Amekopa Sana Lakini Hawajui Walipo Aliowakopa, Anaweza Kutoa Sadaqah Kwa Niyah Yao?

 

SWALI:

 

Salaam Aleykum, kwanza mwenyezi mungu awazidishie duniani na akhera, nilikua na swali mimi wakati niko shule nilikua na mtindo wa kukopa sana na sikumbuki kama nimewalipa watu niliowakopa, nimemaliza shule nikaondoka huku nyuma nadaiwa na wanaonidai wanaishi sehemu za mbali na wala sijui kama taweza kukutana nao tena maishani mwangu hata majina yao nimesahau ila nakumbuka tu nadaiwa sana, sasa naogopa sisi wanadamu tunatembea na vifo, sielewi talipaje? Naweza kutoa sadaka nikanuia kwa wanaonidai lkn inshaAlla nikija kukutana nao sita acha kuwalipa ila uhakika huo sina, nisaidieni jamani, tafadhalini naomba mnijibu haraka mnavyoweza naumia kichwa kwa hili.  Salaam Aleykum

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kukopesha sana mpaka unasahau wanaokudai.

Hakika hili si jambo zuri kwa Muislamu kulifanya au kuwa nalo. Uislamu umehimiza sana endapo tunakopeshana tuwe ni wenye kuandikiana au kuandika ili ujue wanaokudai wewe. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama Alivyomfunza Allaah. Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Allaah, Mola wake. Wala asipunguze chochote ndani yake” (al-Baqarah 2: 282).

Hilo ulilofanya ni kosa unatakiwa ujirekebishe na uweke Niyah ya dhati ya kutorudia tena kabisa kosa hilo.

 

Ni vyema kabisa kuona kuwa kulingana na swali lako umejuta sana kwa ulilofanya la makosa na kuwa na Niyah safi na ya dhati ya kurudi katika msimamo wa Dini thabiti. Linalotakiwa ni wewe kufanya juhudi kuweza kupata mawasiliano na wenye kukudai wale unaoweza kuwakumbuka. Mawasiliano yamekuwa sahali sana siku hizi. Jambo la kwanza ni wewe kujaribu kuwasiliana na shule uliyokuwa ukisoma ukiulizia kuhusu nambari ya simu au sanduku la posta za wale waliokukopesha. Ukishazipata ni jukumu na wajibu wako kuwasiliana nao. Ukipata mawasiliano basi utaulizia pesa unazodaiwa nawe utazilipa kulingana na maelewano yenu, baina yako na anayekudai. Ikiwa miongoni mwao wapo wale waliobadilisha sanduku la posta au simu zao, basi wewe utajaribu kuandika majina ya wanao kudai pamoja na pesa zenyewe. Baada ya hapo utawalipa unaowajua na wale ambao huwajui utaomba msamaha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwani ulifanya hayo kwa ujinga na kutojua, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakusamehe lakini kuanzia sasa ujichunge.

 

Ama wale ambao unawajua lakini umekosa mawasiliano nao kabisa hata baada ya kujaribu kila njia unayoweza kuitumia basi utazitoa kwa nia Sadaqah kuwapatia wanaostahiki na thawabu ziwaendee wadai wako.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

Deni La Mtu Asiyejulikana Yuko Wapi

 

Mzigo Wa Mtu Hamjui Yuko Wapi Afanye Nini?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share