Ghadiyrul Khum: Katika Qur-aan, Sunnah Na Historia

Ghadiyrul Khum  Katika Qur-aan, Sunnah Na Historia

 

Imetarjumiwa Na Muhammad Faraj (Rahimahu Allaah)

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

Mashia wanasema kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyestahiki kuwa Khalifa wa Waislam na si Abu Bakr wala ‘Umar wala ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Hoja zao wanaziegemeza katika baadhi ya Hadiyth zilizomo katika vitabu vya Ahli Sunnah [Al-Bukhaariy na Muslim], na mojawapo ya hoja hizo ni Hadiyth hii ya Ghadiyr al-Khum.

 

 

Kabla hatujaanza inatubidi tuelezee kwanza kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mume wa binti yake Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mwanamke bora kupita wote Peponi, na yeye pia ni bin ammi yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye pia ni Khalifa wa nne muongofu wa Waislamu na kwamba sifa zake njema tunazijuwa vizuri.

 

 

Hata hivyo, hapa hatuzungumzi juu ya utukufu wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu sote tunauelewa vizuri, lakini hapa tunazungumza juu ya Hadiyth ya Ghadiyr al-Khum kuwa ni dalili yakuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyestahiki kuwa Khalifa wa mwanzo.

 

 

Hebu tuisome kwanza Hadiythi hii kutoka katika kitabu cha Sahih Muslim kitabu cha Hadiyth nambari 36 kitabu cha fadhila za Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

Imepokelewa kuwa Yazid bin Hayyaan amesema:

“Nilikwenda pamoja na Huswayn bin Sabra na ‘Umar bin Muslim kumtembelea Zayd bin Arqam, na tulipokuwa tumekaa pamoja naye Huswain akamwambia Zayd:

 

“Zayd, wewe umebahatika sana, umemuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na umemsikia akihadithia, na umepigana vita vingi pamoja naye, na umesali nyuma yake. Kwa hakika Zayd umebahatika sana. Zayd, hebu tuhadithie yale uliyomsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema.

 

Akasema:

“Ee mwana wa ndugu yangu, Wa-Allaahi umri wangu umekuwa mkubwa na siku zangu zimesogea mbele na nimeyasahau mengi niliyokuwa nikiyakumbuka kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa hivyo nitakachokuhadithia wewe kikubali na nisichoweza kukuhadithia basi usinilazimishe. Kisha akasema:

 

“Siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahi ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama kutuhutubia mahali penye maji panapoitwa Khum baina ya Makkah na Madiynah. Akamtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumpwekesha, akawaidhi na kukumbusha, kisha akasema:

“Enyi watu! Mimi ni mwanadamu, na hivi karibuni anaweza kunijia Rasuli wa Allaah na mimi nikamuitikia, na mimi nakuachieni vizito viwili. Cha kwanza ni kitabu cha Allaah ambacho ndani yake umo uongofu (uongozi) na nuru, kwa hivyo shikamaneni nacho kitabu cha Allaah na mkikamate vizuri”. Akatusisitiza juu ya kitabu cha Allaah na kutupendekezesha nacho. Kisha akasema: “Na watu wa nyumba yangu. Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu.”

 

Huswayn akamuuliza Zayd:

 

“Ni nani hao watu wa nyumba yake ewe Zayd, si wake zake pia katika watu wa nyumba yake?”

Akasema: “Wake zake ni katika watu wa nyumba yake, lakini watu wa nyumba yake (alowakusudia hapa) ni wale walioharamishiwa kupokea sadaka”.

Akasema:

“Ni nani hao?”

Akasema:

“Hao ni watu wa nyumba ya ‘Aliy na watu wa nyumba ya ‘Aqiyl na watu wa nyumba ya Jaafar na watu wa nyumba ya ‘Abbaas”.

Akauliza:

“Wote hao wameharamishiwa Sadaka?”

Akasema:

“Ndiyo”.

 

 

Hadiyth hii imo pia katika vitabu vya At-Tirmidhiy na Ahmad na An-Nasaaiy na Al-Hakim na wengine.

Kutoka katika Musnad ya Imam Ahmad imeandikwa kama ifuatavyo;

 

 

Tumehadithiwa na Ibnu Namir kuwa ‘Abdul-Malik bin Abu Sulaymaan amesema kutoka kwa ‘Attwiyah Al-Awfiy amesema: “Nilimuuliza Zayd bin Al-Arqam nikamwambia kuwa watu wamenihadithia Hadiyth juu ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na wakanambia kuwa wamehadithiwa na wewe juu ya siku ya Ghadiyr al-Khum, na mimi nataka kuisikia kutoka kwako”.

