Kulinganisha Vitu Viwili kwa Ubora
SWALI:
assalam alaykum,
nayaleta masuali yangu nikitaraji mafanikio kwanza nihakki kwa muislamu kuuliza mfano wasuali hili? Ni nani ama ipi bora Qur-an ama mtume alayhi swalat was salam? Pili ni nani bora jibril alayhi salam ama mtume alayhi swalat was salam? Tafadhali mutakapo nipa jawabu nipeni kwa dalili ambayo itakua nisilaha yangu
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kulinganisha baina ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Qur-aan au Jibriyl (‘Alayhis Salaam).
Mwanzo tungependa kuelezea kuwa yapo maswali mengine ambayo hayatufaidishi chochote katika Uislamu wetu, Imani yetu na mustakbali wetu Kesho Akhera.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya kuhusu kuuliza maswali mengi kwani kufanya hivyo kunatupeleka pabaya. Amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Hakika waliangamia waliokuwa kabla yenu kwa wingi wa maswali
Maswali mengi ambayo hayana msingi wala faida si vyema katika Dini kwani huenda yakaleta natija mbaya kwa muulizaji. Ndio Allaah Aliyetukuka Akasema:
“Enyi Mlioamini! Msiulize maswali ambayo lau mtafunuliwa, yatawaletea matatizo” (al-Maa’idah [5]: 101).
Hata hivyo, yapo maswali ambayo ni muhimu kwa Muislamu kupata majibu ikiwa kweli anataka kujua ili moyo wake utulie
Ama kuhusiana na maswali yako mawili ni wazi kabisa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni bora kuliko Qur-aan na pia Jibriyl (‘Alayhis Salaam). Hiyo ni kuwa yeye ndiye aliyeteremshiwa Qur-aan na Allaah Aliyetukuka kupitia kwa Malaika Jibriyl ili kuifundisha. Yeye ndiye kiumbe bora kuliko viumbe vyote, ambaye atawaombea watu wahukumiwe na Allaah Aliyetukuka Siku ya Qiyaamah. Na kuonyosha ubora wake wakati wa safari ya Mi‘raaj, ilifika sehemu ambayo Jibriyl alimuambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hapo ndio mwisho wake hawezi kwenda zaidi. Kuanzia hapo Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda peke yake kukutana na Allaah Aliyetukuka. Na yapo mengi mengine matukufu ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanayoonyesha na kuashiria ubora wake ukirejea katika Qur-aan na Siyrah yake utayajua.
Na Allaah Anajua zaidi