moja
na kiasi chake?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Fidia kwa mtu asiyeweza Swawm wakati wa Ramadhwaan wala kulipa baada ya Ramadhwaan ni kwamba: Ikiwa mtu ni mgonjwa mtu na anatarajiwa kuwa atapona na hivyo kuweza Swawm itabidi anapokuwa mzima alipe siku alizokula. Lakini ikiwa ni mkongwe au ana ugonjwa asiotarajia kuwa atapata sahali basi itabidi atoe vibaba viwili (nusu pishi) kwa kila siku aliyokula. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika, watoe fidia; kulisha masikini.. [Al-Baqarah: 184].
Aayah hii inatueleza kutoa fidia kwa kutoweza kulipa siku ulizokula kwa kumlisha masikini mmoja kwa kila siku. Hapa unaweza ima ukamwalika masikini aje ale nanyi kwa mwezi mzima wa Ramadhwaan au pia unaweza kuwaalika masikini sawa na idadi ambayo hukufunga.
Fidia ni nusu swaa' (nusu pishi) ambayo ni sawa na vibaba viwili; navyo ni sawa na kilo moja na nusu (1.5kg).
Ikiwa unataka kumpatia chakula unaweza kuchagua kima ambacho unaweza kumpatia masikini au ukakisia mwenyewe chakula cha masikini mmoja kwa siku moja. Kwa mfano ikiwa ni mchele, ngano, tende au chakula maarufu kinacholiwa hapo mnapoishi utatoa kiasi cha kilo moja nusu kwa maskini mmoja.
Na Allaah Anajua zaidi