Mwanaume Kajibadilisha Maumbile Kuwa Mwanamke, Akajiita Na Jina La Kinaswara; Anafaa Kuswaliwa Baada Ya Kufa?

SWALI:

 ASSALAM ALEYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATU

Ningependa kupata ufafanuzi wa swala lililotokea TANZANIA wiki iliyopita Mwezi huu wa Tano kwa Mwaka wa Kirumi.

Swala linyewe ni MWANAUME kubadili jinsia na kuwa mwanamke, na alipofariki Taasisi inayowaongoza Waislamu katika nchi hiyo ikasema ana haki zote za kuzikwa Kiislamu na wakaenda kumswalia sala ya maiti Msikitini. Isitoshe huyu mtu baada ya kubadili jinsia yake alijiita VICTORIA (Aunt Vick). Swali langu je Uislamu unasemaje kuusiana na swala kama hili?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mwanamme aliyebadilisha jinsia yake.

Ni haramu kwa Muislamu kubadilisha jinsia baada ya yeye kuumbwa kwa umbile bora na Allaah Aliyetukuka.

Ni makosa makubwa kwa Muislamu kubadilisha umbile aliloumbiwa nalo Allaah Aliyetukuka. Huko ni kumtoa makosa muumbaji ambaye ndiye Mjuzi wa kuumba na kufanya kila kitu hapa duniani na katika ulimwengu mwengine ambayo bado hatuujui. Kufanya hivyo ni kosa kusikomtoa mtu katika Uislamu.

Jambo la pili ulilouliza halina maelezo ya kutosha, hata hivyo, ikiwa baada ya kubadili kwake maumbile akabadili jina lake na kubadili Diyn au baada ya hapo akawa anaukebehi na kuutusi Uislamu, basi kwa hali hizo za kuritadi na akatoka katika Diyn ilikuwa haifai kwake kuswaliwa na Waislamu wala taasisi yoyote ya Kiislamu.

Ama ikiwa alibaki katika Diyn katika uasi wake huo wa kubadili maumbile yake, basi atakuwa na makosa mbele ya Allaah Aliyetukuka akiwa bado ni Muislamu na ataweza kuswaliwa na kuzikwa. Lakini viongozi wa Diyn wanatakiwa wasishiriki katika mazishi yake ili liwe funzo kwa wengine baada yake kutofanya tendo la kishaytwaan kama hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share