Zingatio: Je, Unamuaidhi Mwanao Au Unamuusia Chochote?
Zingatio: Je, Unamuaidhi Mwanao Au Unamuusia Chochote
Raashid Husayn
Mara nyingi mzazi mchaji Allaah hupendelea mwanawe afikiwe na khayr au awe mchaji Allaah kama yeye anavyojitahidi kumcha. Hili ni kwa mujibu wa tamko la Allaah kututahadharisha kwa kutuambia ya kwamba:
إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ ۚ وَاللَّـهُ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿١٥﴾
Hakika mali zenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Allaah kuna ujira adhimu. [At-Taghaabun: 15]
Jambo hili humpelekea kila mzazi kumuwaadhi au kumuusia mwanawe pindi anapokuwa yuko hai au pindi anapoona yupo karibu na kuiaga dunia.
Swali ni kwamba: Je, kila wasia au mawaidha huwafikiana na yale Aliyoamrisha Allaah na Rabb wake (Swallah Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?
Tumsikilize Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) aliwausiaje wanawe?
Allaah Anasema ndani ya Qur-aan ya kwamba:
وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٣٢﴾
Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na (kadhalika) Ya’quwb (akawaambia): Enyi wanangu! Hakika Allaah Amekukhitarini nyinyi Dini; basi msife isipokuwa nyinyi ni Waislamu. [Al-Baqarah :132]
Ni desturi ya watu wema kuusiana mema namna ambavyo Nabiy Ya’aquub (‘Alayhis-salaam) alipousiwa na baba yake Ibraahiym (‘Alayhis-salaam), naye akawausia wanawe kama ilivyokuja ndani ya Qur-aan:
أَمْ كُنتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِن بَعْدِي قَالُوا نَعْبُدُ إِلَـٰهَكَ وَإِلَـٰهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ ﴿١٣٣﴾
Je, mlikuwa mashahidi wakati mauti yalipomfikia Ya’quwb alipowaambia wanawe: Mtaabudu nini baada yangu? Wakasema: Tutamwabudu Ilaaha wako (Allaah) na Ilaaha wa baba zako, Ibraahiym na Ismaa’iyl na Is-haaq; Ilaah Mmoja, nasi ni Waislamu (tunajisalimisha) Kwake. [Al-Baqarah :133]
Labda tunaweza kuleta hoja ya kwamba hao wote walikuwa Rusuli ya Allaah, ndio maana walishikamana na neno la Tawhiyd. Hebu na tumuangalie mja miongoni mwa waja wa Allaah, ambaye alisifiwa kwa kupewa hikmah kubwa, kama Alivyotuonesha Allaah ndani ya Qur-aan ya kwamba ni kwa namna gani alimuaidhi mwanawe?
Luqmaan alimuusia mwanawe mambo yafuatayo:
1) Asimshirikishe Allaah na chochote kile, kwani kufanya hivyo ni dhulma iliyo kubwa.
2) Kuwafanyia wema wazazi wawili hata kama ni washirikina, almuradi asiwatii pindi watakapotaka kumshirikisha Allaah.
3) Jambo lolote lile kubwa au dogo, basi ufahamu kuwa kwa Allaah hakufichiki kitu.
4) Ee mwanangu! Shikamana na Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.
5) Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Allaah hampendi kila anayejivuna na kujifakhirisha.
6) Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyozidi ni sauti ya punda.
Luqmaan alikuwa akimpa mwanawe mawaidha haya ambayo yamefikishwa kwetu kupitia Kitabu chetu Qur-aan, ndani ya Suwrah-Luqmaan, Aayah ya 13-19.
Hitimisho
Shikamana na mwenendo sahihi katika kuwausia na kuwapatia mawaidha wanao pindi uko hai na pindi unapokaribia kufa. Kwani ni moja ya jambo ambalo utafaidika kwa kupata thawabu nalo pindi utakapokuwa umeshakufa, kama ilivyokuja kwenye Hadiyth swahiyh inayosema: “Pindi mwanadamu anapokufa ‘amali zake zote hukatika, isipokuwa kwa mambo matatu: …na mtoto mwema anayemuombea du’aa.” [Imepokewa na Muslim]