Mume Kumaliza Haja Yake Kabla ya Mkewe Katika Kujimai

SWALI:

 

 Asalam alaikum dungu zangu

 

BISMILLAH RAHMAN RAHM

 

Hamujabo nashukuru sana kupata site hiyi niliupata wakati wa ramadhan kwa hivyo namushukuru MOLA wangu kuniezisha kwipata na na washukuru enyi jama muliyo fuguwa hiyi program.

 

Na swali moja hilo swali ni la ayibu lakini lazima niyaseme nimeolewa karibuni lakini tangu nimeolewa mume wangu hajawai kunipa nimalize yeye akisha maliza nikwisha nikijaribu kumwabiya haifai kwa deen umalize peke yako na mke wangu ukamuwacha hajamaliza anakasirika nakunitokana matusi nakusema eti tuwachane. Narudiya kwa swali langu ni haki miye kuwoba talak yangu? INSHALLAH NAGOJA JIBU KWAHARAKA

 

ASALAM ALAIKUM

ME DUNGU WENU KUTOKA ****** LAKINI MUZALIWA YA *****

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mumeo ambaye ana tatizo la kumaliza haraka katika kitendo cha ndoa baina yenu.

Kitendo cha ndoa ni ‘amali ya kushirikiana baina ya wanandoa ili kuleta furaha na mapenzi ya dhati kwa kila mmoja.

 

Kwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana pale aliposema:

Dini ni kupeana nasaha njema” (Muslim), hatuna budi sisi kukunasihi wewe kwa njia iliyo bora ili uweze nawe kumnasihi mumeo. Na tawfiki ya kila kitu inatoka kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Mwanzo kabisa kama mke shughuli zako zinatakiwa ziwe ni kuweza kuiokoa ndoa yako na mumeo ili mpate kuishi pamoja katika umri wenu. Kwa ajili hiyo inatakiwa utafute wakati muafaka wa kuzungumza na mumeo kuhusiana na shida aliyo nayo – ya kumaliza mapema katika tendo hilo la ndoa. Wakati huo unapoupata, na fahamu hautakuwa baada ya tendo la ndoa bali utakuwa ni wakati wa faragha baina yenu ambapo mtakuwa mnazungumza mambo tofauti na hilo litakuwa ni mojawapo. Jaribu katika mazungumzo yako kuwa makini, usiwe ni mwenye hasira bali mcheshi ili aone ni jambo tu na kutakiana kheri na mema. Huenda suala hilo akalipokea kwa njia nzuri au kinyume chake. Ikiwa hatalipokea hilo kama ilivyo baada ya tendo la ndoa, basi kuwa makini vile vile wala usikasirike kwani kukasirika kwako ni kumpatia nguvu mumeo pamoja na Shaytwaan.

 

Njia hiyo ikishindikana basi tafuta njia ya pili ya kumpatia vitabu vinavyohusiana na namna wanandoa wanatakiwa waingiliane katika muono na msimamo wa Kiislamu. Mfano ni Adabu za Ndoa na kitabu hicho unaweza kukipata katika Alhidaaya au mawaidha yanayohusiana na mafundisho ya Uislamu kuhusiana na hilo. Na mawaidha hayo pia unaweza kuyapata katika tovuti ya Alhidaaya.

 

Ikiwa njia hiyo ya pili pia umeitumia bila ya mafanikio itabidi uitishe kikao baina yako, mumeo, wazazi au wawakilishi wa mumeo na wale wako. Katika kikao hicho inabidi uelezee tatizo wazi wazi ili upatikane ufumbuzi wa tatizo hilo. Ikiwa kweli Niyah yenu nyote wawili ni kutaka suluhisho Allaah Aliyetukuka Atawatolea njia ya kupatikana kwa masikilizano baina yenu.

 

Ikiwa njia hiyo ya hapo juu pia haikupatikana itabidi suala hilo mlipeleke kwa Qaadhi ambaye atawasikiliza na kutoa uamuzi muafaka kulingana na Uislamu. Hapo kwa sababu ya shida hiyo aliyo nayo mumeo atakuwa ni mwenye kulazimishwa kukutimizia haja zako za kimwili na ikiwa atashindwa basi Qaadhi huyo huyo atakuwa ni mwenye uwezo wa kuivunja ndoa hiyo.

 

Mara nyingi wanandoa huingia katika Sunnah hii kubwa bila kujua wajibu na haki zao, hivyo kuleta tatizo kubwa baina yao wanapokuwa ni wenye kuishi pamoja. Mume kutoweza kumtimizia mkewe haja zake za kimwili ni sababu tosha kwa mke huyo kuomba talaka kupitia kwa Qaadhi au mume mwenyewe anapoona labda hajiwezi akampatia talaka mkewe au akajaribu kutafuta ushauri wa Kidini kuhusiana na tatizo hilo au matibabu kwani mara nyingine huenda ikawa ni ugonjwa.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Mume Ana Tatizo La Kumaliza Kabla Ya Mkewe Kwenye Tendo La Ndoa

 

 

Ikiwa Hawaridhiani Katika Kitendo Cha Ndoa Wafanye Nini?

 

Vitabu hivi hapa vitawasaidia:

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika (Aadabu Az-Zafaaf Fiy As-Sunnat Al-Mutwahharah)

 

Na video hizi pia:

 

JUMA AMIYR - Chumba Cha Ndani Cha Mtume - 1

JUMA AMIYR - Chumba Cha Ndani Cha Mtume - 2

 

 

 

Tunawaombea muafaka katika kutatua tatizo hilo mlilonalo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share