Swali Ambalo Shia Yeyote Hawezi Kulijibu
Swali Ambalo Shia Yeyote Hawezi Kulijibu
Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)
Al-Hasan bin ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikubali kujishusha na kumuachilia Mu’awiyah bin Abi Sufyaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) awe Khaliyfah wa Waislamu. Ingawaje alikuwa na uwezo wa kuendeleza mapambano na jeshi la Mu’aawiyah kutokana na jeshi kubwa alilokuwa nalo la watu wa Madiynah na Waislamu wengine waliokuwa tayari kupigana kwa ajili yake.
Upande mwingine ndugu yake Al-Husayn bin ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alitoka akiwa na jeshi dhaifu lenye watu wachache sana kwa ajili ya kupambana na majeshi ya Yaziyd, ingawaje alikuwa na uwezo wa kufanya amani naye.
Kutokana na Itikadi ya Shia, mmoja kati ya ndugu wawili hawa (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa upande wa haki, na mwingine hakuwa upande wa haki.
Ikiwa Al-Hasan alikubali kujishusha na kumuachilia Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Ukhalifah, hali ya kuwa alikuwa na uwezo wa kupambana naye - alikuwa upande wa haki; basi kule kutoka kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akiwa hana nguvu wala uwezo wa kupambana na majeshi ya Yaziyd juu ya kuwa angeweza kuzungumza na kufanya amani naye hakuwezi kuwa upande wa haki.
Ikiwa Mashia watasema kuwa kitendo cha Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni makosa, basi itabidi pia waseme kuwa Uimamu wake nao ni makosa. Iwapo wakiutia makosa Uimamu wake, itabidi wautie makosa pia Uimamu wa baba yake na umaasumu wake (kuwa hawezi kufanya makosa). Kwa sababu yeye ndiye aliyeusia kutawazwa kwake, na Imaam asiyekosea hawezi kutoa usia ila kwa Imaam asiyekosea (maasum) kama yeye.
Ama Mashia wakisema kuwa kitendo cha Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni makosa, itabidi wakubali pia kuwa Uimamu wake ni makosa na pia ile imani yao kuwa Imaam hatendi makosa nayo pia ni makosa. Kwa ajili hiyo utabadilika Uimamu wa watoto wake wote na vizazi vyake vyote, kwa sababu yeye ndiye asili ya Uimamu wao na kwa njia yake umepatikana mlolongo wa maimamu hao.