 

Akasema; “Nyinyi watu wa ‘Iraaq mnacho kile mlichonacho”.

Nikamwambia: “Usiwe na wasi wasi juu yangu”.

Akanambia: “Ndiyo tulikuwepo Al-Juhfa na ulipofika wakati wa adhuhuri Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea akiwa ameushika mkono wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

“Enyi watu, hamjuwi kuwa mimi ninawsatahiki zaidi (Awla) Waislamu kuliko nafsi zao?”

Wakasema:

“Ndiyo”.

Akasema:

“Basi mwenye kunipenda mimi lazima ampende na ‘Aliy (man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu).”

Attwiyah akasema:

“Alisema (Allahumma waali man walaahu wa ‘aadi man ‘aadahu) Rabb wangu uwe adui wa atakayemfanyia uadui na umpende atakayempenda?”

 

Akasema:

“Nimekuhadithia kama nilivyosikia.”

 

Kauli ya kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema; ‘Man kuntu mawalahu fa ‘Aliy mawlaahu’ ‘Basi mwenye kunipenda mimi lazima ampende na ‘Aliy’, ingawaje haimo katika Sahih Muslim lakini baadhi ya wanavyuoni wamesema kuwa ziada hii ni sahihi.

 

 

Ama ile ziada ya ‘Allahumma waali man waalahu wa ‘aadi man ‘aadahu’ Rabb wangu uwe adui wa atakayemfanyia uadui na umpende atakayempenda” na ziada nyenginezo, ingawaje baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa ni sahihi, lakini ‘Ulamaa wengi wa Hadiyth wanasema kuwa ziada hii ni maudhui. Yaani maneno ya uongo yaliyozidishwa.

 

 

Hadiyth hii inatumiwa na Mashia katika kuthibitisha kuwa ‘Aliy ndiye Khalifa baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwamba neno ‘mawlaa’ maana yake ni ‘waali’ yaani kiongozi, na kwa ajili hiyo tukio hili lina maana kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapa anawaambia Waislamu kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ndiye atakayekuwa khalifa baada yake.

 

 

Huu ndio ushahidi wao katika Hadiyth hii, kwa hivyo tofauti iliyopo ni katika kulifasiri neno ‘man kuntu mawlahu fa ‘Aliy mawlahu’. Mashia wanasema kuwa maana ya maneno haya ni kuwa ‘man kuntu Waliyyahu fa ‘Aliy Waliyyahu’, lakini Masunni wanasema kuwa neno hili maana yake ni mapenzi na uhusiano mwema.

 

 

Katika lugha ya Kiarabu, neno ‘Muwalaat’ ni kinyume (opposite) ya neno ‘Mu’adaat’ na ushahidi unapatikana katika ziada ya mwanzo; ‘Rabb wangu mpende atakayempenda na uwe adui wa atakayemfanyia uadui’.

 

 

Kwa hivyo hapa tunazungumza juu ya ‘Muwalaat na Mu’adaat’, yaani ‘Kupenda na Uadui’, yanayohusiana na watu kumpenda ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Kabla hatujaendela mbele, kwanza hebu tuzungumze juu ya sababu iliyomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusema maneno hayo.

 

 

Mashia wanasema kuwa; Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimamisha watu mahali hapa wakati wa joto kali, na wanasema kuwa idadi yao inafika watu mia moja elfu, na wanasema kuwa hapa ndipo mahali wanapokusanyika Mahujaji wote, na sababu kubwa ya kuwakusanya watu hao ni kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kuwaambia watu kuwa; ‘Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu’, pamoja na maneno mengine waliyoongeza.

 

 

Sababu ya kweli iliyomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusema maneno haya ni hii ifuatayo;

 

 

Anasema Al Bayhaqi kutoka kwa Abu Sa’iyd kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwakataza Swahaba (alokuwa nao safarini walipokuwa wakirudi kutoka nchi ya Yemen) wasiwapande ngamia wa sadaka, kisha akamchagua mmoja wao awe kiongozi na yeye akaondoka na kwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aliporudi akaona kuwa kiongozi wao aliwaruhusu kuwapanda ngamia. Alipoona hivyo, ‘Aliy akakasirika na kumlaumu kiongozi wao. Na riwaya nyingine zinasema kuwa aliwakataza kuvaa nguo lakini wao wakazivaa. Anasema Abu Sa’iyd kuwa; tuliporudi Madiynah tukamhadithia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukali wa ‘Aliy juu yetu, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

 

“Acha kusema ee Sa’ad bin Maalik baadhi ya maneno yako juu ya ndugu yako ‘Aliy, kwani Wa-Allaahi ninavyoelewa mimi ni kuwa (‘Aliy) amefanya mema mengi katika njia ya Allaah”.

