Kufanya Haja Ndogo (Kukojoa) Wima Imethibiti Katika Sunnah?

Kufanya Haja Ndogo (Kukojoa) Wima Imethibiti Katika Sunnah?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Alykum Warahmatullah Wabarakatuh. Swali langu ni kwamba Niliskia kuna Hadith ya Aisha radhiya Allahu anha kwamba amesema sijapato kumwona Nabii Swalla Allaahu alyhi wasallam akikojoa wima, na niliwahi kusikia kuwa imethibiti katika hadith kuwa Nabii Swalla Allaahu alyhi wa sallam alionekana akikojoa wima. Naomba kujua nifuate ipi. Jazaakum Allaahu Khayrah

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Hakika katika mas-ala haya zipo Hadiyth tano kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – tatu sahihi na mbili dhaifu. Moja ni kukataa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikojoa kwa kusimama, ya pili ni kuonyesha kuwa alikojoa kwa kusimama na ya tatu akiwa ameketi. Na katika hizo Hadiyth dhaifu ni kukataza kwake kukojoa kwa kusimama na ya pili ni kukemea kwake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kukojoa kwa kusimama ni katika kukengeuka. Hapa twazitaja zote kwa faida ya kila mmoja wetu:

 

 

1-Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliyesema: “Yeyote anayekuhadithieni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikojoa kwa kusimama msimsadiki. Alikuwa hakojoi ila kwa kuketi.” [Ahmad, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah]

 

 

2- Hadiyth ya Hudhayfah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda kwenye jaa la taka la watu, akakojoa kwa kusimama. Mimi nikaondoka, akasema: “Njoo.” Nikarudi mpaka nikasimama kwenye mabega yake, akatawadha na kupangusa juu ya viatu vyake. [Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah]

 

 

3-Hadiyth ya ‘Abdur-Rahman bin Hasnah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Alitoka kwetu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa mkononi mwake ana ngao ya ngozi, akaiweka, kisha akaketi nyuma yake akakojoa kuielekea… [Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah]

 

 

Na zifuatazo ni Hadiyth mbili zilizo dhaifu:

 

1-Imepokewa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kuwa ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikikojoa kwa kusimama. Akaniambia: Ee ‘Umar! Usikojoe kwa kusimama. Akasema: Sikukojoa tena kwa kusimama baada ya hapo. [Ibn Maajah, Al-Bayhaqiy na al-Haakim lakini ni Hadiyth iliyo dhaifu]

 

 

2-Imepokewa na Buraydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Vitu vitatu ni katika kukengeuka: Mtu kukojoa kwa kusimama, kupangusa mgongo wake kabla ya kuondoka katika Swalaah na kupuliza katika sijdah yake.”  [Ameinukuu al-Bukhaariy katika Taariykh yake, al-Bazzaar, na akaikanusha al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy. Na hii imethubutu kuwa ni kauli ya Ibn Mas‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu)]

 

 

Kutokana na Hadiyth hizo, ‘Ulamaa wametofautiana kuhusu kukojoa wima. Kwa ajili hiyo zikapatikana kauli tatu.

 

1. Inachukiza pasi na udhuru wowote: Hii ni kauli ya ‘Aaishah, Ibn Mas‘uwd, ‘Umar (katika riwaayah yake moja) Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhum); Ash-Sha‘biy, Ibn ‘Uyaynah, Abu Haniyfah na ash-Shaafi‘iy.

 

 

2.     Inajuzu daima dawamu: Hii ni kauli ya ‘Umar (katika riwaayah yake ya pili), ‘Aliy, Zayd bin Thaabit, Ibn ‘Umar, Sahl bin Sa‘d, Anas, Abu Hurayrah, Hudhayfah (Radhwiya Allaahu ‘anhum); ni kauli ya Ahmad bin Hanbal.

 

 

3. Ikiwa ni katika sehemu ambayo hairudishi (hauruki) mkojo kwake inajuzu na ikiwa unarudi basi haifai: Hii ni kauli ya Maalik, na Ibn al-Mundhir akaiona ni sahihi.

 

 

Baada ya hayo yaliyo juu, tunafupisha maneno kwa kusema kuwa hakuna uharaam wowote wa kukojoa kwa kusimama ikiwa mkojo hautarudi au kumrukia mwenye kukojoa ila ni bora kukojoa kwa kuketi. Imaam an-Nawawiy akizungumzia mas-ala haya amesema: “Kukojoa kwa kuketi inapendeza zaidi kwa rai yangu, lakini kufanya hivyo kwa kusimama wima kunaruhusiwa. Matendo yote mawili yamepatikana kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).”.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share