Amepoteza Pesa Je, Inapasa Kumshuku Mtu Yeyote?

 

SWALI:

 

Asalamu alaykum,

 

Natumai kwa nguvu za Allah nyote hamjambo.

 

Mimi kwangu naishi na mwanangu wenye miaka kumi (mtoto wa mdogo wangu) na mchumba wangu uwa anakuja kutembea. Miezi miwili iliyopita rafiki yangu alikuja kutembea hapa katika mji wetu, lakini akapata matatizo kidogo na mwenyeji wake, hivyo akaomba hifadhi kwangu. Nimekaa miaka mingi na watu lakini sijawahi kukutwa na jambo hili.

 

Jumatatu 02/11/2009 nimegundua kama dola mia tatu nilizokuwa nimeziweka chumbani kwangu katika wallet, hazimo nimetafuta mpaka leo hii sijazipata. Mgeni wangu huyu amesafiri siku ya Jumanne 03/11/2009 kwenda kwao kusalimia. Nimepanga akirudi niwaulize watu wote ambao wanaingia kwangu na wanaweza kuingia chumbani kwangu. Pia nimepanga wote niwaapishe kwamba wayasemayo ni kweli mbele za Mola, na baada ya hapa basi nitashukuru na kutafuta pesa za watu sasa nizilipe.

 

Imekuwa ngumu kwangu kuamini kama pesa zinaweza kupotea ndani ya nyumba? Haijawahi kutokea miaka yote na nimeishi na watu wengi tu ambao si ndugu zangu lakini sijawahi kuona mambo haya. Mwanangu DOLA MIA 3 (US$ 300) atazipeleka wapi? Mchumba wangu nimemuuliza kasema hajachukua, Mgeni wangu sikupata kumuuliza kwani ile siku ya mwanzo nilisema nisiulize labda mimi binadamu nimesahau hivyo niangalie kwanza, kwani mtu mwingine ukimuuliza ndiyo ingekuwa uhasama. Lakini kwa sasa sina jinsi lazima nimuulize!!!!!

 

JE NINAYOTAKA KUFANYA NI SAHIHI? JE NINYI MNAUSHAURI WOWOTE KWANGU? WABILAHI TAWFIQ.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kupotea pesa chumbani kwako.

Hakika ni kuwa mwanaadamu ameumbwa katika maumbile ya sahau, papatiko na pia uharaka wa kuamua mambo – mema na mabaya. Kuhusu hilo lililotokea yumkinika pia kuwa umepoteza nje na hukufika nazo nyumbani kwako au umezipoteza nje.

‘Alaa kulli haal, ikiwa pesa zimechukuliwa kweli chumbani kwako wale ambao unatakiwa kuwauliza ni wale wenye kuingia kwenye chumba hicho. Wala huwezi kusema mtoto wangu wa miaka kumi hawezi kuchukua. Pia naye anaweza kuchukua bila ya wasiwasi. Hilo ni kuwa mara ngapi tumepata kusikia jinsi gani mtoto alichukua pesa za baba yake zilizo nyingi akaenda akazitumia pamoja na marafiki na huku anajificha. Unaweza kuchunguza hilo kwa kuwauliza marafiki zake walio watoto kama yeye kama walikuwa wakipewa vitu na mtoto wako. Hiyo pia inategemea na tabia za mtoto wako zikoje.

 

Kabla ya kumuuliza huyo mgeni wako unatakiwa ujibu swali hili: Je, mgeni wako alikuwa amepewa ruhusa nawe kuingia chumbani mwako? Na je, alikuwa akiingia ukiwa upo? Ikiwa jawabu ndio basi una haki ya kumuuliza lakini kwa njia iliyo njema na nzuri ili msiharibu uhusiano kwa kitu ambacho huenda hata hakufanya.

 

Hayo ambayo umeamua kuyafanya hayana neno isipokuwa ni vyema kuwauliza bila ya kuwaapisha na ukaswadiki wanayoyasema. Ikiwa hakupatikana mtu basi fanya subira na Allaah Aliyetukuka Atakulipia yaliyo mema na mazuri kuliko hizo pesa.

 

La mwisho ni nasaha kwako ndugu yetu kwani katika suala lako umesema kuwa una mchumba ambaye anakutembelea. Ikiwa kama tulivyoolewa mchumba, ni kuwa yule uliyemposa na una maandalizi ya kumuoa. Na kama ni hivyo, basi fahamu kuwa hairuhusiwi wewe kuwa na ukaribu au kutembeleana na mchumba wako. Hilo ni jambo lisilofaa na ikiwa tena anakuja na kukaa chumba kimoja na wewe hilo ni haraam na pia unatoa picha mbaya kwa mwanao huyo wa miaka 10 pindi akijua kuwa hilo haliruhusiwi litamfanya apoteze heshima na wewe na pia utakuwa unamfundisha kuwa na mahsiano na mwanamke ambaye hajamuoa.

Unaruhusiwa kumtembelea huyo mchumba akiwa kwa wazazi wake na ukiwa pamoja nao na si faragha wewe na yeye. Kumbuka mnapokuwa wawili faragha basi watatu wenu ni Shaytwaan ambaye kazi yake ni kuwashawishi mfanye maovu na maasi.

 

Na ikiwa huyo mchumba si yule uliyemposa bali ni yule anayejulikana kikafri ‘girl friend’, basi hiyo ni haraam kabisa na maovu yasiyofaa kufanywa na Muislamu. Kwa hiyo kumbuka kuwa usije ukawa unalalamika na pesa zilizoibiwa na hali wewe unamuibia Allaah haki Zake za utiifu na kwenda kinyume na maamrisho Yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share