 

(Anasema Ibn Kathiyr kuwa Hadiyth hii ni njema kwa masharti yaliyowekwa na An-Nasaaiy). Na Hadiyth hii pia imetolewa na Al-Bayhaqiy na wengine.

 

 

Anasema Ibn Kathiyr kuwa malalamiko ya wanajeshi yalipoongezeka baada ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwakataza kuwapanda ngamia wa sadaka na kuwanyang’anya nguo mpya walizoruhusiwa kuzivaa na msaidizi wa ‘Aliy, na Allaah ndiye anayejuwa zaidi, basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akirudi kutoka katika hija yake na baada ya kumaliza shughuli zote zinazohusiana na hija hiyo, na alipokuwa njiani kuelekea Madiynah, alipopita mahali panapoitwa Ghadiyr al-Khum akainuka na kuwahutubia watu akamtetea ‘Aliy, na kuinyanyua heshima yake na akawatanabahisha watu juu ya fadhila za ‘Aliy na pia kuwajulisha juu ya mapenzi yake kwa ‘Aliy na uhusiano uliopo baina yake na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), yote haya kwa ajili ya kuondoa yale yaliyoingia katika nyoyo za watu wengi dhidi ya ‘Aliy.

Al-Bidaayah wan-Nihaayah (5/55).

 

 

Na hii ndiyo maana Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaichelewesha hotuba yake mpaka walipokuwa karibu na mji wa Madiynah na hakuwahutubia pale walipokuwa Makkah wakati wa Hija.

 

 

Siku ya kusimama ‘Arafah, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahutubia mahujaji wote, lakini hakulizungumzia jambo hili kabisa, na baada ya kumaliza hotuba yake akawauliza watu:

 

“Nimeufikisha ujumbe?”

Watu wakajibu:

“Ndiyo (umeufikisha)”

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Rabb wangu shuhudia”.

 

Kwa ajili gani basi Rasuli alichelewesha khutbah yake juu ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mpaka walipokuwa wakirudi, tena karibu na mji wa Madiynah?

 

Kwa sababu wale waliokuwa wakisikitika juu ya ‘Aliy walikuwa ni watu wa Madiynah, wale waliokwenda naye vitani, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalizungumzia jambo hili walipowasili mahali panapoitwa Ghadiyr al-Khum katika mji wa Juhufa, mji uliopo kilomita 250 mbali na mji wa Makkah.

 

 

Ukiiangalia ramani iliyopo chini utaona kuwa si kweli yale maneno yanayosemwa kuwa mahali hapo (Ghadiyr al-Khum) ni mahali wanapokusanyika mahujaji.

 

 

Mahujaji wanakusanyika mji wa Makkah na wanaondokea huko huko Makkah. Mahujaji hawakusanyiki mahali penye umbali wa kilomita 250 kwa ajili ya kuondoka Makkah baada ya kumaliza shughuli za Hija, kwani watu wa Makkah wanabaki huko huko Makkah, na  watu wa Twaif wanakwenda Twaif, na watu wa Yemen wanakwenda zao Yemen na watu wa Al-Kuufa wanakwenda Al-Kuufa na hivi ndivyo ilivyo, na watu wa makabila mbali mbali wanaelekea makwao, na watu waliobaki na kufuatana na msafara wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wale tu watu wa Madiynah na wale wanaopita njia hiyo wakielekea makwao, na hao ndio ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza nao aliposema;

 

Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu”.

 

 

Isitoshe khutbah hiyo haikuwa juu ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yake, ingawaje Ali anastahiki hotuba nyingi, isipokuwa katika hotuba hiyo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza pia juu ya Qur-aan na umuhimu wake na akawakumbusha watu pia juu ya kuwapenda watu wa nyumba yake (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha akawatanabahisha watu juu ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 Maana Ya Neno (Mawlaa) 

 

Anasema Ibn al-Athiyr kuwa neno Mawlaa maana yake ni;

Mwenye kumiliki,

Mwenye kusaidia,

Mwenye kuwaacha huru watumwa,

Msaidizi,

Mpenzi,

Mtumwa aliyeachwa huru (kwa mfano Zaid (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anaitwa ‘Mawlaa wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)’,

Bin Ammi,

Na pia Mtoto wa mjomba na shangazi.

Yote haya katika lugha ya Kiarabu yanabeba maana ya neno hili ‘Mawlaa’.

