Zingatio 7: Yaa Rahiym, Tukubalie Swawm Zetu
Zingatio 7: Yaa Rahiym, Tukubalie Swawm Zetu
Naaswir Haamid
Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu wote, Swalaah na salamu zimshukie kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Yaa 'Aalimal-Ghayb, hakuna mwengine wa kuabudiwa kwa haki illa Wewe. Yaa Rahmaan, heshima zetu zimepunguwa mbele Yako, na wengine walikithirisha madhambi hadi mwezi wa Ramadhwaan.
Tunakushirikisha hali ya kuwa tunajua Huna mshirika. Kwani wapo wengine wamemfanya mwabudiwa kuwa ni Ramadhwaan! Na sasa wanajiandaa kukuasi kwa nguvu mpya. Yaa Rahiym, hatuna uwezo wala nguvu zaidi Yako. Sisi ni dhaifu chini ya dhaifu, hakuna hilla wala uwezo isipokuwa Wako.
Tulikushirikisha asubuhi na mchana ilhali fadhila za Ramadhwaan zilimurika juu yetu. Tumekosa fadhila za kukutambua na kukushukuru kwa Rahmah zako juu yetu. Yaa Maalik! Leo tumeigeuza siku ya ‘Iyd kuwa ni halaal kufanya zinaa na kuigeuza pombe kuwa ‘ibaadah yetu. Vikao vya michezo na kamari ndio miongozo yetu Yaa Qudduws! Wanawake ndio viongozi wetu wanaotembea utupu wa mnyama. Ibliys ndie mwabudiwa wetu wa kutuhadaa. Hatuna chengine ila ‘ibaadah ya kuangalia yasiyofaa. Ramadhwaan imeondoka na tumekuwa ni wenye hasara kubwa, kwani Wewe Ndiye Ujuae nani atamkirimu tena mgeni huyu. Wangapi vipenzi vyetu tulikuwa nao Ramadhwaan iliyopita, na sasa hatunao tena mwaka huu! Yaa Ghafuwr, waghufurie maiti wetu na sisi pia makosa yetu.
Yaa Salaam! Wewe ni Muweza hakuna Mwengine Muweza. Wewe Ndiye Al-Kariym hakuna mwengine kariym zaidi Yako. Yaa Allaah, Tuhifadhi kwa nuru Yako. Tupo mbele Yako Yaa Allaah! Tughufurie maovu tuliyokufanyia asubuhi na mchana Yaa Khaaliq! Usiku tunageuka mbwa asubuhi bina Aadam mnafiki. Ee Muumba wa Mbingu na Ardhi, Muumba wa Jannah na Moto. Tupe ukarimu wako, Hakuna mwengine wa kutupatia usalama zaidi yako. Kama Hujatughufuria Wewe, ni nani mwengine wa kutughufuria Yaa Allaah? Tunatubia madhambi yetu Yaa Allaah kabla ya kufika mbele Yako Ukiwa Umetughadhibikia.
Yaa Mutakabbir! Dunia yetu imejazwa na wanafiki na makafiri. Israafu kwao ndio maadili yao. Wanafiki, Mayahudi na Manaswara wamekuwa ndio jeshi la Ibliys. Basi kwa hakika tunatamka kuwa jeshi Lako ndio kubwa na hamna mfano wake. Basi Yaa Mu-umin Tulinde na Tuhifadhi kutokana na jeshi lako. Tuoneshe njia tupate kuingia ndani ya Pepo Yako. Hakuna Anayejua kuadhibu kuliko Wewe Yaa ‘Aziyz!
Yaa Haakim! Shukrani zote ni zako, Wewe Ndiye Nuru ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Tunakushkuru kwa kuipata Ramadhwaan hii. Yaa Baariu, Yaa Muswawwir, Kwako Ndiye Unastahiki Shukrani. Wewe Ndiye Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Kwako Shukrani zote zinastahiki juu Yako. Wewe Ndiye Mfalme wa mbingu na ardhi. Shukrani zote ni Zako.
Tunaamini kuwa Upo na ahadi Yako ni kweli, kauli Yako ni kweli, Jannah Yako ni kweli, Moto ni kweli, Manabii Wako ni kweli, na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kweli, na Saa ya Qiyaamah ni kweli ipo. Yaa Allaah, Kwako tunajisalimisha, Kwako Tunategemea malipo ya mwezi huu wa Ramadhwaan, Kwako tunaamini, Kwako tunatubu, kwako tunahukumiwa.
Basi tughufurie madhambi yetu yaliyo mbele na yaliyo nyuma yetu. Wewe Ndiye Mwanzo hakuna mwengine kabla yako, Wewe Ndiye wa Mwisho Hakuna mwengine baada yako. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe tu, Wewe ni Rabb Wetu. Hapana mwabudiwa ila ni Wewe tu. Tuongoze njia iliyonyooka Yaa Allaah!
تقبل الله منا ومنكم
Tunamuomba Allaah
Atutakabalie Swawm zetu na
za Waislam wote duniani.
Aamiyn.
‘Iyd Mubaarak