Kufanya Sherehe Ya Harusi Ukitokea Msiba
SWALI
asalaam alaykum
swali langu ni kwamba kama kuna harusi tarehe 5 tarehe 2 ukatokea msiba je ile harusi unawaza kuendelea kuifanya au la?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakuna kipingamizi chochote kisheria kinachokataza kufanyika ndoa katika siku hiyo, si siku hiyo tu ambayo ni ya tatu baada ya msiba, bali hata kama ni siku ya kwanza. Lakini kutokana na hali ya kibinaadam ndio inaweza kuonekana kuwa ni jambo lisilofaa na zito kulifanya. Pamoja na hivyo kisheria ndoa hiyo inaweza kuendelea bila wasiwasi wowote, na haliwezi kusimama jambo la kheri kama hilo kwa tukio lililotokea na ambalo halipaswi kusimamisha harakati na matukio yenye kuendelea.
Tutazame hadithi hizi mbalimbali kuonyesha jinsi Maswahaba walivyokuwa wakikabiliana na misiba na kuweza kuendelea na harakati zao za kimaisha kama kawaida:
Zaynab bint Abi Salama رضي الله عنها anasimulia kuwa amepokea Hadithi tatu zifuatazo. Zaynab anasema nilimtembelea Umm Habibah رضي الله عنها , mke wa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم wakati ambapo babake (Abu Sufyaan bin Harb رضي الله عنه) alikuwa ameaga dunia. Umm Habibah رضي الله عنها aliitisha manukato ya njano, huenda ikawa ni khaluq au kitu chengine. Akampaka nayo kijakazi wake na kisha kujipaka katika uso wake na kusema: Naapa kwa Allah! Sihitaji manukato lakini nimemsikia Mtume صلي الله عليه وآله وسلم akisema, “Si halali kwa mwanamke anayemuamini Allah na Siku ya mwisho kujiepusha kujipamba wakati wa kuomboleza kwa mtu aliyekufa zaidi ya siku 3, isipokuwa kwa muda wa miezi minne na siku 10 kwa kufiliwa na mume. Zaynab رضي الله عنها anasema: Nilimtembelea Zaynab bint Jahsh, mke mwengine wa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم ambaye kaka yake alikuwa ameaga dunia. Aliomba apatiwe manukato na kujipaka. Kisha akasema: “Mimi sina haja ya manukato lakini nimemsikia Mtume صلي الله عليه وآله وسلم akisema kwenye minbar: ‘Si halali kwa mwanamke anayemuamini Allah na Siku ya Mwisho kuomboleza anapofariki mtu zaidi ya siku tatu, isipokuwa kwa miezi 4 na siku 10 kwa anayefiliwa na mumewe” (Al-Bukhariy, Abu Dawud na Maalik).
Imepokewa kwa ‘Aishah رضي الله عنها kwamba Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema: “Si halali kwa mwanamke anayemuamini Allah na Siku ya Mwisho kuomboleza anapofariki mtu zaidi ya siku tatu, isipokuwa kwa anayefiliwa na mumewe” (Muslim).
Imepokewa kwa ‘Aishah na Hafswa رضي الله عنهما , wake za Mtume صلي الله عليه وآله وسلم kwamba Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema: “Si halali kwa mwanamke anayemuamini Allah na Siku ya Mwisho kuwa na huzuni anapofariki mtu zaidi ya siku tatu, isipokuwa kwa anayefiliwa na mumewe” (Muslim).
Kwa dalili hizo, tunapata kujua kiwango cha kuomboleza wakati wa msiba na kuwa baada ya siku hizo tatu mtu anaweza kuendelea na harakati zake za kawaida. Na kuwekwa kiwango hicho cha maombolezi (wa Allaahu A’alam), si zaidi ila kudhihirisha heshima na mazingatio ya tukio hilo. Na vilevile hakuna popote katika sheria za ndoa panapokatazwa kufanyika ndoa wakati panapotokea msiba.
Na hizi siku tatu za maombolezi si kuwa mtu anatakiwa awe ni mwenye huzuni tu na hafanyi chochote. Maombolezi ya msiba huwa nayo mtu anapofiliwa na jamaa au kipenzi chake na anatakiwa katika hata siku tatu za mwanzo aendelee na shughuli zake bila ya pingamizi yoyote.
Na Allaah Anajua zaidi