 

Na Hadiyth hii haina ndani yake dalili yoyote ile ya kuchaguliwa kwa Imam, kwa sababu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angekuwa amekusudia kumchagua Khaliyfah atakayetawala baada yake, basi asingetamka neno linaloweza kubeba maana zote hizo, bali angetamka neno linalobeba maana moja tu. Angelisema kwa mfano;

 

“’Aliy ndiye Khalifa wenu baada yangu”, au “Nikifa mimi basi msikilizeni na mtiini ‘Aliy bin Abi Twaalib”.

 

Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ufasaha wake katika lugha ya Kiarabu hakutamka lolote katika maneno haya yaliyo wazi kabisa na badala yake akasema;

 

Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu

 

Allaah Anasema;

مَأْوَاكُمُ النَّارُ ۖ هِيَ مَوْلَاكُمْ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿١٥﴾

Makazi yenu ni moto, hayo ndio yanayostahiki kwenu, na ubaya ulioje mahali pa kuishia. [Al-Hadiyd: 15]

 

 

 

Katika Aayah hii Allaah Anauita moyo kuwa ni ‘mawlaa’, kwa sababu ya kukamatana nao sana na watu wa motoni.

 

 

Ningependa pia kuwatanabahisha wasomaji kuwa neno ‘mawlaa’ linakhitalifiana na neno ‘waliy’, kwani haya ni maneno mawili tofauti.

 

 

Neno ‘waliy’, (kwa kasrah) asili yake linatokana na neno ‘wilaayah’ na maana yake ni ‘Uongozi’, ama neno ‘mawlaa’ linatokana na neno ‘walaaya’, (kwa fat-hah) na maana yake ni ‘kupenda’, na ‘kusaidia’.

 

Allaah Anasema;

 

فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ مَوْلَاهُ ﴿٤﴾

basi hakika Allaah Ndiye Mlinzi Msaidizi wake). [At-Tahriym: 4]

 

Katika kuifasiri Hadiyth hii ya Zayd, anasema Imam ash-Shaafi’iy;

 

“Kilichokusudiwa hapo ni mapenzi ya Kiislamu, kama Alivyosema Allaah;

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ مَوْلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَأَنَّ الْكَافِرِينَ لَا مَوْلَىٰ لَهُمْ﴿١١﴾

Hivyo ni kwa kuwa Allaah ni Mlinzi, Msaidizi wa wale walioamini na kwamba makafiri hawana mlinzi. [Muhammad: 11]

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelitumia neno hili ‘mawlaa’ mara nyingi na si kwa ajili ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yake. Katika Hadiyth ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Makabila ya Quraysh na Answaar na Juhaynah na Muzaynah na Aslam na Ghifaar na Ashja-a wote ni wasaidizi wangu (mawaalii – wingi wa neno mawlaa) na hawana mlinzi mwingine isipokuwa Allaah na Rasuli wake”.

Al-Bukhaariy Volume 4, Book 56, Hadiyth nambari 715 na imetolewa na wengine pia.

 

 

Ipo mifano mingi ya aina hiyo, lakini iliyotajwa hapo juu inatosha kuwa ni dalili.

 

 

Ni muhimu pia kuzingatia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutumia neno ‘baada yangu’, pale aliposema:

 

Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu”.

 

 

Alitamka maneno hayo bila kuweka wakati maalum, hii ikimaanisha kuwa amri hii haina wakati maalum na kwa ajili hiyo ikiwa kusudi ya hotuba yake ni kuwaambia watu kuwa ‘Yeyote aliye chini ya uongozi wangu basi na Ali ni kiongozi wake’, kama wanavyofasiri Mashia, kwa hivyo patakuwa na tatizo kubwa, kwani maneno haya yataleta maana kuwa wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa na viongozi wawili wenye kuuongoza ummah, jambo lisiloingia akilini.

 

 

Bila shaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukusidia hivyo na wala Swahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hawakufahamu hivyo, ama sivyo pangekuwa na fitna kubwa wakati ule.

 

 

Hata hivyo kuwepo kwa ‘mawlaa’ wawili au zaidi kwa maana ya wapenzi au wasaidizi ni jambo linalowezekana, yaani kumpenda na kumsaidia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia kumpenda na kumsaidia ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakati mmoja.

 

 

Kutokana na yote haya tunaelewa kuwa Hadiyth hii ya Ghadiyr al-Khum haina uhusiano wowote wa nani atakayekuwa kiongozi baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini wakati huo huo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatujulisha kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni kipenzi chake na kwamba anatutaka sisi tumpende pia na tumnusuru.

 

 

Tunamuomba Allaah atufufuwe pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pamoja na ‘Aliy na pamoja na Swahaba wote watukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Share