Mwanamume Kuvaa Pete

 



SWALI:

Assalaam aleykum

KUVAA PETE: NINGEPENDA KUPATA JAWABU LA SWALA HILI "JEE, MWANAMME KUVAA PETE INAKUBALIKA KATIKA UISLAM"

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 Shukrani kwa suala lako hili ambalo huenda likawa linawatatiza wengi au baadhi.

Mwanamme Muislamu hakatazwi kuvaa pete ingawa si jambo la Sunnah kama wanavyodhania wengi kwa kujua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) alikuwa akivaa. Ni jambo lenye kuruhusiwa tu ikiwa mtu anataka kuvaa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) alikuwa havai kwa mapambo bali alikuwa akiitumia kama muhuri wake katika barua alizokuwa akiwaandikia watu mbalimbali.

Labda swali linaweza kujitokeza, je Muislamu mwanamme anafaa kuvaa pete aina gani au yoyote? Jibu la haraka ni: Hapana! Dalili yetu kuhusu hili ni zifuatazo:

 

1-     Amesimulia Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa pete ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa ya fedha yenye kijiwe cha Habasha ndani yake (Muslim).

2.     ¨ Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) anahadithia tena: “Wakati mmoja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliandika barua au alikuwa na wazo la kuandika barua. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliambiwa kuwa wafalme hawaandiki barua mpaka ziwe na muhuri. Kwa hiyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya pete ya fedha iliyoandikwa ‘Muhammad RasuluLlaah – Muhammad Mjumbe wa Allaah’. Kama ninaangalia mng’aro wake mweupe mkononi mwa Mtume” (al-Bukhaariy).

3.      Amesimulia Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) alikuwa na pete ya fedha ambayo alikuwa anaivaa. Baadaye ilivaliwa na Abubakar, kisha ‘Umar na baadaye ‘Uthmaan mpaka ilipoanguka katika kisima cha Aris (al-Bukhaariy).

Pete isiyofaa kwa Muislamu mwanamme kuvaa ni ya shaba ya njano, chuma na dhahabu. Makatazo hayo ni kwa mujibu wa Hadiyth za bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam).

1.      Anasimulia Buraydah bin al-Haasib (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla ALlaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amevaa pete ya shaba ya njano. Alimwambia: “Kwa nini nasikia harufu ya masanamu kwako?” Hivyo, aliitupa hiyo pete, akaja baadaye akiwa amevaa pete ya chuma. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) alimwambia: “Vipi nakuoa umevaa mapambo ya watu wa motoni?” Yule mtu aliitupa (hiyo pete) kisha aliuliza: “Ewe Mtume wa Allaah! Ni kifaa gani nitumie?” Akasema: “Tengeneza pete ya fedha, lakini wizani wake usizidi mithqaal moja” (Abu Daawuud).

 2.   Al-Baraa’ bin ‘Aazib (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  ametuamuru   mambo  saba na ametukataza saba. … na ametukataza kuvaa pete ya dhahabu …”

         (al-Bukhaariy na Muslim).

Tanbihi: ikiwa pete yako ya fedha ina maandishi ya jina la Allah au jina lolote katika majina ya Allaah inafaa unapoingia chooni uwe ni mwenye kuivua na kuiacha nje kama alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam).

Na Allah Anajua zaidi

 

Share