Anamtaka Kijana Amuoe Lakini Hajui Aamue Vipi?

 

 
SWALI:
Assalam alykum warahmatullahi wabarakatu shukran kwanza kwa kazi yenu murwa ALLAH (subhanahu wataallah) awabariki na atujalie tuwe wenye kuupokea uongofu ameen ama kuhusu swali langu ni kuwa pana shabab ambaye ni muumin na dhamira yake ilikua kuoa, kwa kuwa ashaafikia, sasa dada wa mamake aliyekuwa anaishi nae wakiwa pamoja na mume wake wakamwashiria kijana huyo wao kwangu, lakini rijali huyu hakupiga hatua yoyote kuhusu swala hilo la kuashiriwa kwangu, basi kwa vile mimi na wao ni majirani, na yule mama nina uhusiano mzuri nae wakijirani mimi huenda sana hapo kwao kuwajulia hali nikipata muda, na niliwahi kusikia mara kadha wakinitaja bila kunihusisha hadi siku, akanambia kama utani, hutaki nikuoze mwanangu, nami sikuchukulia sana jambo hilo uzito, baada ya muda hivi nikawa simuoni rijali yule pale nyumbani kwa halati yake, bahati nikakutana na kakake nikamuuliza akanieleza kuwa kwa ajili ya kazi yuko mjini, basi nami nikachukua no yake hapo kwa kuwa  nilikua nikimtaja moyoni sana nikawasiliana nae na hapo ndipo pia aliwahi sasa kunieleza kinagaubaga mambo yalivyokuwa pale nyumbani kwao, kuwa walitaka anioe mimi, sasa sababu aliyonipa kwa nini hakupiga hatua ni, alikua hanijui vyema ni kuniona 2, kisha kuna shangazile aliwahi kumwambia kuwa huyu halati yake ana moyo wa huruma na akiona yatima hasa kama mimi nilivyo hutaka amsaidie kivyovyote ili awe pahala pazuri bila kufikiria baadaye mara akuletee balaa pengine ukimuoa, na akanambia pia alikuwa amekwenda mpaka rwanda kwa ajili ya kutafuta mke, ila hakupata, kisha akanambia nikae nifikirie na niwahusie wazee huyu kijana, lakini kila nikitafakari na kupima niliona anapata pressha kwa huyu halati lakini yeye sikumuona na interest, tukakaa muda bila mawasiliano kisha halati na mume wake wakanifuata kutaka kujua nani wali wangu wa haki kuposwa mimi, nikawaambia  kwani babangu yuko hai japo hakunilea kwa ajili ya kutengana, mama ndo alifariki,  lakini  sikufurahia utaratibu huo kwani yule kijana hakuniambia chochote na hakukua na mawasiliano ndipo nikawaambia siko tayari kwa ndoa, basi baada ya muda wa mwezi hivi jambo hili likawa lanizunguka kichwani, na sasa amesafiri tena saudia lakini kikazi , sasa mimi nimekua nikimtumia mail za kukumbushana mema ya kidini kama vile ninavyowatumia ndugu zangu waislamu ambao ninazo adress zao, sasa mawazo ya mimi kuolewa nae yamenijia tena moyoni na sina uhakika nikumbane nalo jambo hili vipi kwani sijamwambia kitu tena na hajanambia kitu ila halati kila akiniona aniuliza, hakuna mabruk yoyote bado, naswali istikhara na nataraji kupata jibu kwa kumtegeme Mola Aliye mjuzi, na pia niliona niwatake ushauri wenu, samahani kwa maelezo yangu marefu ila nimetaka munielewe vyema, je mutanishauri vipi? Jazakallahu kheir
 

 
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihiwasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Kwanza tunakukumbusha kuwa hakutakiwi kwa mwanamke au mwanamme wa Kiislamu kuwa na mawasiliano na jinsia nyingine na hata kufikia kuomba namba ya simu au mawasiliano na asiye Mahram wake. Hali hiyo ni katika zile hali za kukaribia zinaa na haifai inapaswa iepukwe kabisa.
 
Ndoa ni katika ‘Ibaadah nzuri kabisa kwa Muislamu – kwa mwanamme na mwanamke. Na haifai kwa mwanamme kukaa kwa muda mrefu baada ya kubaleghe na ana uwezo naye asioe. Na vile vile mwanamke naye hafai kukataa posa pasi na sababu yoyote ya kishari’ah, kwani kufanya hivyo kunaweza kumtumbukiza Muislamu katika dimbwi la madhambi makubwa ya zinaa.
 
Hata hivyo, mara nyingi hutokea shida kubwa sana kwa wanandoa kwa ajili ya wao kusukumwa kumuoa au kuolewa na asiyempenda. Na kwa ajili ya kuridhishana mnakuja baada ya kuoana kusumbuana na mwisho kuachana jambo ambalo si zuri Kiislamu.
 
Nasaha ambazo tunaweza kukupata ni kuendelea kuswali Swalaah hiyo ya Istikhaarah, na hujatuambia umeona ishara gani kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Ikiwa ishara ni nzuri basi kubali posa ya huyo kijana lakini ikiwa ni kinyume basi achana naye na Allaah Aliyetukuka Atakuletea mwenye kheri nawe katika maisha yako.
 
Ikiwa mpaka sasa hakuna ishara yoyote, anza kuuliza kuhusu huyo kijana, kuhusu utekelezaji wake wa Dini kama Swalaah, Funga na amali nyengine na vile vile tabia yake. Ikiwa ameshika Dini na tabia yake ni nzuri basi tawakali kwa Allaah Aliyetukuka na In-shaa-Allaah, Allaah Atakutilia tawfiq. Na kama sifa hizo mbili hana achana naye. Na kufanya hivyo utapata msaada wa Allaah Aliyetukuka kwa kukutunukia aliye na kheri nawe.
 
Nasaha nyengine ambayo tunaweza kukupa ni wewe kukata mawasiliano uliyonayo hivi sasa na kijana huyo kwani hiyo ni njia ya kujikurubisha na zinaa na kuwemo katika maasi.
 
Tunakuombea kila la kheri hapa duniani na Kesho Akhera.
 
Na Allaah Anajua zaidi
 
Share